Tunapokuwa Pamoja Tunaishije?

 





Adeladius Makwega MBAGALA.

“Tanzania inawajibu wa kutembea kifua mbele kwa kuwa Baba Mtakatifu Leo wa XIV amewahi kuishi nchini Tanzania huku makazi yake, mabweni, Nyumba alizokaa, makanisa aliyosali na hata rafiki zake aliyokaa nao bado wapo hai, hivyo lazima tutumie fursa hii ili kukuza utalii”

Haya ni baadhi ya maelezo ya mapema Februari 2026 ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Mussa Azzan Zungu ndani ya kikao cha bunge la taifa hili akiwa na joho lake na siwa ikiwa mezani kwake.

 

Mwanakwetu ameyatafakari mno maelezo haya kwa namna yalivyotolewa, muda yalitolewa na hali ya taifa la Tanzania huku akilini mwake akiwa na vitu vingi ambapo kwa leo machache ndiyo yatajenga makala haya.

Kwako msomaji wangu nakuomba uyasome makala haya kwa umakini mkubwa hasa wale walei, Makatekista, Mashemasi, Maburuda, Masista, Mapadri, Maaskofu na Makadinali ambao naamini makala haya yaweza kuwafikia kulingana na maendeleo ya tekinolojia ya sasa yalivyo.

Makala haya yanawalenga hawa ndugu niliowataja lakini ni njia ya kuwafikia viongozi na wanasiasa wetu wa Tanzania ili wabadilike maana jamii ya Watanzania wa leo ni jamii nyingine kabisa.

 

“Mwaka wa 2025 Mwanakwetu alikuwa likizo , hivyo akiwa eneo alipo, alihisi usalama wake eneo hili ulikuwa mdogo sana hivyo kwa kuwa mara nyingine hupenda kwenda kusali dominika kwa kutembea kwa miguu aliamua kusali kanisa jirani na makazi yake.

Wakati huo ulikuwa ni wakati wa Kwaresma jumapili aliyosali eneo hili Padri aliyesalisha misa hii alikuwa anaitwa Padri Mpete ambaye umri wake ulikuwa mkubwa sana, huku kanisa hili dogo la Warosiminiani ambapo watawa wa wanovise hawazidi 15 , masista wakubwa wawili lakini pia walikuwepo vijana wasiozidi 10 wa malezi ya Upadri na siku hii kanisani Mwanakwetu alikuwa na wanawe watatu.

Padri Mpete, Padri mzee katika dominika hii alikuwa mchangamfu sana, muwazi sana na hata mahubiri yake yalionesha hilo.

Mara nyingi ibada za watawa huwa hazina sadaka, muumini ukiwa umesali katika ibada hiyo haina maana kuwa sadaka yako unabaki nayo mfukoni, hapana sadaka yako unaitoa na unaipeleka atareni na wao wenyewe watawa huwa wanazipeleka Parokiani kwa utaratibu wao. Kwa bahati mbaya katika Kanisa hili dogo huyu aliyeandaa ibada hii hawakuweka chombo cha sadaka, mimi wanangu tukaweka sadaka vizuri pembeni altare ibada ikasaliwa hadi mwisho.

 

Baada ya ibada kwisha Padri Mpete alikuwa nayeye ni mgeni lakini mwenyeji nadhani alikuwa ametoka Seminari ya Shirika hilo huko Kenya aliamua kurudi nyumbani, jumapili hii ya mwaka 2025 ndiye ilikuwa ya kwanza baada ya kutoka huko SEMINARI.

Padri Mpete mwishoni alijitambulisha hayo yote na siye yaani Mwanakwetu na wanawe wakajitambulisha pia.”

Maelezo ya Mwanakwetu yalikuwa haya:

“Mimi ninaishi jirani nanyinyi kwa kuwa tupo jirani na chapel yenu ndiyo maana tunakuja kudoea kusali kanisani kwenu kila ibada za misa zinapofanyika”

Tukaimba wimbo mzuri tukaagana na sie kurudi kwetu na hawa wanovisi, vijana wa malezi ya Upadri na Padri Mpete wakatawanyika kurudi kila mmoja kwenye makazi yake.

Mwanakwetu na wanawe wakaendelea kusali dominika zote katika kanisa hili dogo na kwa bahati nzuri dominika zilizofuata wale Rosimiani wakaweka bakuli jeupe juu ya stuli kwa ajili ya sadaka kwa hiyo adha ile ya kuweka sadaka altareni ikaondoka, wakijua kuwa sasa ipo familia moja inasali pamoja nao.

Katika jambo hili msomaji wanagu nakuomba ukumbuke hili:

“Mwaka wa 1990 ile ibada ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II (Sasa Mtakatifu) Septemba 2, 1990 yalisemwa maneno haya: Jamani ibada za Misa za Baba Mtakatifu huwa hazina sadaka lakini sadaka hii mnayotoa leo hii zinatumika kwa ajili ya huduma za kichungaji…”

Haya yanakumbukwa tu Mwanakwetu.

 

Mwanakwetu anasali katika Kanisa hili dogo vizuri tu,  huku wanakwaya Wanovisi na Vijana wa Malezi ya Upadri wanaimba nyimbo za misa wakijitahidi, japokuwa hawana zana bora za kwaya. Jumapili zinasonga sasa ni jumapili nyingine ya Kwaresma nadhani ya dominika za mwisho wa Kwaresma, akaja Padri mwingine kijana, akatusalisha vizuri kama siku zote, mahubiri akafanya vizuri tu huku akisitiza mno juu ya kuungama.

“Jamani eeeh hata Baba Mtakatifu nayeye anaungama, tujitahidi kuungama, wapo wanakuwa wazito kuungama kwa mapadri wao mathalani sisi ambao tupo pamoja shirikani, tunahofia yale maungamo kutumika kufanyia maamuzi katika maisha yetu shirika.

Hili mimi nakataa, hakuna padri anayeweza kufanya hilo. Kama yupo mkuu wa shirika Padri akatumia maungamo ya mnovisi au mwanafunzi wa malezi ya utawa, padri mwenzake hilo halipo.”

Mwanakwetu katika ibada hii alipowatazama waamini wote Kanisani siku hii tangu Padri wanovisi , wanafunzi wa mwaka wa malezi ya Upadri na wanawe alitambua kuwa kwa anavyoona yeye siku hii ndiye alikuwa na MKRISTO mwenye umri mkubwa kuliko wote kanisa.

Huku akitambua fika mtu aliyemtazama Mwanakwetu alijua ni kijana mdogo tu.

Ibada ya Misa ilifanyika vizuri wakati wa matangazo ulifika Padri huyu kijana ambaye nadhani alikuwa na nyadhifa katika Shirika, huku matamshi yake yalikuwa ya KICHAGA akawauliza wale wanafunzi wa malezi na Wanovisi

“Huyu aliyekuja kusali nasi mnafahamu? Huyu alikuja kusali nasi mnafahamu?”

Swali hili linamlenga Mwanakwetu .

Kijana mmoja mwembamba, mweusi ambaye nadhani alikuwa kijana wa mwaka wa malezi ya Upadri ambaye nadhani pia alikuwa kiongozi alijibu ndiyo tunamfahamu, hapa nadhani akirejea jumapili ile ya Padri Mpete aliyosalisha katika Kanisa lile la Warosiminiani ambapo vijana wa Mwanakwetu husali kila mara.Ibada ikaisha tukatoka vizuri kisha siye tukaanza kurudi kwetu.

Wakati tunarudi nyumbani mwanangu mmoja akawa anahoji… Baba inakuwaje kila siku sisi tunasali hapa Kanisani inakuwaje Padri anatuuliza sisi tunafahamika?

Mwanakwetu akamjibu :

“Vi vizuri kufahamiana kutokana na hali ya usalama wa dunia ilivyo na mashaka, mashaka yamekuwa mengi. Kama sisi tulivyoshindwa kwenda kusali Parokiani kwa hoja ya usalama wetu , nadhani ndivyo na Padri huyu hivyo hivyo… lakini hali ya usalama isiwe kikwazo cha watu kushindwa kusali .

Pia wanangu hapa tunaposali hawa Warosiminiani wakiwa Shirikani mwao wanatambuana kama Warosiminiani tu, Wale Makapuchini hivyo hivyo, wale Wadada Wadogo hivyo hivyo wale Wabenedictine hivyo hivyo.

Haya mashirika yao yanafunga katika sanduku hilo. Sisi huku nje hatufungwi na dhana hii.Jambo hili lazima mashirika yetu ya watawa walitambue Yesu Kristo hauwezi kumfungia katika dhana ya Shirika, dhana ya kikundi fulani.”

Mjadala unasonga huku tunarudi nyumbani:

Watoto wa Mwanakwetu wanasema Padri huyu amekosea kuuliza swali lile. Mjadala huu unaendelea huku familia hii inarudi nyumbani, Mwanakwetu akasema:

“Katika maisha binadamu kila mmoja anakosea iwe Padri, iwe Sista, iwe katekista, iwe Mchungaji iwe Kadinali iwe Baba Mtakatifu iwe mama yenu iwe mie baba yenu kukosea ndiyo ubinadamu na ndiyo maana Mungu katuandalia kitubio, siye sote wakosaji lakini tunapokoseana tusirudishwe nyuma juu ya Yesu Kristo, kwamba fulani kanikosea ndiyo basi, kila mtu ni mkosaji mie ninazo zangu na mwingine anazo zake, ndiyo maana tunaungama kama alivyosema huyu Padri Kijana .”

Watoto Mwanakwetu wakawa wanacheka:

Tukiwa tunatembea kushoto kulia mtoto wa Mwanakwetu mwingine akasimulia kisa hiki:

“Siku moja shuleni walikuja watawa kadhaa wakiwamo Mapadri na Masista tukaambiwa tuingie ukumbini, wanafunzi wote tukajaa ukumbini, katika ukumbi huo yakatolewa maelezo mengi juu ya kujiunga na shirika moja la watawa. Mwisho wa maelezo wakasema ambaye yupo tayari anyooshe mkono, kwa bahati mbaya hakuwepo hata mwanafunzi mmoja aliyefanya hivyo.

Mwishoni Kiongozi wa taasisi hii akasema nyinyi wanafunzi mnasoma shule ya dini lakini hamna malezi ya Kikristo kwanini mnakata kuwa watawa? Jamaa akaongea kisha wakaondoka na siye wanafunzi kutawanyika. Kwa hiyo Baba nikawa najiuliza hivi kuwa mtawa pekee ndiyo maaadili ya Kikristo?”

Mwanakwetu kumbuka anarudi nyumbani na kundi la wanawe huku akiulizwa swali hilo kisha Mwanakwetu akajibu:

“Ni kweli kanisa linahitaji watawa ambao wanaofanya kazi shambani mwa bwana lakini siyo lazima sote tuwe watawa… Jambo la msingi ukizaa mwanao akawa na wito usimkataze kuwa mtawa kwa sababu wewe ulishindwa hili siyo sahihi. Kama wewe unafedha changia wenzako ambao ni watawa na wana wito huko utawani.

Pia wale ambao ni watawa lazima maisha yao yawavutie vijana wetu ili wawe watawa kwa hiyari yao wenyewe maana kanisa ni mimi, wewe na yule huku tukivumiliana.”

Kweli baada ya dakika tano tulifika nyumbani tukanywa chai ya hii dominika kisha kila mmoja kuendelea na majukumu yake.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika kanisa ni mimi, wewe na yule huku tukiwa na madhaifu yetu pia tukivumiliana na pale tunapokeseana tunaombana misamaha na kutubu.

Rejea visa vya vijana wa Mwanakwetu wametaja mambo kadhaa .

 “…nyinyi mnasoma Shule ya Kanisa mnatakaa kuwa watawa hivyo hamna maadili ya  Kikristo…”

Aaah kwanini Padri anauliza kuwa sisi tunafahamika?

Watawa wale wakiyasoma makala haya na wakaziona hoja hizi siku nyingine hawawezi kuyasema haya yaliyonukuliwa katika makala haya n ahata ile dhana ya mashirika ya dini yasifikirie tu ndani ta taasisi zao Warosiminian, Wabenediktine,Wakapuchini, Wadada Wadogo hapana maana kwa Yesu hakuna mgeni, milango ipo wazi kwetu sote.

Hata hili la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya Mussa Azzan Zungu hoja siyo kumjengea maboresho, makumbusho Baba Mtataifu Leo wa XIV hoja ya msingi, hoja kubwa je sisi wenyewe kwa wenyewe tunaishije? Serikali inawatendeaje raia wake? Lazima tutendeane wema .

“Watu wanauliza nyinyi CCM mnakaaje wenyewe kwa wenyewe? Humphrey Polepole yupo wapi? Nani Kamteka? Mbona hamtoi majibu? Je watoto wetu wengine wanaofanya siasa na nyinyi watakuwa salama? Hata kama ujenge na kuboresha makazi yote aliyoisha Baba Mtakatifu Leo wa XIV, kama usalama wa raia haupo unafikiria nani atakwenda huko kutalii?”

Kwa hiyo ndugu yetu Mussa Azzan Zungu hoja ya msingi ni usalama wa raia, wenyewe kwa wenyewe Watanzania tunaishije? Hoja zingine kwa sasa hazina mashiko, kama ilivyojengwa hoja za watawa katika makala haya Bunge lijadili Ndugu Humphrey Polepole yupo wapi na wengine wote waliotekwa wapo wapi? Nani kawateka? Nani anafanya huu ujinga? Vijana Mwanakwetu ni wadogo lakini wanakagua maisha yao kila hatua na wale wanaishi nao, namna wanavyoongea bila wale wanaokaa nao kufahamu labda kwa hisani ya makala haya tu. Hawa vijana wa Mwanakwetu ndiyo Watanzania wenyewe Bunge letu lijifunze katika visa hivi vya kanisa.

Mwanakwetu upo ?Kumbuka:

“Tunapokuwa Pamoja Tunaishije?”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeius@gmail.com

0717649257







 

0/Post a Comment/Comments