Adeladius Makwega-MBAGALA
Katika maisha ya binadamu ni kawaida na ni jambo jepesi sana kumsema mtu ambaye unamfahamu lakini ni kazi kubwa kumsema, kumsimanga, kumng’ong’a au kumrushia maneno, matusi na hata kebehi mtu ambaye haumfahamu.
Kutopigwa maneno kwa mtu ambaye hafahamiki hakuna maana kuwa mtu huyu ni mwema sana au mbaya kuzidi kifani la hasha.
Hilo ndiyo maana mara baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025 Jeshi la Polisi wamebeba lawama mno, maana ukilitaja Jeshi la Polisi Tanzania picha inayokuja akilini ni ya ndugu yetu IGP Camilius Wambura huku akitajwa moja kwa moja hadi kabila lake na nasaba yake na wazazi wake na Mwanakwetu ana hakika maneno haya yanamkera sana mtu anayesemwa vibaya:
“Yule Camilius Wambura tunamfahamu vizuri sana, kwao ni watu wazuri sana, kama shida ipo ni kwa ukoo wa mama yake lakini ukoo wa baba yake ni watu wakarimu mno, washika dini mno. Kama kurithi mabaya basi Camilius Wambura kachukua kwa ukoo wa mama yake…”
Hawa mawazo ya Watanzania wanamzungumzia IGP wao kwa uhuru kabisa maana ni mtu aliyetoka katika jamii yao koo zinazofahamika kwa Watanzania.
Huku jamii ndiyo inayofahamu kipimo cha kusema ukoo wa mama yake fulani ni wabaya au wema.
Jamii kusema haya ina haki maana yule anayetajwa anashika nafasi ya umma.
“Kama hauna nafasi ya umma hakuna anayeweza kusema maneno hayo labda kama kuna mtu anataka kuoa katika familia husika ndipo maneno kama haya yangesemwa.”
Huku kwa sehemu kubwa Watanzania wanaofanya kazi na Idara ya Usalama wa taifa wengi wao hawafahamiki labda kidogo Mkurugenzi wa Idara hii na mtu mmoja mmoja ambaye anaweza kufahamika kutokana na majukumu yake haya iwe ngazi ya Wilaya na Mkoa.
Msomaji wangu naomba leo nizungumze jambo hili:
“Katika jamii yoyote ile zipo mamlaka zinazooneka wazi na zipo mamlaka ambazo hazionekani wazi. Hili jamii iweze kufikia malengo yake mamlaka hizo mbili lazima zifanya kazi kwa pamoja na kidugu. Mamlaka zisizoonekana zinatakiwa kuwa makini mno na kuziheshimu mno mamlaka zile zinazoonekana maana taswira inayoonekana ina umuhimu mkubwa kuliko taswira iliyojificha. Huku Taswira inayoonekana ndiyo itaamua dhidi ya taswira mficho.”
Msomaji wangu nakuomba nikusimulie kisa hiki cha kweli kabisa nadhani ni tukio la Agosti , 2017.
Rais John Pombe Magufuli mwaka 2017 alifanya ziara Mkoani Tanga ambapo ndiyo siku zile alipowapatanisha huyu Waziri wa Habari wa mwaka 2026 na marehemu Ruge Mutahaba. Rais Magufuli nadhani alifanya ziara hiyo karibu Wilaya ya zote za Mkoa wa Tanga huku Wilaya ya Lushoto hakuitembelewa. Mwanzoni ilifahamika kuwa John Pombe angetembelea ya Lushoto na kufungua miradi kadhaa likiwamo jengo la Halmashauri ya Lushoto .
Katika haya maandalizi Halmashauri ya Lushoto ilipokea ugeni wa ndugu mmoja ambaye aliambatana na vijana wawili:
“Hawa ndugu walifika na kuingia ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, wakiwa watu watatu vijana wawili ambao walikuwa miili iliyojengeka sana na mtu mwingine aliyevalia kaptura na fulana ambaye ndiye alikuwa mkubwa wao, lakini mwili wake haukuwa umejengeka vizuri, ndugu huyu aliyejitambulisha na kusaini kitabu cha wageni kuwa Mkuu wa Oparesheni za Ndani wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kiongozi huyu alifanya mazungumzo na Mwanakwetu mlango upo wazi, Mwanakwetu akasema mlango ufungwe tuongee vizuri tukiwa wenyewe ndani, kisha vijana wale wakaufunga mlango na kuongea na ndugu Mwanakwetu kisha kuondoka zao na gari moja rangi nyeupe Toyota New Model gari ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Hawa jamaa walienda zao Mwanakwetu akilini mwake lilimjia hili jina la NYAULINGO ambapo wakati Mwanakwetu mwalimu wa Isimani Sekondari shule hii ilikuwa na Mkuu wa Shule mwenye jina la NYAULINGO na hata majina yalivyosainiwa katika kitabu cha wageni majina mawili ya mwisho kati ya matatu yalikuwa yanafanana na ya yule aliyekuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Isimani.
Kwa kumtazama yule Mkuu wa Oparesheni Za Ndani hata wajihi wake ulifanana na Mwalimu Nyaulingo. Wakati ugeni huu unaondoka Lushoto yule Mkuu wa Shule alishafariki lakini huu urefu wa Mkuu wa Oparesheni za Ndani, rangi ya sura yake, namna anavyoongea kulikuwa na mfanano mkubwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Isimani Mwalimu Nyaulingo aliyefanya kazi na Mwanakwetu.
Baada ya ugeni huu kukawa na mjadala mbona hawa jamaa wana gari nzuri ya serikali mbona huyu mwingine kavaa kaptura kaja katika ofisi za umma?Mbona Ofisi za Umma inakatazwa mavazi yale? Mbona utumishi wa umma unasisitiza namna ya mavazi ya mtumishi wa umma? Kwa hakika hili swali halikuweza kujibiwa.
Mwanakwetu kimoyomoyo akasema kama Mwalimu Nyaulingo angekuwa hai ningempigia simu kumwambia juu ya ugeni wa nduguye huyu aliyefika ofisini kwake lakini Mwalimu Nyaulingo alishafariki, Mwanakwetu akabaki nalo moyoni.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mamlaka ambazo hazionekani katika kila hatua yake ya kila yanavyofanywa nayo ziwe makini katika kuzijengea mazingira mazuri mamlaka zinazoonekana wazi katika macho ya jamii maana kushindwa kwa mamlaka zinazoonekana ni kushindwa kwa mamlaka zisizoonekana.
Mwanakwetu Upo? Kumbuka:
“Ningempigia Simu Mkuu Wangu wa Shule.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257








.gif)
.gif)
Post a Comment