Taarifa Za Wenye Ulemavu Zikusanywe Kwa Usahihi

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Ni majira ya asubuhi ya Machi 30, 2026 wageni wawili kutoka Ofisi ya Waziri wa Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Mwigulu Nchemba wanafika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, wanaripoti na kisha kueleza kuwa wanafanya mafunzo ya uhuhishaji wa taarifa za walemavu kwa maafisa kadhaa wa mkoa wa Mara wakiwamo maafisa TEHAMA na Maafisa Ustawi wa jamii kutoka kila Halmashauri.

Wageni hawa walifika alipo Mwanakwetu wakiongozana na Richard Magoiga miongoni mwa Maafisa Waandamizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, kisha Mwanakwetu kuambatana nao hadi katika mafunzo hayo katika majengo ya ofisi za Manispaa ya Musoma.

 

Kipenga cha mafunzo haya kilianza huku kwanza ndugu Josephy Humphrey ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kueleza umuhimu wa kuhifadhi taarifa za wenye ulemavu katika mfumo tangu ngazi ya mtaa/kijiji hadi taifa kwa ofisi ya Waziri Mkuu:

“Hizi taarifa zinaonesha mambo kadhaa ikiwamo jina, umri, tarehe ya kuzaliwa, eneo analotoka , kadi yake ya NIDA kama anayo na kama alihamia eneo lingine na hata aina ya ulemavu na kisha mwisho kuonesha aina ya mahitaji yake kulingana na huo ulemavu na haya yote yatajazwa na afisa ustawi wa jamii. Huku vipengele vingine vitajazwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.”

Ndugu Humphrey aliongeza kuwa taarifa hizi zikifanyiwa kazi vizuri walemavu labda wakawa na kadi zao, kisha huduma zikitolewa kwa wakati kama mlemavu atahamia eneo lingine atajua atakosa huduma, hivyo lazima atafika kwa afisa ustawi wa jamii kuhuhisha taarifa zake na hilo nidiyo shabaha ya Serikali kwanza kuwapa kuwatambua walema, kutambua mahitaji yao na kisha kusaidia kupatikana kwa mahitaji yao.

Huku akiongoza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kueleza aina ya ulemavu wa mhusika ili kujua usahihi wa mahitaji yake mathalani baiskeli ya mlemavu au mafuta kwa walemavu wa ngozi.

 

Katika mafunzo haya ilitolewa nafasi ya maswali naye Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Musoma Bi Consolata Anselim Makomelo akauliza ni kwanini kunahitajika kuwekwa picha ya mtu namna alivyo na siyo picha ya pasipoti? Swali hili lilijibiwa na ndugu Bruno Mwakabibi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii, akisema:

“Ni kweli lazima mlemavu apigwe picha ya muonekano wa mwili mzima ili picha hiyo itoe taswira halisi ya mlemavu wetu namna alivyo.”

Ndugu Mwakabibi alisema kuwa kunawakati ajira zilitangazwa na ndugu mmoja aliomba ajira hizo mara kadhaa na kisha jina lake kupata ajira mara mbili, moja akitumia vyeti vya kidato cha nne na nyingine kwa vyeti vya ngazi ya juu huku akitumia kigezo cha ulemavu wa ngozi alibinism, wakati hakuwa na sifa hiyo.

 

Ndugu Mwakabibi aliwaambia wana semina kuwa:

“Baadaye ilipofanyiwa uchunguzi ilibaini kuwa mhusika huyu hakuwa na ulemavu wa ngozi wakati picha yake pasipoti katika maombi ilionesha kuwa anao ulemavu wa ngozi, mamlaka husika ilifanya mawasiliano na Mkuu wa Shule ya Sekondari aliyosoma na kisha kuuliza hivi Fulani bini Fulani ni mlemavu wa ngozi? Mwalimu wake alijibu hapana na halikuishia hapo mwalimu alienda hadi nyumbani kwa ndugu huyu na kumuuliza kwanini alifanya udanganyifu huo? Alijibu ‘Nilifanya hivyo ilia nipate ajira maana wenye ulemavu wanapata kazi.’ Baadaye lilikuwa kosa la jinai kwa mhusika.”

Bi Makomelo aliuliza swali lingine, je itakuwaje kama mlemavu huyu ana tatizo la kusikia? Je ofisi ya Waziri Mkuu itahakikisha vipi?

 

Ndugu Mwakabibi alijibu swali la pili na kusema maneno haya:

“Jamii husika inamtambua kila mmoja wetu namna alivyo kama taarifa inaonesha mtaa/kijiji anapotoka. Mawasiliano yafanywe na eneo husika na wao watasema ahaa yule Bubu ahaa yule kiziwi taarifa sahihi zitapatikana tu.”

Mafunzo haya yaliendelea hadi tamati na baadaye Mwanakwetu kwenda kuyatayarisha makala haya:

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Taarifa za Wenye Ulemavu Zikusanywe Kwa Usahihi.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 


















 





0/Post a Comment/Comments