Unajua Sisi Wapambe ni Nuksi Sana

Adeladius Makwega-MBAGALA

“…mwambie bosi wako Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara kuwa akiwa anakwenda nje ya Mkoa awe anakumbuka kutuaga na sisi akina Mwanakwetu, maana sisi ndiye wapambe wenyewe na wapambe mara nyingi nuksi sana, sisi ni zaidi ya mwenye mali.”

Huu ni mjadala baina ya Mwanakwetu na Bi Adventina Chacha karani wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara mapema Februari 6, 2026 wakati Mwanakwetu alipokwenda kumuona Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt .Zabron Masatu.

“… Mwanakwetu RMO anaposafiri anatoa taarifa kwa Katibu Tawala Mkoa, kisha Wakuu wa Idara na Vitengo wote wanapatiwa taarifa lakini pia anatajwa mtu anayekaimu nafasi hii, wewe kama siyo Mkuu wa Idara na Vitengo hiyo nyaraka haikufikii lakini kama unamtaka anayekaimu niambie nikuelekeze umuone…”

Mwanakwetu akasema sawa huku akimwambia Bi Adentina Chacha kuwa lazima ubao wa matangazo uwe umebandikwa kuwa RMO MARA hayupo na yupo pahala kadhaa kwa kadhaa fulani ili siye wapambe nuksi tuwe tunafahamu.

Mwanakwetu akacheka sana kisha aliagana na bi Adventina Chacha akiwa anatoka hapa hapa alielezwa kuwa siku ya Februari 5, 2026 alijulishwa juu ya dazeni tatu ya vitabu vilivyopokelewa huku akiambiwa kuwa kulikuwa na dazeni nyingine mbili ya vitabu kutoka Wizara ya Afya ya Tanzania ambavyo:

“Menstrual Health And Hygiene Facilities na kingine ni Menstrual Health And Hygiene Products And Materials zote ni Took Kits na Edition 1, 2025.”

Mwanakwetu akiwa hapa hapa Ofisini kwa RMO Mkoa wa Mara Dkt.Masatu alikifungua Kitabu cha pili ambacho kilikuwa na kava gumu lenye picha ambapo mabinti watatu mmoja mwanafunzi na wezake wawili wakiruka kamba huku kando yupo baba mmoja mtu mzima akitazama zoezi hili.

Kitabu hiki kilipewa jina Menstrual Health And Hygiene Products And Materials, hapa hapa Mwanakwetu akafungua ukurasa wa yaliyomu na kuvutiwa sana na module ya tatu ambapo neno sodo lilikuwa ajenda kubwa.

Kitabu hiki kilisema kuwa Sodo yaweza kuwa kitambaa , nguo, kikombe au plastiki maalumu laini ambayo inatumika na mwanamke/msichana aliyepevuka kujihifadhi wakati wa hedhi.

“Zipo aina kadhaa za Sodo mathalani zile zinazotumiwa mara moja tu na kuteketezwa, zile zinazotumiwa zaidi ya mara moja na kufuliwa , zipo zile kama kikombe na zipo zile kama utambi .”

Haya ni maelezo ya Bi Flowina Muuzaji ambaye ni Mratibu wa Chanjo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara akimueleza Mwanakwetu aina hizo nne za sodo.

“Mara nyingi aina ya sodo zinazofahamika sana ni hizi zinazotumika na kuchomwa moto mara baada ya matumizi kwa wasichana/wanawake wakiwa katika hedhi ambazo ndizo zinazopopatikana kwa wingi maduka ya kawaida, maduka ya dawa na hata mahospitalini. Hii aina ya sodo tunaamini ipo salama maana imethibitishwa na mamlaka ya Chakula/Lishe na Vifaa Tiba.”

Gafla wakati elimu hii inamfikia Mwanakwetu akaingia mama mmoja anayefahamika kama Hellena Mligwa huyu ni mhudumu wa ofisi .

 

 MAMA huyu mpole sana akasalimiana na ndugu hawa kisha akaomba kitu alichokifuata na alafu akaulizwa hivi Hellena unazifahamu sodo zinazotumika zaidi ya mara moja? Bi Hellena akasema haya:

“Hizi ni sodo nzuri sana maana gharama ya kununua sodo kwa shilingi kati ya 2000-5000 kwa mazingira ya kimasikini nani anaweza? Hizi huwa ni vitambaa maalumu ambavyo hushonwa vizuri, kwa kitambaa chenye hali kama sponji ambayo inafulika vizuri. Hizi ni nzuri kwa wanafunzi na hata maeneo ambapo kunamakundi makubwa ya wasichana/akinamama. Shida yake ni moja tu inahitaji usafi wa kila mara.”

Mjadala huu ulikuwa mzuri sana nayeye Leah Daniel ambaye ni Mratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi na Mtoto akasema haya:

“Ipo aina nyingine ya sodo ambapo kunakuwa na kitu kama kikombe ambacho huwa kama plastiki laini ambacho kinawekwa pahala husika na kisha mwanamke akajihifadhi vizuri akiwa katika hedhi yake na kila kinapokuwa kimejaa anakwenda kuimwaga na kisha kukirejesha pahala pake baada ya kufanyika usafi hadi hedhi itakapokamilika.

Hii pia ni sodo ambayo gharama yake ni nafuu ukinunua umenunua huku usafi ni muhimu kufanyika kila mara.”

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yupo Idara ya Afya ya Ofisi ya Mkoa wa Mara ambapo mjadala huu juu ya Sodo unaendelea,  mara akaingia Dkt. Magreth Shaku kisha akauliza ehee leo Mwanakwetu kaja tena? Wenzake wakajibu ehee, Mwanakwetu yupo amejaa tele kama pishi la mchele Kyela.

 

Hapa hapa mhudumu wa Ofisi Bi Hellena Mlingwa akamuomba Dkt Shaku aeleze juu ya aina ya nne ya sodo.

Kwanza Dkt Shaku akauliza aina zote zilizotajwa awali alipojibiwa kisha akatoa maelezo haya:

 

“Ipo aina nyingine ya sodo ambayo inakuwa kama utambi ambao unamezwa ndani ya uke na wengine wanaita Tampons hii ikiwa ndani inakaa vizuri na kunyonya kila kitu kinachotoka. Mara nyingi hii inatumiwa na wanamichezo, wanawake wanaofanya kazi za mikiki mikiki iwe vitani, jeshini na hata wanawake viongozi maana lolote laweza kutokea muda wowote ule. “

Dkt. Shaku aliendelea kuelezea aina hii ya sodo ambapo aliongeza na haya:

“Kuna wakati nakumbuka Tanzania ilipata msaada kutoka CHINA katika masuala ya afya, hawa Wachina walileta sodo za aina hii. Kwa sasa sina hakika kama zinapatikana madukani kwa matumizi ya mtu mmoja mmoja lakini natambua hospitalini lazima ziwepo.”

Mjadala huu uliisha hapa hapa, kisha Mwanakwetu kurudi ofisini alipokuwepo na kuamua kuuweka mjadala wote huu katika makala haya unayoyasoma msomaji wangu.

Mwanakwetu Upo? Kumbuka

“Sisi Wapambe Ni Nuksi .”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 




 

 



0/Post a Comment/Comments