
Adeladius Makwega– MBAGALA.
Haya yalikuwa ni majira ya usiku wa Machi 10, 2026, Mwanakwetu katoka kula wali wake na maharage na kipande cha embe dodo, akasema ngoja alale, akapanda kitandani kisha akajifunika blangeti lake vizuri na kuiweka vizuri simu yake, wakati anafanya hivyo, ukurasa wa akaunti ya facebook ya mwanahabari Robert Okanda ukafunguka, kisha picha ya Rostam Aziz ikaonekana.
Mwanakwetu akasema kimoyomoyo:
“Huyu Mnyamwezi wa Tabora Rostam Aziz kafanya nini usiku usiku? Au zile safari za kutusumbua sisi waungwana kwenda kumpeleka Tabora zimefika? Keshatema Bungo?”
Mwanakwetu huku akiwa na lepe la usingizi ndipo akaamua kuusoma huu ukurasa wa Robert Okanda, mpiga picha mkongwe na mwanahabari maarufu:
“Mfanyabishara Maarufu wa Afrika Mashariki na Kati ndugu Rostam Aziz kupitia kampuni yake ya Taarifa LTD amenunua hisa zote zilizokuwa zikimilikiwa na AgaKhan Fund For Economic Development (AKFED) katika Kampuni NPRT Holdings Africa Limited na hatua hii inafanya kuwa mbia Mkuu wa Nation Media Groups (NMG).”
Mwanakwetu akasema moyoni, huku akimlaumu nduguye Robert Okanda kwa kuipachika habari hii usiku huu, kwanini isingegoja kesho?
“Nilijua safari ya kwenda Tabora kwenye mibuyu na asali imefika…”
Mwanakwetu akajifunika vizuri ili alale, huku akilini mwake akamkumbuka rafiki yake mmoja aliyesoma naye Chuo Kikuu darasa moja na mwaka wa tatu darasa lao lenye wanafunzi karibu 60 wa Shahada ya Sanaa ya Habari wanafunzi wawili tu ndiyo waliochagua kusoma PRINT MEDIA nao ni huyu jamaa na Mwanakwetu.
Mwanakwetu pia akiwa kitandani kwake alikumbuka Julai 11, 2011 aliyekuwa mbunge wa Igunga CCM Rostam Aziz alijiuzulu ubunge wa jimbo hilo miezi tisa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2010. Wakati huo ndipo baadhi wa wanahabari wa TBC Taifa wakampachika Rostam Aziz jina la Hodari wa Kutema Bungo.
“Kwa wale ambao hawatokei Pwani ya Tanzania Bungo ni aina la tunda la msituni, hasa maeneo ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam , Lindi , Mtwara ambalo lenyewe linakuwa na ukakasi likiiva unalipasua na kuchukua tunda zake na kuziweka mdomoni huku ukizimung’unya kwa muda mrefu na unapofanya hivyo utapata ile radha ya Bungo yenye ukakasi kama inavyofanyika kwa Ubuyu.”
Haya msomaji wangu tambua kuwa Mwanakwetu yu kitandani kwake anayakumbuka tu haya yote kwa sababu ya lile Bango katika ukurasa wa Robert Okanda kwenye mitandao ya kijamii, huku Mwanakwetu akisema kuwa huyu Rostam Aziz Hodari wa Ubuyu Mabungo Hayawezi.
Mwanakwetu baadaye aliuchapa usingizi.
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini ?
Mwanakwetu anampongeza ndugu yake Rostam Aziz kwa kufanya huu uwekezaji mkubwa katika vyombo vya habari katika Afrika ya Mashariki na Kati na hili ni jambo zuri na la kupigiwa mfano kwa Mtanzania mwenzetu maana ametutoa kimasomaso. Ni ukweli usiopingika kuwa Agakhan ameifanya kazi hii nzuri kwa miaka mingi na inavyoonekana siyo kwa mradi huu wa vyombo vya habari tu bali hata kwa miradi ya Elimu na Afya inayosimamiwa vizuri na taasisi yao kwa Afrika Mashariki hata kabla ya uhuru huku kwa vyombo vya kwa Tanzania Magazeti mawili dada ya Mwananchi na Citizen yalianza kazi wakati wa Utawala wa Rais Benjamin Mkapa baada ya Rais Mkapa kumuomba Agakhan afanye hivyo na alikubali.
Kwa ndugu yetu Rostam Aziz tambua kuwa
“Yale mambo yetu ya kuweka mpira kwapani kama ya pale Shule ya Msingi Nzega haya tuyaweke kando maana umetutoa kimasomaso lakini mikoba ya Agakhan ni mizito inahitaji kweli uhodari na umakini wa hali ya juu kuwaudumia watu zaidi ya milioni 350.
Tambua kuwa Agakhan katika kipindi chote hiki hakuingiza siasa katika vyombo vyake, alijitahidi kutoa nafasi huru kwa vyama vyote vya siasa na hata kwa makundi yote huku Kenya, Uganda na Tanzania tukiwa na migawanyiko mikubwa na bado vyombo vyake viliaminiwa na huku hata muda mwingine kufungiwa na serikali na wanahabari ambao hatukuwa tunafanya kazi huko tulipaza sauti pale vilipofungiwa kwa kutambua mchango wao kwa jamii yetu.
Kwa hakika vyombo vya habari kwa Afrika Mashariki na Kati bado vina jukumu kubwa la kusimamia utendaji kazi wa serikali zetu kwa namna ya uhuru zaidi, huku vyombo vya habari vya serikali vimekuwa vikitoa nafasi finyu ya maoni ya raia wake,vyombo vya habari vya serikali ni majukwaa ya viongozo tu kwa hiyo ujio wako wa kishindo isije ikawa isije ukawa mkakati wa kudhoofisha Vyombo vya Habari Binafsi katika kwa ukanda huu. Hili litakuwa baya sana kwa umri wako maana wewe sasa ni mzee wetu, yasitokee yale kama ya mwaka 2011 pale jimboni Igunga.
Kwa hakika ubuyu ni tunda la polini kama lilivyo bungo lakini ubuyu umekuwa ukiwekewa radha kadhaa na kuwa mtamu wakati kwa asili ubuyu ni mchachu kama bungo, tunda la Bungo limebaki kama lilivyo hakuna wa kuliwekea ladha . Kwa hakika siasa ni ubuyu nalo bungo ni taaluma ya habari viwavyo na iwe lazima ibaki vile vile na ndiyo maana maamuzi yako ya kuingia kwa miguu yote katika vyombo vya habari yanaibua maswali mengi juu ya usalama wa taaluma hii, kwa nini iwe sasa? Je ujio wake hauna nia ya kuharibu ladha ya bungo letu tunayoifahamu?”
Swali linalobaki je Rostam Aziz mfupa huu atauweza au yeye ni Hodari wa Ubuyu Mabungo Hayawezi?
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Hodari wa Ubuyu Bungo Haliwezi.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257

.gif)
.gif)




Post a Comment