Hakuna wa Kukuroga

 

Adeladius Makwega-MBAGALA.

Machi 21, 2026 Mwanakwetu alialikwa Kata ya Kwemashai iliyopo Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga, katika Sherehe za Idd Al Fitr ambapo Waisilamu wa kata hii walimuomba ndugu yao Mwanakwetu akale pilau la sikukuu hii.

Inawezekana msomaji wa Mwanakwetu haifahamu sherehe hii ni nini?

“Idd al Fitr ni sikukuu kubwa ya dini ya Kiisilamu inayoadhimishwa mwishoni mwa mwezi wa Ramadhani baada ya mwandamo wa mwezi, ikimaanisha sikukuu ya kufungua funga ya Ramadhani, maadhimisho haya kikalenda huadhimishwa tarehe mosi Shawwal kwa sala maalumu ya asubuhi, kutoa sadaka-Zakat al Fitr kwa wasiojiweza, kuvaa nguo mpya, kutembelea ndugu na kula vyakula pamoja na marafiki, ndugu, jamaa na familia.”

Msomaji wangu nadhani itakuwa hekima kama nitaeleza kwa kifupi kalenda ya dini ya Kiisilamu inayofahamika kama Hijl Waswahili wa Mbagala wanaita Hijilia ambayo ina miezi 12 yenye siku 354/355, miezi hiyo ni:

“Muharram-1, Swafar-2, Rabiul-Awwal-3,Rabii Thani-4 Rabi m Jamadal uula 5, Jamasal- Thanil-6, Rajabu-7, Shaaban-8, Ramadhan-9, Shawwal-10, Dhul-Qaadah-11 na Dhu-Hijjah-12. Huku mwaka wa 2026 kwa mwaka Hijilia ni mwaka 1447 AH.”

Haya yote yalikuwa ni uelewa kwa msomaji wa Mwanakwetu juu ya Sikukuu hii kubwa ya dini ya Kiisilamu.

Mwanakwetu alitoka kwake Mbagala majira ya asubuhi na hadi anafika Kwemashai ilikuwa majira ya 10 ya jioni.

 

Hapa alipokelewa nyumbani kwa Diwani wa Kata hii mheshimiwa Jafari Nkupe kwanza alikaribishwa na chakula kizuri katika nyumba hii kilichopikwa na Shufaa Ramadhani Binti Shemweta ambaye ni mke wa Diwani wa Kata hii. Mwanakwetu alikula chakula hicho kitamu.

Kumbuka wakati wa kula hakuna kuongea na alipomaliza yalifanyika mazungumzo kidogo. Wakati mazungumzo haya yanafanyika mheshimiwa Nkupe alipiwa simu na mtu mwigine waliongea mazungumzo kadhaa yakiwamo haya:

“Wewe mbona msikitini hakuja kusali leo? Ni kweli sikuja kusali leo, Unajua ndugu yangu siku hizi ninavyoingia kulala huwa sifahamu kesho yake ninaamkia wapi, yaani nilienda kupandisha mitamba ya ndugu zetu lakini nakuja kwako unipe hekima je kama sala ya Idd naweza kulipa? Kama sala ya Idd inalipika basi nitafanya hivyo, hapa ndiyo narudi nyumbani. Sasa ukifika kwao uje kwangu hapa nina mgeni ndugu yako Makwega yupo… sawa nakuja…”

Mwanakwetu alipewa soda akanywa kisha, akaanza kuzunguka nyumba zote alizoalikwa na kila alipofika Mwanakwetu alikula matonge kadhaa ya wali uliyopikwa na akina mama wa Kata ya Kwemashai ambao ni wanawake hodari mno kwa kupika. Sasa ili kuweka nafasi ya kula angalau matonge matatu kila nyumba anayopita hekima ilikuwa ni kula kidogo kidogo. Baadaye ikanyesha mvua kubwa , hivyo basi wakajificha katika nyumba moja kama saa nzima na baadaye waliendelea na jukumu lao la kuzunguka kula pilau ya Idd Al Fitri hapa Kwemashai Wilayani Lushoto.

Mvua ilipokata Mwanakwetu  na ndugu zake kadhaa wakarudi nyumbani kwa mheshimiwa Jafari Nkupe. Walipofika hapa wakakutana na yule ndugu aliyekuwa hakusali sala ya Idd ambaye alinuia kulipa sijuhi wanazuoni wa dini hii walimjibu nini? Shida ni kutokana na kuwa bize kupandisha mitamba huko vijijini, ndugu huyu anaitwa Abadallah Salim Shemdoe.

 

Mwanakwetu akasalimiana na ndugu Shemdoe na kisha kuongea mambo kadhaa hasa suala la ufugaji katika kata hii:

“Makwega hapa kata yetu ufugaji ndiyo kila kitu , katika kitongoji kimoja unaweza kukuta ni watu 4 mpaka 5 tu ndiyo hawana ng’ombe za kisasa na hilo ni uvivu wao tu,  kila mtu anafunga ng’ombe wa kisasa na wanatoa maziwa na maziwa haya yananunuliwa vizuri na hata juzi wamekuja Wapemba wananunua ng’ombe mmoja hadi milioni mbili , wanakijiji wa Kata ya Kwemashai wanaheshimu ufugaji mno.”

Mazungumzo haya Mwanakwetu na ndugu Abdallah Bini Shemdoe yanaendelea:

“Mwanzoni wanakijiji walikuwa na ng’ombe za kizamani lakini baadaye walibadilisha mpaka sasa tija wanaiona. Kama unakumbuka mwaka wa 2017 nilipata mafunzo ya upandishaji wa mitamba chuo cha Nike Arusha kwa kulipiwa na Idara ya Mifugo iliyokuwa inaongozwa na ndugu Eliezer Moses, nikalipiwa shilingi 1000,000 ya kitanzania nikakaa hapo chuoni hadi nikahitimu na sasa nimeona faida ya kazi hii. Hapa napandisha mtamba mmoja kati ya shilingi 20,000- 50,000 na kwa siku napandisha kwa wastani mitamba 4-7 na kwa mwezi napandisha hadi mitamba 100.”

Mazungumzo haya yakiwa yanaendelea huku kijijini ngoma ya dufu ikipigwa mitaani vijana watoto wakike kwa wakiume wakiwa wamevaa nadhifu wanapita na ngoma hii mitaani. Mazungumzo haya yakawa yanaendelea:

“Unajua Makwega wakati ule ilikuwa tunapandisha ng’ombe 5- 10 kwa mwezi lakini sasa mimi nazunguka wilaya nzima ya Lushoto hadi Bumbuli, mathalani Machi 20, 2026 nilikuwa Kongei , Ubiri , Mhelo na Mlalo.”

Ndugu Shemdoe alimuuliza Mwanakwetu wa lini hapo Kwemashai? Mwanakwetu alijibu kuwa ndiyo anaingia kutoka Mbagala na amekuja kula Idd al Fitri Kata ya Kwemashai.

“Makwega wewe unashida sana unakuja kwa kushitukiza? Usifanye hivyo! Ungesema mapema leo ungeondoka dumu la mtindi, dumu la samli, dumu la maziwa fresh sasa leo Mwanakwetu utaondoka na mikungu ya ndizi na kabichi tu, kwanini unakuja kwa kushitukiza?”

Mwanakwetu akajibu kuwa anaogopa Kurogwa na Wasambaa, Wapare na Wambugu. Hapa ndugu Abadallah Shemdoe akacheka akisema:

“Makwega hapa Kwemashai, Lushoto Tanga na hata nchi hii wa kukoroga hakuna, wapo wale wakukaa vikao tu, watakaa wee, watasema hili na lile wee lakini wakukuroga akafanikiwa hayupo…Sisi tupo muda wote tunashikilia mafiga yetu huku tukikutaja Makwega, Makwega Makwega Ngwana wa Makwega(Mtoto wa Makwega.)”

Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba utambue kuwa kulingana na mila za Kisambaa wachawi wakiwa wanaroga wengine huwa wanakuwa wanakaa jikoni sehemu wanapopikia chakula katika mafiga matatu hasa wanawake huku mikono yao imeshika mafiga , yakitamkwa maneno kuhakikisha ule uchawi unakuwa na nguvu ya kumfikia yule anayerogwa. Huku hata wale wanaokulinda hufanya hivyo hivyo kuzuia wabaya wasikufikie kwa uchawi wao.

 

Baadaye mvua ilipungua nayeye Mwanakwetu kuanza safari ndefu ya kurudi nyumbani kwao Mbagala mwendo saa karibu 10 kutoka Lushoto Tanga.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu anawashukuru sana ndugu zake wa Kata ya Kwemashai Lushoto Mkoani Tanga kwa kumualika kula Idd Al Fitri na huku akiomba samahani kwa baadhi ya nyumba alizoalikwa alishindwa kufika kutokana mvua kubwa ilivyokuwa ikinyesha lakini pia kutokana safari ndefu ya kutoka Mbagala kwenda Lushoto.

Mwanakwetu anawapongeza wakazi wote wa Kata ya Kwemashai kwa kuwa wafugaji wazuri wa ng’ombe wa kisasa, hongereni sana maana taarifa alizozipata kutoka kwa mpandishaji Ng’ombe maarufu Wilayani Lushoto Abadallah Salimu Shemdoe zimemtia moyo. Mwanakwetu kwa makala haya anamuomba Mkuu wa Wilaya ya Lushoto amtembelee huyu ndugu aone juhudi zake zilivyo kwa manufaa ya wananchi wa wilaya hii.

 

Pia Mwanakwetu anamuomba mbunge wa Lushoto Profesa Riziki Shemdoe amsaidia huyu mpandishaji mitamba ya ng’ombe usafiri wa pikipiki ili aweze kuwafikia wafugaji wengi na katika huu msaada Mwanakwetu anamuomba Profesa Shemdoe pia amsaidie huyu mdau wa ufugaji mtungi mpya wa kuhifadhi mbegu ambapo madukani unauzwa shilingi za Kitanzania kati ya 700,000-1000,000. Kuliweka jambo hili vizuri mhe. Riziki Shemdoe hii pesa nashauri itapatikane kutoka mfuko jimbo.

“Mwanakwetu kwa binafsi yake anakuomba mheshimiwa Waziri msaidie huyu jamaa anawasaidia sana ndugu zako.”

Katika hili Mbunge wa Mlalo mheshimiwa Rashid Shangazi ambaye ni rafiki yake Mwanakwetu, huyu mpandishaji mitamba anafika mpaka jimboni kwako, nakuomba wewe angalia umsaidie Abdallah Salim Shemdie atembelee wakulima na wafugaji wanaofuga kisasa kama vile mzee wetu Mizengo Pinda  kule Dodoma ili elimu hii ya ufugaji iwe chachu wa watu wa Lushoto.

“Ndugu huyu jina lake ni Abdallah Salim Shemdoe na namba yake ya simu ni 0785459760.”

Mwanakwetu upo ?Kumbuka:

“Hakuna wa Kukuroga.”

Idd Mubaraka.

makwadeladius@gmail.com.

0717649257


















 


 

0/Post a Comment/Comments