Adeladius Makwega MBAGALA.
Safari hii ilikuwa ndefu sana karibu saa 26, hatua ya kwanza ya safari Mwanakwetu alifika, kisha akafika kituo cha kwanza na kupanda basi lingine kwa malipo ya shlingi 25,000 za Kitanzania ikiwa sawa na dola 10 za Kimarekani, wakati safari aliyoanza awali nayo ilikuwa ya shilingi 65,000 za kitanzania sawa na dola 26 za Kimarekani.
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yupo katika safari ya pili na hadi afike huko aendapo ni safari sita, kweli safari ya pili ilifika ukingoni na yeye kushuka kugonja basi la safari ya tatu, hapa akapanda basi aina ya costa, hii akaenda nayo hadi alipopaswa kushuka kisha kupanda basi la usafiri wa safari ya nne na kisha kupanda usafiri wa safari ya tano.
Safari hii Mwanakwetu alipata kiti jirani na dereva, huku upande wa mkono wa shoto alikaa mama mmoja mnene sana huku alikuwa mama mmoja mwema mno. Safu ya mbele ilianza na dereva kisha Mwanakwetu alafu mama mnene, huku kiti cha Mwanakwetu kilikuwa cha juu hivyo miguu ya Mwanakwetu mirefu ilining’ing’inia juu juu, mama kando akasema :
“Wee Baba miguu yako mirefu! Hapo ulipokaa ukifika nyumbani kwako si utakuwa mgonjwa? Ebu miguu yako iangushie kwangu mie.”
Mama mnene, mama mwema , mama mkarimu anamwambia Mwanakwetu maneno haya, gafla mama mnene, mama mwema , mama mkarimu akapigiwa simu:
“Eeh… natoka kumuangalia mtoto shuleni, ndiyo kesho Jumatatu kazini… ndiyo nitakuja kukuona… sawa sawa…sawa.”
Kondakta akamwambia mama mnene, mwambie huyo jamaa tunaomba nauli, Mama mnene akamwambia Mwanakwetu, wanataka nauli yao. Mwanakwetu akauliza nauli kiasi gani? Mama mnene akamwambia kondakta, kisha Mwanakwetu akajibiwa shilingi 4000 za Kitanzania ambayo ni sawa na dola moja unusi ya Marekani kwa mwaka wa 2026, Mwanakwetu akatoa na kulipa kiasi hicho kwa noti mbili za shilingi 2000.
Safari ikawa inaendelea, huku ndani ya gari kukawa kimya na utulivu sana, huku kondakta anaongea na utingo wake:
“Jamaa amefariki jana, tumetoka kuzika na leo ndiyo siku ta tatu tumeanua matanga, ndiyo maana mlipopita tripu ya kwanza hatukuonana, nilikuwa msibani, ila huko msibani tumekula mno nyama ya paa, mimi sikumbuki mara ya mwisho kabla ya msiba huu nimekula lini nyama hii. Yaani nyama ya paa ilikuwa nyingi kulika hata wali. Ule msiba ulikuwa wa kipekee sana. (Watu maliasili hawajawasumbua?) Ahaaa wapi walijua ile ni nyama ya ng’ombe, kwani askari wa wanyama pori wenyewe hawapati misiba?Hata kama wangejua unawakamataje watu wanaozika marehemu wao? tumezika huku tukila nyama ya paa.”
Kondakta akamuuliza huyu utingo hiyo nyama ya paa wameipataje?
Jamaa akajibu:
“Jamaa wawindaji haramu wawili walikwenda kuwinda mbugani na pikipiki yao, wakiwa kazini wakapata paa watano, siku hii neema iliwatembelea, wakajificha machakani wakawakatakata vipande vipande kadhaa wale paa wao huku ngozi wakichuna na vichwa vya paa kuvivunjavunja ili wakikamatwa isijulikane , zile ngozi zilikuwa dili kwa ajili ya kuwambia ngoma , hivyo basi wakazifunga vizuri kisha wakaziweka chini ya kiti cha pikipiki na nyama yaoa katika matenga mawili na kuanza safari ya kurudi nyumbani. Wakati wanaanza safari mvua kubwa ikaanza kunyesha msituni, hivyo basi mvua hii ilisaidia sana wao kuweza kusafiri safari ndefu bila ya kukutana na mtu njiani. Walipofika kijiji kimoja wakanunua nyanya na vitungu kama vya shilingi 30,000 ya Kitanzania ambayo ni sawa na dola za Kimarekani kama 12 vitunguu vikapangwa chini kisha nyanya juu yake, kitendo hiki kilikuwa kama geresha kama wangekutana na mtu njiani ambaye angewatilia mashaka.
Hii njia jamaa wanaifahamu vizuri sana ila kutokana mvua kubwa kunyesha kuna ile mito ya msimu wa mvua lakini jamaa wanaijua ni mito midogo, wakiwa safarini nyuma yao wanasikia pikipikipi inakuja kwa kasi. Wakajua hao ni askari wa wanyama pori ambao waliitilia shaka ile pikipiki yenye matenga na bila shaka pale waliponunua nyanya na vitunguu kuna mtu aliwajulisha askari wanyamapori. Jamaa hawa wenye tenga la nyama ya paa wakapita kwa kasi juu ya mto ule , kasi ya maji ikawasomba lakini huyu jamaa aliyekuwa amekaa juu ya tenga alirukia tawi la mti wa kando , tawi la kwanza likakatika na kwenda kwenye maji, tawi la pili likamsaidia na akakaa juu ya mti kimya.
Hapa pikipiki, dereva wake, matenga nyama ya paa, nyanya na vitunguu vimesombwa na maji. Jamaa wa wanyama pori walipofika pale ambapo ni nje ya mbuga wakayaangalia maji hawakuona kitu,askari hawa wanayaona matairi ya pikipiki yanaingia mtoni lakini jamaa hawaonekani. Vipi hawa jamaa wamepita kimiujiza? Jamaa hawa wakageuza kurudi mbugani. Kumbuka kule juu ya mti jamaa yule aliyekuwa juu ya tenga kajificha askari wa wanyama pori walipoondoka ndipo jamaa akashuka zake, akaufuatilia mto hakuona kitu, hivyo basi alitoa taarifa kijiji jirani na kwao, siyo kile kijiji walichonunua nyanya na vitunguu bali kijiji cha mbele watu wakaja kumsaka ndugu yao na pikipiki yao.
Sakasaka na wewe baadaye wakakutana mwili wa jamaa ameshafariki na wakaisaka pikipiki wakaiona ipo vile vile na tenga la nyanya, vitunguu na nyama ya paa.Taratibu zikafuatwa ndipo msiba ukaandaliwa, jamani tumekula nyama ya paa siku tatu.”
Mwanakwetu alifika kituo chake, huku basi hili likiendelea na safari yake, kisha kushuka na kuanza safari yake ya sita ili afike kule aendapo.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika unaweza ukadhani ya kuwa leo katika mawindo yako Mungu kakubariki, umepata wanyama wengi, leo ngekewa imekutembelea, kumbe mawimbo haya unayoyafanya ni kwa ajili ya kitoweo kwa msiba wako wewe mwenyewe.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Kitoweo Cha Msiba Wako Wewe Mwenyewe.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257










Post a Comment