
Adeladius Makwega-MBAGALA
Mwanakwetu aliingia ndani ya basi hili jipya lenye choo ndani na alipofika kutaka kukaa katika kiti alibaini kuwa kiti namba 14 alikuwepo mama mmoja na kiti kilichokuwa wazi kilikuwa nambali 15.
Kwa hakika ili Mwanakwetu afike katika kiti namba 15 kinachoonekana katika tiketi yake ilitakiwa mama aliyemkuta asimame na apishane nae. Huku kupishana na mama huyu lilimkwaza mno Mwanakwetu maana lazima kungekuwa na kushikana na kubahashiana hivyo kiungwana Mwanakwetu akamuomba mama huyu asogee na akae kiti namba 15 naye Mwanakwetu akaketi kiti namba 14.
Mara kondakta mwanamke akafika na kuwauliza abiria hao nambali ya viti vyao akajibiwa kuwa wamebadilishana, hilo halikuleta neno kondakta aliendelea na kazi zake na safari hii ilianza.
Safari hii ndefu iliendelea nayeye Mwanakwetu kwanza alipatwa na lepe la usingizi. Unajua haya mabasi ya sasa yana viyoyozi Mwanakwetu Kabwela mambo ya viyoyozi anajulia wapi? Mwanakwetu kiyoyozi anachokijua ni upepo mwanana wa Bahari ya Hindi pale Mtoni Kijichi au upepo mwanana chini ya mikorosho na miembe ya kurithi tu huko Mbagala na Kiparang’anda. Sasa kiyoyozi cha basi hili kikamlewesha Mwanakwetu na kumbeba mzega mzega na kisha akaupiga usingizi mzito.
Mwanakwetu alilala sana huku akiamka amka maana akiwa usingizini alikuwa anamuegemea huyu abiria jirani nayeye abiria jirani alimuegemea mno Mwanakwetu. Hapa hakukuwa na kesi ile ya shambulio la aibu. Katika hizo hekaheka za kuegemeana usingizini Mwanakwetu hakuomba namba ya simu ya mrembo huyu, wala akili ya Mwanakwetu haikuwa huko maana Mwanakwetu keshavuka hatua ya kuomba namba za simu, siku hizi Mwanakwetu huwa anapewa namba za sim utu.
Safari inaendelea na katika kulala huko Mwanakwetu akaota ndoto kadhaa fupi fupi zipo alizozikumbuka na zipo kadhaa ambazo alizisahau, mojawapo ya ndoto anayoikumbuka ilikuwa hii kuna mtu mithili ya hakimu au jaji mwanamke amekufa, huku watu wanalia sana, kisha waombolezaji wakambeba na kwenda kumzika.
Baada ya kumzikwa huyu Jaji Binti Hakimu inaonekana baadaye yupo katika mandhari nyingine huku huyu mama yu hai amevaa nguo nyeupe na yu mahakamani lakini hatoi hukumu, bali yeye yu kizimbani. Upande wa hakimu unaonekana mwanga tu wenye miale mikali lakini hakuna taswira binadamu inayoonekana vizuri zaidi ya mwanga, Mwanakwetu ndotoni akawa anasema:
“Huyu si hakimu kwanini yeye hatoi hukumu bali yeye anahukumiwa?Au huyu Jaji Binti Hakimu ana pacha wake?”
Mwanakwetu akawa anasema kwa sauti kubwa ndotoni lakini sauti yake ikawa haitoki, kama ameshikwa na jinamizi lakini baadaye sauti ikatoka kwa nguvu.
“…Au yeye Jaji Binti Hakimu ana pacha wake!”
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu anastaajabu ndotoni.
Mwanakwetu ndotoni akatambua kuwa japokuwa aliyasema maneno haya kwa nguvu lakini hayakuwa kero kwa hakimu yaani ule mwanga na kama huyu hakimu mithili kama hakuyasikia.
Hakimu wa kule juu ambaye unaonekana mwanga akasikika akisema na huyu mtuhumiwa. Wewe si ulikuwa hakimu ? Jaji Binti Hakimu akajibu ndiyo? Likaulizwa swali lingine wewe Jaji binti Hakimu ukiwa huko umehukumu kesi ngapi? Akajibu kuwa amehukumu kesi nyingi tangu akiwa binti hadi sasa ni ajuza lakini idadi yake amesahau. Yule hakimu ambaye ambaye haonikani akasema idadi tunazifahamu lakini tukuulize swali-
Wewe ulikuwa unatoa hukumu za haki? Jaji Binti Hakimu wakati anataka kuanza kujibu akapiga chafya tano chaa..chaaa. chaaaa chaaaa… chaaaa… huku makamasi yakawa yanamtoka na machozi juu yake katika macho yake mawili, kisha akajibu ndiyo nilitoa sana hukumu za haki.
Ndugu mmoja aliye mbele ya huyu mama kama mzee wa baraza kando ya ule mwanga unaotoa maneno ya hakimu akasema wewe mbona haukuwa na hamu ya haki? Jaji binti Hakimu akajibu hamu ya haki nilikuwa nayo na nimejitahdi kulitimiza hilo vizuri. Ndugu mbele kama mzee wa baraza anamuuliza maswali mengine huyu Jaji Binti Hakimu lakini maswali mengine Mwanakwetu hakuyasikia vizuri.
Mwanakwetu ndotoni akasema hii mashine yangu ya kurekodi kama ningewahi hapa mahakamani ningeiweka kando na jirani na spika ya huyu mzee wa baraza.
Baadaye likaulizwa swali na mzee baraza:
“Mbona kuna kesi namba 15 uliipokea na ambapo mtuhumiwa alimsukuma mwenzake ili aanguke tu shabaha akae yeye kitini lakini huyu mtuhumiwa wa kumsukuma mwenzake anayetumiwa kumsuka mwenzake yeye alipigwa mishale 36 mwili mzima lakini wewe mbona kesi hii haukushughulika nayo?”
Jaji binti Hakimu kizimbani akajibu ni kweli kesi namba 15 ndiyo ililetwa mahakamani lakini kesi namba siifahamu na kama kesi ilikuwa na namba basi pengine alipewa Jaji mwingine siyo mimi.Kama sikupangiwa hiyo kesi alipewa mtu mwingine.
Huyu hakimu ambaye haonekani bali mwanga tu akauliza , Kwa hiyo hadi aamue mtu mwingine kuileta mahakamani ? Jaji Binti Hakimu akajibu ndiyo. Likaulizwa swali lingine sasa wewe ulishindwa kuwauliza walioleta kesi namba 15 mbona kesi namba 14 kimya? Si wanakuja mahakamani? Ungewauliza ? Jaji Binti Hakimu akajibu hayo mamlaka sikuwa nayo.
Hakimu huyu ambaye anatoa sauti yake katika mwanga mkubwa akasema:
“Kumbe wewe haukuwa na kiu ya haki. Si ungefanya jambo jepesi tu, si ungesema nyinyi mmeleta kesi namba 15 lakini mimi mkata shauri najua ipo kesi namba 14 hivyo basi nitaanza na kesi 14 kisha nitakuja na kesi namba 15 hapo kazi ingeisha lakini wewe haukufanya hivyo. Unadhani kesi hii ingekuwa mbele ya Mfalme Seleiman asigali fanya kama hivi ninavyokueleza?”
Jaji Binti Hakimu alikaa kimya huku akipigwa na butwaa.
Kumbuka Mwanakwetu yu safarini huku amelala usingizi gafla huyu binti kando ya Mwanakwetu akawa anamuamsha Mwanakwetu
“Kaka kaka kaka basi limesimama twende kutanunue chakula.”
Mwanakwetu aliamka usingizini, akampisha huyu mrembo ili akashuke ndani ya basi na akununue chakula. Mwanakwetu akavua sweta lake kisha nayeye kushuka basini akanunua kikombe cha chai ya rangi akanywa huku akiwa anatafakari hii ndoto. Mwanakwetu alikuwa na tafakari kubwa juu ya ndoto hii ya Jaji Binti Hakimu aliyoiota safarini. Alipomaliza kunywa chai hii alingoja amuone yule mrembo kama amerudi kitini ili nayeye arudi basini , baada ya dakika kama tano huyu mrembo alirudi basini nayeye Mwanakwetu kurudi kuketi kitini, mrembo ameketi kiti namba 15 nayeye Mwanakwetu ameketi kiti namba 14 na kuendelea na safari
Huku Mwanakwetu akitafakari hii ndoto akisema kumbe mahakama na hakimu wanaweza kuwa na kiu ya haki kama hivi alivyoota ndotoni? Ati unaletewa kesi namba 15 kisha wewe unaanza na kesi namba 14 ya mtu kupigwa mishale 36? Mwanakwetu akabaki na bumbuwazi huku akijilaumu kwani huyu mrembo alimuasha ndotoni maana alikuwa na kiu ya kujua huyu hakimu anayetoa sauti katika mwanga angemuhukumu vipi huyu Jaji Binti Hakimu?
Mwanakwetu alitafakari mno hii ndoto na hakulala tena hadi anafika mwisho wa safari yake, huku akishangazwa na ndoto hii tangu pale alipobadilishana viti vya kukaa na yule dada safarini huku hakujua maana ya ndoto hii.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Ndoto ya Jaji Binti Hakimu.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257


.gif)




Post a Comment