Waziri wa Mambo ya Kigeni Tanzania Anazamisha Jahazi

 



Adeladius Makwega-MBAGALA

“Utawala wa Rais Ali Hassani Mwinyi tangu 1985 hadi mwaka 1995 nchini Tanzania ulikumbwa na misukosuko mikubwa ya kisiasa na kikatiba, hasa mwanzoni mwa miaka ya 1990 hadi wakati wa uchaguzi wa mwaka 1995, kipindi hiki kuliibuka shida ya Organisation of Islamic Cooperation (OIC). Suala ili lilihusu Zanzibar kujiunga kwa siri na OIC bila idhini ya Serikali ya Muungano, kadhia hii ilisababisha mvutano mkubwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Swali la kujiuliza Rais wa Zanzibar wakati huo ndugu Salmin Amour hakumwambia lolote Mzee Mwinyi juu ya OIC? Je Mzee Mwinyi alikuwa hajui?

Kwa hakika ukisema kuwa Salmin Amour hakumwambia Ali Hassan Mwinyi juu ya OIC ni uwongo, hapa kuna kila dalili za kuchezeana shere.

Disemba 1992, ilibainika kuwa Zanzibar ilikuwa imejiunga na OIC. Hatua hii ilichochewa na baadhi ya Wazanzibari ambao hawakuridhika na nafasi yao ndani ya Muungano na walitaka kujiunga na shirika hilo. Hatua hiyo ilikuwa ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani masuala yote ya mambo ya nje ni ya Muungano, si ya upande mmoja wa Muungano. Serikali ya Mwinyi ilijiumauma vidole katika kadhia hii.

“Hali hiyo ilisababisha upinzani mkubwa kutoka Tanganyika, ikiwemo shinikizo kutoka kwa kundi la wabunge 55 (G55) waliotumia tukio hilo kupendekeza mfumo wa serikali tatu ya Tanganyika, Zanzibar na Muungano.

Julius Nyerere alikuwa hai aliikosoa vikali serikali ya Mwinyi kwa kuruhusu ukiukwaji huo wa katiba, akisisitiza kuwa dola isiyoegemea dini haipaswi kuwa mwanachama wa OIC na Mungu bahati Agosti 1993 Zanzibar ilijiondoa kutoka OIC na matokeo yake yalikuwa hata kuondolewa kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano John Samuel Malecela.”

Haya msomaji wangu ni historia ya Tanzania wakati huo.

 


Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika hali ilivyokuwa miaka ya 1990 inafanana na hali ya sasa ya Tanzania, Waziri wa Mambo ya Kigeni ni Mzanzibari na Rais wa Muungano ni Mzanzibari, Wazanzibari wanalo Bunge lao, wanaye Rais wao, nani anatetea maslahi ya Tanganyika katika hali kama hii? Je hayawezi kutokea kama yaleyale ya mwaka 1990 ya OIC? Hapa Wazanzibar wameshika hatamu mbili za Muungano na za Zanzibar.

“Nafuu ya mwaka 1990 Nyerere alikuwa hai, Nyerere alikuwa na nguvu ndani ya CCM, Nyerere alikuwa anaheshimika na Nyerere alikuwa anaogopwa pia n ahata Nyerere hakuwa kiongozi mwenye maslahi ya kibiashara na kampuni yoyote ile. Nani anayeweza kuvaa koti la Nyerere kwa Tanzania ya sasa? Jibu lake hayupo.Walio wengi walioshika nafasi wanakosa sifa za Mwalimu Nyerere., Watanganyika ni wakiwa.”

Katika hali kama hii ndiyo kusema yaleyale ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ni zaidi ya OIC ya mwaka 1990, hali ni tete.

Huyu Ahmed Hassan Diria wa sasa anaongea nini anapozungumza na vyombo va habari viwe vya ndani au vya kimataifa?

“Haiwezekani Waziri wa Mambo ya Kigeni kutetea kuzimwa mitandao, haiwezekani Waziri wa Mambo ya Kigeni kutoonesha huzuni kwa watu waliopigwa risasi kufa na wengini kubaki vilema huku wengine wakiuguza vidonda hadi leo.”

Je huyu Ahmed Hassan Diria anapokuwa na Ali Hassani Mwinyi wanaongea nini? Na hata wakiwa na ndugu yao Salmin Amour dhidi ya hawa Watanganyika wanajadili nini?

“Kama watu walifanya uhuni wakati Julius Nyerere akiwa hai sembuse leo hii? Huku Nyerere amelala Mwitongo Butiama?”

Mwanakwetu anasema wazi kuwa huyu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania wa sasa Mtoto wa Thabiti Kombo, nduguye Ahmed Hassan Diria nafasi yake ya Uwaziri wa Mambo ya Kigeni hakuna kinachofanyika, hali na Watanzania tangu udhalilishaji, kutekwa, kuuwawa na haya yale ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata anazidi kutupeleka gizani.

Mwanakwetu anaamini kuwa kwa sasa mtoto wa Thabiti Kombo cheo chake cha mwisho kiwe hiki hiki kama ilivyokuwa kwa Ahmed Hassan Diria miaka ya 1990 wakati wa kadhia ya OIC maana hali ya sasa ni OIC mara dufu.

“Kwa sasa Waziri wa Mambo ya Kigeni Tanzania ameshindwa kabisa kuonesha uhodari wa baba yake marehemu Thabiti Kombo ama kweli Mzee Thabiti Kombo amepata hasara, kumbe ni kweli mkwezi hawezi kuzaa mkwezi. Waziri wa Mambo ya Kigeni Tanzania Anazamisha Jahazi.”

Mwanakwetu upo?

Je makala haya yaitwaje? Sheikh Thabiti Kombo Amepata Hasara? Au Waziri wa Mambo ya Kigeni Tanzania Anazamisha Jahazi? Vichwa vyote Mwanakwetu kavipenda lakini msomaji wangu kumbuka Waziri wa Mambo ya Kigeni Tanzania Anazamisha Jahazi.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

 




 

 

 

0/Post a Comment/Comments