LIMBWATA LA SANSA NA MLENDA

 

Adeladius Makwega MBAGALA.

“Mimi ni Muisilamu, nikifa Dodoma udongo wa Dodoma ushanipenda, msinisafirishe kunipeleka Bagamoyo kwa sababu Bagamoyo yetu kule Pande tayari Bandari ishakuja. Nilipendekeza nizikwe pale alipozikwa mama yangu na mimi nizikwe hapo hapo…Kwa hiyo nikidondoka hapa Dodoma msihangaike, msipate tabu kunisumbuasumbua…Nilishawambia wanangu nitanunua kiwanja Dodoma, nitajenga hapa hapa na watoto wangu watakuja hapa hapa Dodoma…”

Haya ni maelezo ya Mwanamuziki maarufu wa Afrika Mashariki Kocha wa Dunia Mwinjuma Muumini akiwa na kipaza sauti ukumbini jijini Dodoma, akiutoa wosia huu kwa wapenzi wake wa muziki juu ya kifo chake kama kitatokea Dodoma basi mambo yote yamalizikie hapo hapo Dodoma makao makuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Maneno haya yalimshitua mno Mwanakwetu mara alipoyasikia, inakuwaje Kocha wa Dunia, Prince Muumini kuyasema maneno haya yote? Kocha wa Dunia amepata mwanamke wa Kigogo?Mwanamke wa Kirangi, hadi kanogewa na kuyasema haya yote? Kocha wa Dunia ameshalishwa limbwata la Sansa na Mlenda?

Haya yote ni maswali ya Mwanakwetu juu ya ndugu yake huyu kutoka Bagamoyo ya Pwani ya Tanzania.

Mwanakwetu akiwa katika mzigo wa tafakari haya akakumbuka mawasilinao haya na nduguye kwa mika karibu mitano mfululizo:

“Mwinjuma Muumini ndiye mwanamuzi pekee wa Muziki wa Dansi nchini Tanzania ambaye wanaheshimiana mno na Mwanakwetu kwa miaka mingi na mara nyingi Kocha wa dunia akifika Dodoma huwa anawasiliana na Mwanakwetu kujua kama Mwanakwetu yu Dodoma na miaka mitano mfululizo kila mwanamuziki huyu akiwa Dodoma Mwanakwetu hayupo.”

Kwa kumbukumbu za Mwanakwetu, kwa mwaka wa 2022 Mwinjuma Muumini alifika Dodoma na kumtafuta Mwanakwetu, kaka upo Dodoma? Siku hii Mwanakwetu alikuwa Zanzibar na ile Kamati ya Vazi la Taifa, mwaka 2023 Mwinjuma Muumini alifika Dodoma na kuuliza kaka upo Dodoma? Mwanakwetu akajibu kaka nipo Mbeya, mwaka wa 2024 Muumini alifika Dodoma na kuuliza kaka upo Dodoma? Mwanakwetu akajibu kaka nipo Mwanza na mwaka 2026 Mwinjuma aliwasiliana na Mwanakwetu akauliza swali lile lile. Mwanakwetu akajibu Kaka nipo Musoma nimehamishiwa Musoma kwa sasa nipo wa Wajaluo, Wajita, Wakwaya na Wakurya nduguze Julius Nyerere nakula limbwata za dada wa Mchongomeno(Julius Nyerere) hadi navimbiwa. Mwinjuma Muumini ni mchangamfu sana akawa anacheka tu.

 

Mwinyijuma Muumini  baadaye akajibu :

“Kaka si unajua huu ni utu uzima, nimesahau tu ulishaniambia kuwa upo Musoma Mara mwaka wa 2025.”

Mwanakwetu akajibu ndiyo na hapohapo Mwanakwetu tena akamuuliza Dodoma kaka umefikia wapi? Mwinjuma Muumini akajibu kuwa amefikia NZUGUNI B. Mwanakwetu akacheka kisha akasema:

“Kaka angalia Limbwata za Sansa na Mlenda zinaungwa kwa ufuta na karanga , kuwa makini hapo hakuna limbatwa za nazi.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa kuwa Mwanakwetu ni rafiki wa Mwinjuma Muumini na hakuwepo wakati mwanamuziki huyu anatoa wosia wake hapo Dodoma, juu ya pahala pa kuzikwa hivyo leo Mwanakwetu aliamua kurudia kauli ya Mwanamuziki huyu katika makala haya siku ya leo huku akijiuliza swali hili:

“Wadala wa Chigogo (wanawake wa Kigogo) Wamemlisha Mwinjuma Muumini Limbwata la Sansa na Mlenda?Hili litakuwa Limbwata la Uzeeni?”

Mwanakwetu hajapata jibu lakini ana hakika maswali haya yatamfikia ndugu yake Mwinjuma Muumini(Kocha dunia? popote alipo kisha atayajibu kwa haraka iwezekanavyo.

 

Mwanakwetu upo? Je Makala haya niyahitaje? Wagogo Wamemlisha Mwinyijuma Muumini Limbwata la Sansa na Mlenda? Au Limbwata la uzeeni? Wasomaji wangu naomba mnipe mji ili nichague kichwa kimoja kati ya hivyo viwili lakini Kumbuka Limbwata la Sansa na Mlenda.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com.

0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments