Waziri wa Mambo ya Kigeni Tanzania Yanamgoja Yaleyale ya Balozi Ahmed Hassan Diria

 



Adeladius Makwega MBAGALA

Kwa sasa Tanzania inapitia kigumu sana ambapo baadhi ya watu wanaweza kulinganisha hali hii na ile ya miaka ya 1990, lakini kwa hesabu za Mwanakwetu anaona kuwa hali ya sasa ya Tanzania ni tete kuliko ile ya miaka1990 kuelekea uchaguzi wa vyama vingi.

Kwa nini Mwanakwetu anaamini hili?

Kwa hesabu za Mwanakwetu anaamini kuwa yapo mambo yanayofanana kiasi ikiwamo lile la rais wa sasa anatokea Zanzibar siyo hili tu bali hata Waziri wa sasa anayeshughulikia mambo ya Kigeni ni Kijana wa marehemu Thabiti Kombo ambaye ni Mzanzibari chotara kama alivyokuwa mheshimwa Ahmed Hassan Diria wakati ule na ndugu Ali Hassan Mwinyi.

Mwanakwetu amekuwa akimfuatilia kwa karibu huyu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania namna alivyo, hulka yake inalingana fika na marehemu Ahmed Hassan Diria, ulinganifu huu umempa tafakari kubwa Mwanakwetu akisema kuwa kama yalivyomkuta Diria ndiyo itakavyokuwa kwa kijana wa marehemu Thabiti Kombo.

Mwanakwetu anaona kuwa kijana wa Thabiti Kombo amekosa sifa moja kubwa ambayo alikuwa nayo Baba yake mzazi marehemu Sheikh Thabiti Kombo ambapo mzee Kombo alilijua hili vizuri:

“Hili Zanzibar kufanikiwa katika Muungano lazima kuhakikisha Tanganyika ambayo imepoteza kila kitu katika muungano inakuwa na utulivu, inakuwa salama, inakuwa haina malalamiko na kama yapo basi machache maana mara zote Zanzibar haiko salama. Tanganyika ikiwa katika kaa la moto Zanzibar inakuwa majivuni. Hata CCM kubaki salama ni usalama wa Tanganyika tu, hakuna kingine ambapo ni sawa na mama mwenye mtoto anayetembea kwa miguu umbali mrefu, bega moja likichoka unaibadilisha mbeleko bega lingine sasa huyu mama mwenye mtoto apate kipindupindu, safari itaendeka?”

Kwa sasa ukimtazama huyu waziri wa mambo ya kigeni namna anavyojieleza katika vyombo vya habari ,iwe vya ndani au vya kimataifa kuna kasoro kubwa kadhaa:

“Haoneshi huzuni, haoneshi masikitiko, haoneshi kutubu, haoneshi kuomba radhi, mazungumzo/ maneno yake hayaponyeshi majeraha bali yanatoa gamba gumu la kidonda kilichoanza kupona na kukirejesha kidonda kibichi huku kikitiririka damu na maji na kibaya zaidi majibu ya maswali yake kila anapoyatoa hajaridhishi wauliza maswali, bali yanaonesha kuthibitisha baadhi ya hoja zinazoibuka.”

 

Katika hili Mwanakwetu anakumbuka maneno haya aliambiwa na Wakwere:

“Mwanakwetu sikia -Jakaya Kikwete alikuwa Mbunge mtembea pekupeku, haiwezekani Mbunge mtembea pekupeku amzae mbunge mtembea peku peku. Ridhiwani Kikwete hawezi kuwa mbunge makini kama baba yake, maana Ridhiwani Kikwete ni mbunge mvaa viatu. Bila ya kufahamu kuwa raia wengi ni raia watembea pekepeku wavaa viatu wachache.”

Katika hili Mwanakwetu anasema:

“Mbunge mpiga kasia hawezi kuzaa mbunge mpiga kasia. Kwa kile alichokuwa anaishi baba mtoto hakifahamu kwa hiyo haya ndiyo ya Thabiti Kombo na Kijana wake waziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika mizunguko ya Mtoto wa Thabiti Kombo inalingana na changamoto zile zile za Ahmed Hassan Diria alipokuwa Waziri wa Mambo ya Kigeni hadi Tanzania ikaingia OIC na baadaye kushinikizwa kujichomoa OIC na hadi baadaye Ahmed Hassan Diria Mtanzania aliyekuwa chotara wa Kizanzibari na Kisomali mwisho alisalia tu na ubunge hadi anafariki dunia.

 

Kwa hakika Ahmed Hassan Diria alifanya kazi kama Mkuu Wa Mkoa huko Pemba na baadaye Balozi na mwisho Mbunge na Waziri.

Katika ngazi zote tatu Diria alipata tuhuma nzito na uwaziri ndiyo hoja ya Tanzania na OIC ikaibuka.

Balozi Diria alipokuwa mtumishi Ubalozi na baadaye Balozi alibebesha mzigo wa kuchochoa mgogoro baina ya Oscar Kambona, Abdallah Kassimu Hanga na Abeid Amani Karume , na aJulius Nyerere hadi hadi Abdallah Kassimu Hanga anapotea huku wengi wakiamini Diria ni miongoni mwa wale walitia kibiriti katika mafuta ya taa ya mgogoro huu.

Wakati Balozi Ahmed Hassan Diria ni Mkuu wa Mkoa huko Pemba alituhumiwa kutumia vibaya madaraka yake hata watu kufariki dunia huku visa kadhaa vikitajwa kwa mifano.

Kwa hakika hii shida ya Kifo cha Hanga inalingana fika na hali ya Tanzania ya sasa baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoa 29, 2025 Hanga yupo wapi, ndugu zetu wapo wapi?

 

Haya yote ukiyaona wanaolalamika ni Watanganyika ambapo ni sawa na ile kesi ya OIC walalamikaji walikuwa Watanganyika, inakuwaje Mwinyi kaingia huko? Huku yale ya udhalilishaji wa wananchi ndiyo yale yale yalitokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ambapo Diria alilalamikiwa tangu akiwa kijana mara bada ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwa ni viongozi wa awali kuteuliwa na Karume.

Mwanakwetu anaona fika kuwa Mtoto wa Thabiti Kombo kisiasa ameshapoteza na hawezi kudumu katika siasa tena na huu Uwaziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania ndiyo cheo chake ya Mwisho, Hawezi Kuvuka Hiki Kizingiti .

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Waziri wa Kigeni wa Tanzania Yanamgoja ni yaleyele ya Balozi Ahmed Hassan Diria.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeius@gmail.com

0717649257

 

 










 

0/Post a Comment/Comments