Siyo Kila Mwenye PHD Anazo Mbinu za Kufundishia

 


Adeladius Makwega-MBAGALA.

Mwanzoni mwa Februari mwaka wa 2026 Mwanakwetu alitayarisha makala moja ambayo ilikuwa ya masuala ya uchumi juu hifadhi ya dhahabu.

Katika makala hayo Mwanakwetu aliwataja Maprofesa wawili: Honest Ngowi na Profesa Mafwenga, huku Mwanakwetu akisema wazi kuwa Profesa Honest Ngowi alikuwa ni mwalimu mzuri, anajua kufundisha alikuwa na mbinu za kufundishia na somo lake lilieleweka sana kwa wanafunzi wake.

Nchini Tanzania tatizo kubwa la elimu ya juu tangu Astashahada , Stashahada na Shahada, Shahada ya Uzamili na hata Shahada ya Uzamivu, elimu hizi zinafundisha na watu waliofanya vizuri masomoni lakini wengi wao hawana mbinu za kufundishia(Teaching Methodology) yaaani hawana kabisa na ndiyo maana elimu ya juu ni elimu yenye malalamiko mengi kuliko Elimu ya Msingi, na Sekondari nchini Tanzania, tatizo ni ukosefu wa mbinu za kufundisha hasa kwa wahadhili wengi.

Nafuu inakuja tu pale ambapo mhadhili husika kama alibahatika kusoma ualimu kwa ngazi yoyote ile, iwe cheti, Stashahada au Shahada akiwa mhadhili vyuoni anakuwa na nafuu kwa kuwa anafahamu mambo mengi ya UALIMU DARASANI.

Mwanakwetu kukataa mia kwa mia kwamba kuwa hakuna wahadhili hata mmoja mwenye uwezo wa mbinu za kufundishia ambao hawana elimu ya ualimu hapana, wapo lakini wachache mno inawezekana kumi yupo mmoja tu maana wapo baadhi ya wahadhili Mungu kawapa vipaji maana Mungu ni hodari wa kumtunuku yule amtakaye.

Katika hili Mwanakwetu anashauri haya:

“Vyuo vya Juu vinapotangaza kazi ya Uhadhili kama katika waombaji watatu yupo muombaji mmoja ambaye ana taaluma ya ualimu iwe ana cheti, Stashahada au Shahada kisha ana Shahada ya Uzamivu huyu mwenye vyeti vya ualimu ngazi ya chini ni mtu muhimu sana kusimamia taaluma ya watu, huyu apewe kipao mbele maana mwisho wa siku katika muktadha wa mazingira darasani hawezi kuwaletea matatizo.”

Mfano wa madhaifu ya wahadhili wengi hawana elimu ya UPIMAJI yaani namna bora ya kuyatengeneza matokeo ya wanafunzi, wanadhani mwanafunzi akifanya vibaya ni kosa lake peke yake.

 

Kwa hiyo ushauri wa Mwanakwetu anaviomba hasa Vyuo Vikuu na mamlaka zinaazosimamia jambo hili wawe nalo makini maana elimu kwa sasa ni uwekezaji wazazi wanalipa karo, elimu ni biashara. Wasimamie elimu hii kwa umakini lakini vigezo vya upimaji vizingatiwe.

“Maana matokeo ya wanafunzi yawe mazuri yawe mbaya yanatoa taswira ya taasisi, taswira ya mwalimu na taswira ya mwanafunzi na hata nchi ilipo taasisi hiyo.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Ukitaka kuliona tatizo hili ni la kweli tambua hii shida hauwezi kuiona katika Vyuo Vikuu vinavyotoa kozi za ualimu lakini balaa huko kwenye taasisi zingine mathalani Shule ya Sheria, kwenye Udaktari na hizi elimu nyingine ni kero. Siyo kila Mwenye PHD Anazo Mbinu za Kufundishia huko wapo wahadhili wanaona fahari wanafunzi wachache kufaulu.

“Wakifaulu wanafunzi wachache tambua kuwa imefeli taasisi, umefeli mwalimu na mwisho ndiyo amefeli mwanafunzi.

Mzazi gani atapoteza pesa yake kumpeleka mtoto wake katika taasisi hodari ya kufelisha?”

Jambo hili hata wale wanaokuwa Wakuu wa Vyuo wawe na chembechembe za ualimu maana watakuwa wakali kwa Wakuu wa Vitivo wakati wa mchakato wa matokeo kabla ya kubandikwa katika tovuti zao. Huku wahadhili wenye changamoto ya kufelisha katika taasisi za umma mathalani kama ni Shule ya Sheria wapangiwa majukumu mengine hata wawe mawakili mahakamani.Wahadhili wa ajira za mikataba wasipewe vipindi na wale ajira ya kudumu tufuatilie mienendo yao.

Mwanakwetu upo?

Je makala haya yaitwaje? Taswira ya Taasisi, Taswira ya Mwalimu na Taswira ya Mwanafunzi? Imefeli taasisi, Amefeli Mwalimu na Amefeli Mwanafunzi? Au Siyo Kila Mwenye PHD Anazo Mbinu za Kufundishia

Mwanakwetu vichwa vyote kavipenda. Wewe Msomaji wangu chagua kichwa kimoja kati ya hivyo lakini kumbuka

“Siyo Kila Mwenye PHD Anazo Mbinu Za Kufundishia.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257







 

 

0/Post a Comment/Comments