Kanisa Letu Dogo na Zuri la Mbagala

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Wakazi wa asili wa Mbagala wana Kanisa lao dogo sana ambalo lilijengwa miaka mingi wakati Ukristo unaingia Kijijini Mbagala. Kanisa hili dogo, zuri ukingia ndani lina mambo mengi mazuri ambayo Mwanakwetu aliyaona tangu akiwa mdogo, wakati ule wa kutazama sinema za Yesu hasa wakati wa Krisimasi. Humu ndani kuna samani nzuri sana, imara sana za miti imara sana ya Pwani ya Tanzania kama vile mivule, mininga na mipingo ambayo inaonesha asili ya watu wa Mikoa ya Pwani, Lindi, Morogoro, Dar es Salaam na hata Mtwara hapa hapa Tanzania.

Huku mbele ya Kanisa hili imara sana mkono wa kulia likipambwa na picha ya Bikira Maria na nyota kadhaa, picha hii ikipambwa na nakshi kadhaa zinazozungukwa za magamba ya Konokono wa Bahari Hindi,huku ukiwa Kanisani hapo kwa kando unaiona vizuri mandhari ya Bahari ya Hindi kupitia Hospitali ya Buruda inayomilikiwa na Masista wa Consolata.

Huku Masista hawa wa Consolata waliwatibu mno akina Mwanakwetu miaka ya 1970 na 1980 wakati wakiugua Koshakoo, Pepopunda, Kichocho, Malaria, Malare, Kifadulu na kipindupindu, kanisa lilifanya kazi kubwa sana.

Kanisa letu dogo na zuri la Mbagala linapendeza sana.

Ndani ya Kanisa hili dogo mkono wa shoto kuna taswira ya Mtakatifu Antony wa Padua ambaye ndiye somo wa Kanisa hili na somo wa Parokia ya asili ya eneo hili tangu enzi hizo. Kwa juu Kanisa hili lina madirisha yanayofunguka pande mbili ambayo ni madirisha ya kizamani sana yenye flemu za kupachika mbao mdogo ndogo ili kuingiza hewa kwa walio kanisa nyakati zote. Ukitazama juu macho yako kwanza yatakutana na makechi mazito ya mninga, kisha vigae imara vya tangu enzi hizo.

Unapotaka kuingia Kanisani mlangoni kuna ngazi kadhaa chache, kisha mkono wa kulia kuna kile kibanda cha kuungamia na mkono wa kushoto kuna kengele kubwa ya miaka mingi sana, kengele ya tangu kale ambayo ilikuwa ikipigwa miaka ya zamani inasikika Mbagala nzima, Mtoni, Temeke na hata Tandika. Kengele hii nzito ilikuwa na mambo makubwa sana maana ilikuwa na tabia mbaya iliwahi kumrusha juu Mwanakwetu pale alipokuwa na zamu ya kugonga kengele, huyu alikuwa Mwanakwetu mdogo.

Sijuhi kengele hii kwa sasa ikimuona Mwanakwetu haiwezi kumfanyia vituko vyake vya zamani?Abadani aibu ya Kengele haimkuti Mwanakwetu.

“Najua itamuogopa Mwanakwetu maana sasa ana ndevu, sasa ana mvi, sasa ana sauti nzito na sasa Mwanakwetu ni mkubwa.”

Nje ya Kanisa hili ipo sanamu nzuri ya Bikira Maria ambayo inamkumbusha Mwanakwetu tangu akiwa mdogo maana alikuwa anakalishwa mbele, huku wakubwa wanakaa katika viti ndipo ile sala ya Salaam Maria inaanzishwa na akina mama wa Mbagala kama vile Mama Mwingizi, Mama Ngunga, Mama Mtinda, Mama Maufi, Mama Kazigoma, Mama Mkundi na wengine wengi, sasa Mwanakwetu ni mzee wadogo ndiyo wanakaa chini. Wakubwa siye tunakaa katika viti.

Baadaye lilijengwa Kanisa Kubwa, kisha likavunjwa na Parokia Kujengwa Mbagala Zakhem. Wakati siye Wakristo wenyeji tulikuwa jirani na Parokia yetu hapa sasa tukawa wageni huko Mbagala Zakhem, ukienda kusali unapanda gari na kama hauna nauli unatembea kwa mguu kwa umbali mrefu-Ama kweli wakwanza atakuwa wa mwisho naye wa mwisho atakuwa wa kwanza. Pale lilipovunjwa kanisa letu kubwa yakajengwa makazi ya nyumba ya Shirika la Dada Wadogo.

Jambo zuri ni tu kwa sasa Kanisa letu dogo bado lipo, halikunjwa lakini Dada Wadogo Wametupora Letu Kanisa, ni kweli tunakwenda kusali katika Kanisa Letu Dogo, lakini dada Wadogo wamehodhi kanisa letu. Kwanza kumezungushiwa ukuta mkubwa, tukiingia pale getini tunaingia kwa maswali mengi ya walinzi, wakati zamani hatukuwa tunaulizwa maswali, sisi ndiyo wenye kanisa letu. Kanisa letu nyumba Mungu, Yesu yupo anatoa neema. Kwa hakika Mimi Mkristo mwenyeji wa Mbagala, kwa madhaifu yangu yote hakika rasilimali yangu ni lile Kanisa Dogo la Mtakatifu Antony wa Padua lililonifundisha Ukristo na ndiyo maana nachukizwa sana na maswali ninayoulizwa getini, nyie punguzeni maswali, ama kweli Dada Wadogo Wametupoka letu Kanisa.


 

Mwanakwetu siku ya leo amelikumbuka tu Kanisa lao la asili la Mbagala na hili ndilo kanisa la kwanza la Mbagala na kama ingekuwa hakuna walinzi kama zamani, hakuna maswali basi leo hii makala haya yangeambatana na picha tele za kanisa letu hilo tangu picha ya ile kengele ambayo ilikuwa haimuheshimu Mwanakwetu, picha ya kile kibanda cha mninga cha kuungamia, picha ya Bikira Maria iliyopambwa na Konokokono wa Bahari ya Hindi, picha ya Mtakatifu Antony wa Padua, picha ya altare yetu, picha ya madirisha ya mbao za kupachika na picha ya samani zote za miti ya mipingo, mivule na mininga ndani ya kanisani lakini leo hii kanisani kwetu unaingia kwa maswali.

Leo Machi 9, 2026 nikitaka kupiga picha hizo walinzi Wataniuliza wewe nani?Unakwenda kufanya nini? Mwanakwetu nitajibu nini mie? Hapa nitaonekana mie mkorofi lakini hili ni Kanisa letu.

Wazee wetu wanatusimulia kuwa pale ilipo Mbagala Spritual Center awali palikuwa na Kanisa hilo dogo na nyumba moja ya Padri tu, huku Katekista alitafutiwa kiwanja na Wakristo Wenyeji nje ambao walikuwa ni Wamakonde, Wazaramo, Wamatumbi, Wangindo, Wapogoro na Magoa huku wakimjengea nyumba ya tope na makuti Katekista wao na ndiyo maana koo nyingi za makatekista wa Mbagala wengi waliotokea Songea familia zao zilisalia Mbagala hadi kesho.


 

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu anasema kuwa kama Kadinali Laurean Rugambwa angekuwa hai angemtumia makala haya maana yeye anakumbuka tangu Shirika la Dada Wadogo analianzisha pale Mbagala huku makazi haya yakiwa na Kanisa Kubwa moja, Kanisa dogo hili linalosimuliwa leo hii na nyumba dogo ya Mapadri, godauni la mbao na nyumba dogo mbili lakini huko alipolala Kadinali Rugambwa hana hakika kama anaweza kusoma makala haya lakini matumaini makubwa ya Mwanakwetu ni kwamba Mapadri wanaokaa hapa na watawa wa Shirika la Dada Wadogo waambieni Walinzi pale getini, wenyeji tupo, huwa tunakuja mara moja moja , tupo mikoani katika miraba yetu(kazini) tunapokuja siyo wageni bali wenyeji punguzeni maswali kwetu, kikubwa tunapokuja mpunguze maswali mengi, hatuji kwenye hoteli bali tunakuja katika Kanisa letu dogo na zuri la Mtakatifu Antony wa Padua ndani ya Kituo cha Kiroho Mbagala na ndiyo maana Mwanakwetu ameeleza uzuri wa kanisa hili la wala hakueleza uzuri wa vyumba vya hoteli au uzuri wa vyakula vinavyopikwa ndani ya kituo hiki.

Kwa hakika kwa sasa Kanisa la Tanzania linafanya biashara kadhaa, iwe hoteli, iwe Zahanati, iwe Vituo vya Afya, iwe Hospitali na hata Vyuo Vikuu hili ni jambo la msingi biashara zetu na haya yote yanayofanyika mfalme wetu siyo FEDHA yupo mfalme wetu.

“Tujifunze katika Zahanati ya Masista wa Consolata Mbagala Misheni maarufu kama kwa BURUDA namna ilivyolinda uhai wa watoto wadogo rika za Mwanakwetu wakati ule, walivyokuwa wakiugua Kifadulu na Kwashakoo hadi leo hii miaka 52 Mwanakwetu anaisimulia zahanati hiyo. Maana watoto wagonjwa walitibiwa na kupewa chakula bure maarufu kama Buruga, Maziwa na nguo za kuvaa…bila ya kujali dini ya mgonjwa –Tukumbuke Wakristo siye Mfalme wetu siyo mali bali Kristo Yesu Mfufuka.”

Kwa hakika suala la usalama ni muhimu sana lakini usalama wetu, vyeo vyetu, ratiba zetu, walinzi wetu, mageti yetu, biashara zetu, taasisi zetu na fedha zisiwe sanamu ya kumzuia mwanadamu, kumzuia Mkristo kupata huduma za kiroho.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka:

“Kanisa Letu Dogo na Zuri la Mbagala.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.


 



 



0/Post a Comment/Comments