Seleiman Bungara, maarufu kama Bwege, mwanasiasa maarufu mno nchini Tanzania katika siasa za upinzani, akiwa na tambo za kuvutia katika majukwaa ya kisiasa na vipaza sauti amefariki dunia Machi 30, 2026.
Mwanakwetu kwa majonzi makubwa, huku mchozi ukimtiririka mithili ya maji ya Mto Rufiji siku ya leo anamtazama Seleiman Bin Bungara aliyekuwa na ndoto alizozikamilisha na ndoto ambazo hakuzikamilisha, japokuwa alikuwa na maradhi lakini alikuwa akipambana kuzikamilisha ndoto zake.
Ndugu huyu hakuyatumia maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kufunga sala na kusema basi, bali alitumia pumzi yake vizuri kusema lililo haki mbele ya walimwengu waliojaa husuda, giliba na hadaa tele.
Mwanakwetu siku ya leo anaomba akusimulia msomaji wake mambo mawili ambayo ni ndoto mbili moja imekamilika na moja ambayo alikuwa mbioni kuikamilisha ndugu yetu Bungara lakini hakuikamilisha.
Tarehe za mwanzoni mwa Machi, 2026 Mwanakwetu alipigiwa simu na kijana mmoja ambaye alikuwa na nasaba na Seleiman Bungara, akisema maneno haya:
“Kaka Makwega shikamoo ! Hapa nina ujumbe kutoka kwa Seleiman Bungara ameniagiza kazi huku Kilwa lakini ameniomba niongee na wewe, umsaidie kuandika kitabu chake juu ya maisha yake, naomba unipe mwongozo ili kazi hii ifanyike mapema.”
Mwanakwetu alijibu kwa maneno haya;
“Kwa namna Seleiman Bungara alivyo mwema, mimi hapa sina fedha lakini kazi hii nitaifanya asinilipe chochote lakini nashauri haya, mchango wangu utakuwa hadi kupata andiko la muswada la awali, yeye agaramie mhariri na kuelekea kwa mchapaji. Mhariri Mzuri ni yule kijana wa Kiluguru Doto Rangimoto, najua ataifanya kazi hii vizuri. Kwa mwezi Machi nina nafasi ya kutosha, mwambie Mzee Bungara yote niliyokueleza akamilishe lakini muhimu sana wakati anasimulia nitaomba turekodi sauti na video ili iweze kuwa rejea ya maisha yake, mimi kamera kubwa ninazo lakini zipo Lushoto Tanga kuja nazo Dar es Salaam ni mzito, mwambie amtafute kijana atakayefanya kazi hiyo ya kurekodi video na sauti hapo hapo nyumbani kwake.”
Jambo hilo akaelezwa ndugu Bungara likawa jepesi sana huku akisema:
“Nina kijana wangu ana studio, hilo la kurekodi sauti na video limekwesha nitawapigia kuwaambia lini mje.”
Wakati inasubiriwa lini kwenda kuifanya kazi hii ndipo mwezi machi unafika ukingoni hadi Seleiman Bungara taarifa ya kifo chake zinatangazwa. Lakini wakati kukiwa na ukimya sana mawasiliano kulifanyika mawasiliano huku tukiambizana pengine Bwege ni mgonjwa, ngoja tumumbee dua apone haraka. Ndiyo kusema Seleiman Bungara alikuwa na ndoto ya kuandika kitabu juu ya maisha yake. Hili ni la kwanza na ni ndoto isiyokamilika. Katika maisha ya binadamu hapa dunia kila mmoja Mungu kamjalia kipawa chake iwe kuimba, kucheza, kulima, kuwinda, kufundisha, Uandishi wa Habari, ualimu, ufundi, utabibu kuongoza na hata kufanya siasa.
Swali la kujiuliza mtu anapofariki sisi wengine tunapomtazama ameikamilisha kazi hiyo aliyokuwa anaifanya? Au kuna deni analodaiwa?
“Mathalani mie Mwanakwetu mwana habari, leo Mungu mwenye pumzi yake kaichukua, katika taaluma yangu ya habari je kazi hii nimeitendea haki? Hilo ni kwa kila mmoja lazima ajiulize.”
Msomaji wangu naomba nikusimulie kisa hiki:
“Mwaka wa 2014 nyumbani kwetu Mbagala Sabasaba kulikuwa na bibi mmoja Mndengereko aliyefahamika kama Bibi Faida(Mama Faida) huyu mama alifiwa na kaka yake. Kwa kuwa Bibi Faida alikuwa na urafiki mno na Bibi Mzaa Baba wa Mwanakwetu Hedwiki Omari Binti Mkomangi. Bibi wa Mwanakwetu akasema:
‘Mjukuu wangu nenda kazike Mbagala Kongowe maana Mama Faida kafiwa na kaka yake. Kwa kuwa huu ni msiba wa Waisilamu mimi nimeenda msibani, nikatoa pole yangu kisha nikarudi, mjukuu wangu unafahamu maziko ya Waisilamu hawaruhusu wanaweka kwenda makaburini. Mjukuu wangu nenda kazike.’
Siku iliyofuata saa nne kamili Mwanakwetu yupo Kongowe nyumbani kwa marehemu ili kumzika huyu ndugu. Mwili ukatolewa nje ili kusaliwa, wale waliokuwa wamejiandaa wakawa tayari kando na mwili wa marehemu. Shekhe akasema kabla ya kuusalia mwili huu naomba kama kuna mtu anamdai marehemu au kama kuna mtu anadaiwa na marehemu aje hapa aseme ili tukimaliza hilo twende tukamsitiri ndugu yetu.
Wazee wa Kiisilamu kando na mwili wa marehemu wakasema sheikh hiyo fatua ya madeni haujaisema vizuri, sema moja moja.
Shekh yule akafuata maelekezo. Haya jamani swali la kwanza anayedaiwa marehemu? Hapa palikuwa kimya. Swali hilo likarudiwa mara tatu kimya. Swali la pili likasemwa nani anayemdai marehemu? Ndugu mmoja aliyekuwa amekaa jirani na mnazi alinyosha mkono juu kisha akasimama akasema namdai marehemu 495,000/=. Huku wakaombwa mashahidi, hapa hapa jamaa ambao ni Viongozi wa sokoni Temeke Stereo wakajitokeza kutoa ushuhuda, kuwa marehemu alichukua mzigo wa nazi muda mchache kabla ya umauti maana sokoni mizigo inachukuliwa kwa mali kauli.
Huyu shekhe alikuwa makini mno akasema jamani hapa tupo wengi, mimi nimeshatawaza (nimeshajiandaa kusali) ili tuusalie mwili lazima ili deni tulitatue maana marehemu anadaiwa hivyo basi, vijana wa madrasa pitisheni michango tuone tunapata kiasi gani… mchango ulipitishwa haraka haraka na kupatikana 455,000/- huku elfu arobaini iliyobakia ikaongozewa na familia, kisha mwili ukasaliwa na kwenda kuzikwa makaburi ya Mbagala Kongowe.”
Kwa marehemu huyu ambaye kazi yake ilikuwa biashara alifariki akiwa na deni ambalo huyu aliyekuwa anadai alikuwa na nafasi ya kusamehe lakini kusamehe au la inategemea na hali deni, dhamiri ya anayedai na inawezekana pale msibani walikuwepo wengi ambao pengine walikuwa wanamdai marehemu lakini waliisamehe maiti hii lakini huyu aliyekuwa anadai 495,000/= pengine deni hilo lisingelipwa jambo hili lingemtia katika dhambi zaidi.Siku hii hapa msibani waombolezaji waligawanyika katika makundi mawili, wengine wakisema sahihi wengine wakisema kitendo hiki si cha kiungwana. Maziko yalipomalizika kila mmoja alirudi kwake.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa ndugu yetu Seleiman Bungara Mwanakwetu anaamini ukiungalia mwenendo wake tangu mwishoni mwa mwaka wa 2024 alikuwa muwazi, alikuwa mkweli na huku akitoa msimamo wake kuhusu siasa za Tanzania wazi wazi, kuelekea Uchaguzi Mkuu na hata msimamo wake baada ya uchaguzi Mkuu.
Mwanakwetu anaamini kisiasa Seleiman Bungara hana deni analodaiwa na wala hahitaji kuombewa msamaha au kulipiwa deni ilo na mtu yoyote yule maana ndugu Bungara alijitahidi katika hali ya ugonjwa wake kupaza sauti yake bila ya kuchoka huku baadhi ya watu walimkebehi.
Kama kudaiwa basi Watanzania tunadaiwa na Seleiman Bungara. Kwa hiyo kisiasa ndoto yake Seleiman Bungara aliikamilisha vizuri na Watanzania wameshuhudia Bungara akisitisha na kutengana na wale waliokuwa wanafanya siasa ambazo alizikataa.
Mwanakwetu kwa makala haya anatoa pole kwa familia ya Bungara kwa kupoteza ndugu yao. Mwanakwetu anatoa pole kwa watu Kilwa na Waislamu wote wa Kilwa kwa msiba huo.
Mwanakwetu anatambua Seleiman Bungara hakuikamilisha ndoto yake ya kuandika kitabu cha maisha yake lakini maisha yake ya kisiasa yaliykuwa ni ndoto iliyokamilika na ndoto hii ni kitabu tosha ambacho kimeshasomwa na kila Mtanzania kabla hakijachapishwa, hasa wale Watanzania wenye mapenzi mema.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Kitabu Kilichosomwa Kabla Hakijachapishwa.”
Buriani Seleiman Bungara.
0717649257





.gif)




.gif)
Post a Comment