

Adeladius Makwega-MBAGALA
Siku hii wanahabari walikuwa bize sana maana eneo lao lilipokea ugeni wa aina mbili: Ugeni wa Sauti ya Kilimo na Ugeni wa Sauti ya Haki, huku kila mmoja alieleka huko alipoagizwa aende kulingana na makundi haya mawili. Nao wanahabari ili waripoti matukio haya wawili waligawanya katika makundi haya mawili. Kundi la Sauti ya Haki likiwana wanahabari wachache na kundi la Sauti ya Kilimo lilikuwa na wanahabari wengi, watu wakidai kuwa leo Sauti ya Kilimo wamependelewa.
“Kama mimi ningeenda katika Ugeni wa Sauti ya Haki kazi hii ningeifanya vizuri sana, lakini sina namna nipo huku…”
Hapa haya mwanahabari mmoja katika kundi la Sauti ya Kilimo akizungumza. Huyu mwanahabari akapiga simu kwa mwanahabari mwingine aliyepo katika kundi la Sauti ya Haki akiomba arekodiwe kitakachotokea kisha amtumie katika barua pepe yake ili akimaliza kazi hii ya Sauti ya Kilimo aifanye pia kazi ya Sauti ya Haki. Kazi huko Sauti ya Kilimo ilifanyika katika vituo viwili ambapo yote yalikuwa mashamba. Kazi ya Sauti ya Kilimo ilifanyika vizuri na kundi hili wakarudi na kuifanya kazi yao safi kabisa na habari zao kusambazwa. Wakati zoezi la kukamilisha kazi ya kwanza linakamilika-mhariri mmoja ambaye anatokea chombo kimoja miongoni mwa wale wanahabari waliopangiwa Sauti ya Kilimo akapiga simu .
“…Bwana Mdogo asante sana… nimepokea hii kazi ni nzuri lakini vipi kule kwenye Sauti ya Haki mbona haujanitumia?”
Bwana mdogo mwanahabari ambaye anajitambua vizuri, ana akili timamu na uwezo mzuri wa kuifanya kazi ya habari vizuri akamjibu mhariri wake:
“Kule mimi sijakwenda lakini waliokwenda huko nilimtuma ndugu mmoja, nasubiri anitumie materials husika ili niandae hiyo ripoti, nimepanga lazima niifanye na nitakutumia hivi punde.”
Kazi ile ya Sauti ya Kilimo ikawa sasa inarushwa katika runinga. mhariri akapiga simu tena.
“Vipi mbona bado?... nataka kuitumia katika taarifa ya habari ya usiku, fanya haraka....”
Kijana huyu makini mwanahabari akajiuliza kwa sauti ya chini hivi huyu mhariri mbona anahangaika sana…mtu mwingine akasema mithili ya kuku aneyetaka kutaga? Hii stori ya Sauti ya Haki nyuma ya pazia kuna nini? Jamaa kando akasema mhariri pengine keshawezeshwa, sasa wewe subiri kama kweli kawezeshwa simu itapigwa tu tena na atatoa maelekezo ya namna ya kuifanya hii ripoti. Huyu mwanahabari makini akatumiwa yale materials akayatengeneza vizuri huku akiingiza sauti yake ya ripoti hii ya Sauti ya Haki. Wakati hii ripoti inatengenezwa mhariri akapiga simu tena akisema maneno haya:
“… kama umeyapata yale materials hakikisha insert (sauti za ushahidi wa mashuhuda kwa ripoti au makala) zisiwe mbaya mbaya, ziwe nzuri naomba ziwe nzuri maana hii ni kwa habari ya saa mbili…”
Huyu kijana mwanahabari makini akauliza kwa sauti nzito unasemaje? Mhariri akajibu kwa kusisitiza hoja yake:
“…insert zisiwe mbaya mbaya, ziwe nzuri nzuri na hii kwa habari ya saa mbili…”
Kijana mwanahabari kulipotezea hili agizo haramu akasema sijakusikia vizuri, sijakusikia vizuri bosi. Kisha simu hii ikakatika huku msimuliaji wa makala haya hakufahamu nani aliyekata simu hii, kama ni huyu mwandishi makini au yule mhariri. Msomaji wangu nisikuache njia panda kwa heshima na taadhima ni vizuri kufahamu kidogo juu ya zile insert zilikuwaje?
“…watu wapo katika kikao wanatoa ushuhuda namna ndugu zao walivyouwawa,walivyopigwa risasi, wengine wakisema wamezika nguo na hawajapata miili ya ndugu zao hadi muda huo. Huku wengine wakiongea huku wakilia, sauti za vilio vikisikika…Pia sauti ya aliyekuwa anakusanya maoni hayo akitoa hakikisho kuwa kamati yao itafaya kazi vizuri kwa haki bila upendeleo wowote…makelele yakisikika.”
Baadaye hawa jamaa walitawanyika kisha kila mmoja kuelekea kwake. Bila ya kufahamika kama ile ripoti ilitoka au la. Mara baada ya tukio hili ndipo Mwanakwetu akaamua kuyaandika makala haya unayoyasoma msomaji wangu.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika katika vyombo vya habari va sasa iwe redio, iwe magazeti na hata runinga siyo vyombo vya kuviamini kabisa mia kwa mia maana katika redio, magazeti na hata runinga inawezekana mia kwa mia watu wakaamua kuzitengeneza habari wanazotaka wao ziwe kwa kutumia mamlaka yao, nafasi zao na hata uwezo wao wa kifedha. Hapa tazama kwa kina hii simulizi vizuri tangu wanahabari wanapangiwa kazi, aina ya wanahabari waliokwenda katika kila kazi, inawezekana mhariri huyu akapigiwa simu na kaandaliwa bahasha au kapewa ahadi ya nafasi fulani, huku inawezekana hawa wanaowapanga wanahabari wao ndiyo wanaotoa fedha za malipo kwa wanahabari siku ya kazi husika, hapa Anayemlipa Mpiga Filimbi Ndiye Anayechagua Wimbo. Mwanahabari mmoja pekee hawezi kwenda pahala fulani kwenye tukio muhimu kama hajaalikwa na hana kipato cha kumfikisha huko.Kama mwanahabari akijitahidi kujitutumua kufanya kazi ya jamii na hana kipato lazima mazingira yatakuwa magumu kwa kutumia kanuni, sheria na hata uchumi, vyombo vya ulinzi n ahata mamlaka za Mawasiliano kwa kuvifungia ndiyo yale ya Humphrey Polepole na Dkt.Jabiri Bakari aka Mkata Swichi.
“Kama wenye nacho wanaweza kugharamia kila kitu kwa kuvialika vyombo va habari kwa kazi zao –pesa hii ipo katika Bajeti Kabisa au kwa kutumia rasilimali zao hivi nani ataweza kumsaidia mnyonge kuweza kupaza sauti yake na ikasikika kama ilivyo? Kwa hiyo redio, magazeti na hata runinga kwa sasa hazifanyi kazi ya kupaza sauti za wanyonge labda kidogo burudani na michezo ambayo hii pia inatumika kuipumbaza jamii na ndiyo kusema michezo na burudani katika magazeti redio na runinga haina faida kwa watu masikini bali ni sindano ya ngazi kwa yale yanayowasibu. Leo ushangilie Taifa Stars Imeingia makundi, wakati unashangilia ukateguka mguu, unakwenda Hospitalini unakosa matibabu! Hapa ndipo unaweza kuelewa michezo na burudani ni sindano ya ngazi.”
Msomaji wangu kidogo nafuu ni mitando ya kijamii isiyo rasmi peke yake:
“Mathalani pitia na utazame ukurasa ule facebook wa Baba Askofu Emmaus Bandakile Mwamakula namna unavyofanya kazi nzuri. Hana ubaguzi kila atakalo julishwa litapachikwa na kwa wakati. Huku akipaza sauti za wanyonge. Kwa hiyo ni heri uwe na namba ya simu ya Baba Askofu Mwamakula ili ukiwa shidani mtumie ujumbe sauti yako itasikika kuliko kuwa na namba ya simu chombo chochote cha habari. Kipimo cha haya angalia mfano mdogo sana juu ya watu waliotekwa na hata kuuwawa ni chombo gani cha habari iwe redio, runinga au magazeti kinaendelea kuwazungumzia ndugu hawa bila ya kuchoka? Hakuna hata kimoja lakini mfariji ni Mitandao ya Kijamii peke yake hawa hawa akina Baba Askofu Emmaus Bandakile Mwamakula na wachache wenye mapenzi mema huku Dkt Jabiri Bakari akiendeleza uhodari wake wa Kukata Swichi.”
Mwanakwetu Upo?Kumbuka:
“Simu ya Baba Askofu Mwamakula?”
Nakutakia siku njema.
0717649257






Post a Comment