Hii ilikuwa mapema ya Machi 19, 2026 Mwanakwetu alipokea simu kutoka kwa Diwani wa Kata ya Kwemashai iliyopo Lushoto Mkoani Tanga, mheshimiwa Jafari Nkupe huku akimualika katika Sikukuu ya Idd.
Mheshimiwa huyu akisema maneno haya:
“Ndugu yangu Kazimbaya hivi unajua sikukuu ya Idd inawezekana ikawa Machi 20 au 21, 2026 jitahidi ndugu yangu njoo tusherekee Idd. Pamoja.”
Mwanakwetu akaupokea mwaliko huu kwa mikono miwili maana ukiwa mwaliko wa kwanza aliyoupokea kwa sikukuu hii, huku akisema atajitahidi aende huko kula pilau ya Sikukuu hii ya Waisilamu.
Kisha yalifanyika mazungumzo kadhaa ya kidugu baadaye Mwanakwetu akamuuliza ndugu yake huyu je kuna mapya yoyote ?
Mheshimiwa Jafari Nkupe ambaye alikuwa diwani mdogo kuliko wote mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2015 akajibu kwa maneno haya:
“Nimepokea taarifa za tanzia kuwa ndugu yetu Lukas Shemndolwa ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Lushoto kwa miaka 15 amefariki dunia huko Dar es Salaam ambapo alikuwa anatibiwa…”
Mwanakwetu alishituka mno kwa msiba wa Ndugu Shemndolwa ambaye ameiongoza Halimashauri ya Lushoto tangu mwaka wa 2005 ikiwa pamoja na Bumbuli hadi zilipotenganishwa, hata zilipotenganishwa ndugu Shemndolwa aliendelea kuongoza Halmashauri hii hadi mwaka wa 2020 na huku Mwanakwetu alifanya nae kazi kabla ya kuhamishiwa Halmashauri ya Mbozi.
Lukas Shemndolwa ameiongoza Halmashauri hii kwa vipindi tafauti huku kukiwa na Wakurungenzi kadhaa akiwamo Lucy Msofe, Jumanne Kiango Shauri, Kazimbaya Makwega na wengineo na pia akifanya kazi kwa karibu na Wakuu Wilaya ya Lushoto kadhaa akiwamo Alhaji Majidi Mwanga.
Hata alipotafutwa katika simu yake ya mkononi Alhaji Mwanga simu yake ilikuwa inatumika.
Kipindi cha mwisho cha uenyekiti wake wa Halmashaur Mkuu wa Mkoa wa Tanga alikuwa ni Mheshimiwa Martine Shigella na Katibu tawala Mkoa alikuwa Injinia Zena Said.
Kulingana na taarifa kutoka katika familia ya marehemu Shendolwa inayoishi Malindi, Lushoto mkoani Tanga ilisema kuwa taratibu za kuusafirisha mwili kutoka Dar es Salaam kuelekea Lushoto Tanga zinafanywa ili mazishi yafanyika nyumbani kwake Malindi.
Lukas Shemndolwa alikuwa Diwani wa Kata ya Malindi kwa miaka kadhaa huku akizaliwa na makabila mchanganyiko ya Lushoto ikiwamo Usambaa, Upare na Mbungu na alikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha zote hizo za makabila haya.
Lukas Shemndolwa alikuwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mara baada ya kutimu Chuo Kikuu hiki wazazi wake walimwambia arudi Lushoto Mjini katika makazi yao hapo Malindi na kusimamia miradi kadhaa ya familia hiyo hadi alipoingia katika siasa kupitia Chama cha Mapinduzi.
Mwanakwetu kwa kuwa alifanya kazi Lukas Shemndolwa kama Mwenyekiti wake Wilaya ni Lushoto tangu Julai 12 2016 hadi Agosti 15, 2018 ambapo Mwanakwetu alihamishiwa Wilayani Mbozi hapa anaungama wazi kuwa mara zote pale alipokuwa na changamoto katika hili na lile ndani ya kipindi cha miaka mitatu alimpigia simu ndugu Shemndolwa au kufunga safari hadi Malindi Lukozi nyumbani kwake kumuona ili kupata ushauri wa hili na lile na mambo yalikuwa mazuri.
Mwanakwetu anaungama wazi :
“Lukas Shemndolwa alikuwa Mwenyekiti mtulivu na mwenye hekima sana…
lakini kidole kimoja hakivunji chawa hekima na uimara wa kiongozi mmoja unahitaji nguvu ya walimzunguka ili aweze kufikia shabaha ya jamii nzima maana kiongozi mmoja muda mwingine anaweza kuchoka au kukata tamaa kulingana na mazingira yanayomzunguka.”
Mwanakwetu kwa heshima ya marehemu Lukas Shendolwa ameukumbuka wimbo huu:
“Amenena Mwenyewe Haleluya , Utaishi Ukitazama, Amenena Mwenyewe Haleluya, Utaishi Ukitazama, Amenena Mwenyewe Haleluya , Utaishi Ukitazama.
Tazama utaishi Ipasavyo , kumtazama Yesu. Amenena Mwenyewe Haleluya Utaishi Ukitazama…”
Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa Jina la Bwana Lihimidiwe Ameni.
“Buriani Lukas Shemndolwa.”
0717649257

.gif)








Post a Comment