
Adeladius Makwega MBAGALA
“Naomba sana mheshimiwa spika tuachane na mambo ya uchama, tuache mambo ya uchama. Jiulizeni hapa Bungeni. Tujiulize hapa Bunge walikuwepo wangapi? Tujiulize walikuwepo wangapi na sasa hivi wapo wapi? Sasa hivi wapo wapi? Leo tunasimama hapa Bungeni, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wewe siyo Mbunge wa CCM! Kazi yako wewe ni Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kazi yako kuisimamia Serikali. Serikali ikisema baya mmm… ikisema nzuri mmm... Wabunge mmekuwa kama mbumbumbu… Ukimuuliza Mbunge unanjaaa mmmm…! Umeshiba mmmm... Mbunge hata unachokisimamia haukijui?
Amani haipatikani bila haki, amani haipatikani bila haki. Hapa tunasema serikali haisikii na ndiyo maana watu wanakimbilia nje ya nchi hata huko Marekani, Mtu akienda nje ya nchi mnasema msaliti, mimi niliwaambieni huku Waisilamu wamepigwa risasi na hata Wakristo wamepigiwa risasi. Jamani lazima tuisimamie amani ya nchi yetu, lazima tusimamie usalama wa nchi yetu…”
Haya ni maelezo ya mheshimiwa Seleiman Bwege ambaye wakati huo akiwa Mbunge wa Kilwa Kusini akiwananga wabunge wenzake, namna walivyo katika hoja za maslahi ya umma wa Watanzania, wakati huo mheshimwa Bwege alikuwa mbunge kupitia chama cha ACT Wazalendo.
Kwa nini Mwanakwetu amekumbuka na kuyanukuu maelezo haya ya mheshimwa Seleiman Bwege?
Hivi karibu mheshimiwa Bwege amekikicha chama cha ACT Wazalendo na kuhamia CHADEMA ambapo maamuzi haya yalitanguliwa na kauli kadhaa za mheshimiwa Bwege dhidi ya msimamo wake katika masuala ya kitaifa na isitoshe mheshimwa Bwege ameonesha kitendo cha kiungwana kwenda mahakamani huku akibebwa na wheel chair yake wakati shauri la uhaini dhidi ya Tundu Lissu likiendelea katika kuta za Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kitendo hiki kwa wale Wakristo naomba niwakumbushe Injili ya Mathayo 25:36 inasema haya:
“…nilikuwa uchi mkanivisha nguo, nilikuwa mgonjwa mkanitunza, nami nilikuwa kifungoni mkaja kunitembelea…”
Wangapi wenye miili kamili, wazima wenye afya wamefanya hivyo?Je mimi na wewe tunajifunza nini katika kitendo hiki cha mheshimwa Seleiman Bwege?
Swali ambalo Mwanakwetu anatakia kulijibu je maamuzi haya ya mheshimwa Bwege ya kuhamia CHADEMA ni maamuzi sahihi?
Mwanakwetu bila ya kutafuna maneno anaona kuwa maamuzi haya ya mheshimiwa Bwege ni maamuzi sahihi kulingana na upepo wa siasa za Tanzania kwa sasa, japokuwa ACT Wazalendo kina wabunge na madiwani na kimeshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2025 lakini upepo unaovuma kwa kasi kwa vyama vya upinzani nchini Tanzania ni wa CHADEMA.
Mwanakwetu kwa kumtazama Zitto Kabwe ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ACT na mtu mwenye ushawishi katika chama hiki, Mwanakwetu anaubeba moyo wa mashaka unasafiri na makala haya akitilia mashaka uthabiti wa ACT Wazalendo kufanya vizuri siasa za upinzani na hata kuaminiwa na Watanzania wengi.
Hapa msomaji wangu unaweza kurejea mgogoro Zitto Kabwe ndani ya CHADEMA hadi kuvuliwa nyadhifa na kufurusha katika chama hiki tangu mwaka wa 2013, 2014 na hadi 2015 huku ndugu Zitto Kabwe alibaki Bungeni na kupata stahiki zote kama Mbunge wakati Bunge linavunjwa.
Katika ili pia msomaji wangu unaweza kupata picha ya watu wa karibu wa Zitto Kabwe miongoni mwao ni huyu aliyekuwa mkufunzi wa vyuo kadhaa Kitila Mkumbo japokuwa alikuwa ACT baadaye akahamia CCM na kupachika nyadhifa kadhaa.
Msomaji wangu naomba leo nisikuchoshe sana juu ya ACT Wazalendo ya Tanzania Bara.
Kwa kumalizia makala haya na ili niutue moyo wangu wa mashaka pahala salama naomba kwa hisani yako msomaji wangu nikusimulie kisa hiki cha kweli kabisa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa mwanachama wa ACT Wazalendo aliyeshiriki katika Uchaguzi Mkuu:
“Kijana mmoja mtoto wa marehemu Profesa Juma Mikidadi Omari Mtupa ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa CCM katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka mkoa wa Pwani nadhani Kibiti- kijana huyu alichukua fomu ya udiwani na kufanya kampeni vizuri.
Naomba nirudi nyuma kidogo …wakati Profesa Juma Mikidadi yu hai Mwanakwetu alipata bahati ya kumfahamu kupitia Ustadh Mpembenue (mdogo wa ustadhihuyu alikuwa Mkuu wa Wilaya Ilala enzi ya Jakaya Kikwete), Ustadh Mpembenue alikuwa mwalimu wa madrasat moja pale Mtoni Relini, jirani na Msikiti Wa Maboksi (Mtoni Sokoni) hapa jirani na msikiti huu Binti Makwega alikuwa biashara zake ambapo Mwanakwetu alikuwa anashinda sana baada ya kumaliza kidato cha sita. Jirani na hii madrasat kulikuwa na dada wa Profesa Juma Mikidadi ambaye alikuwa mama mmoja fukara sana lakini Profesa mara nyingi akitoka Bungeni alikuwa anapita kumsalimu huyu dada yake ambaye alikuwa ameolewa na mtu fukara sana. Jirani na nyumba moja iliyokuwa wamepanga Wazanzibari wengi waliyokuwa wanafanya biashara ya mchele kutoka Shinyanga jirani na Mtoni Sokoni.
Profesa Mikidadi kila alipofika alikuwa anamsalimu dada yake kisha anakwenda ile madrasat kwa Ustadh Mpembenue anamsalimu anamuachia pesa kidogo kisha anarudi kwa dada yake, Profesa Mikidadi akifika pale alipokaa Mwanakwetu wakiwa na ustadh Mpembenue walimtania Mwanakwetu n-huyu jamaa ni Mkristo lakini ni mtu nzuri, tukiwa na shida zetu ndogo ndogo dukani madrasat yetu anatusaidia (Profesa anasema hata dada yangu ameniambia) Jamaa wakawa wanamtania Mwanakwetu wakisema shida ya huyu jamaa ni hodari sana kwa kula nyama ya nguruwe-Jumapili lazima aende Temeke mwisho na hata Mzee Maembe (Baba wa Vitali Maembe akichinga nguruwe ) huyu jamaa ananunua kilo nyingi. Hapa Profesa Juma Mikidadi anacheka kisha Profesa anapita zake na kuondoka.”
Mtaani wakati wa kucheza drafti watu wanasema huyu mama kwanini Profesa hamsaidii? Watu wanajibizana kijiweni kuwa kumsaidia ndugu yake Profesa anafanya na ndiyo Profesa anapita kumsalimu dada yake kila mara akitoka Bungeni.
Msomaji wangu sasa nakuomba turudi kwa huyu mtoto wa Profesa Juma Mikidadi ambaye amesomea ualimu kama marehemu baba yake na mwaka 2025 kagombea udiwani wa kata siyo kwao Kibiti bali pale Morogoro. Kwa wale mnaokumbuka Profesa Juma Mikidadi aliwahi kuishi Morogoro wakati akiwa hai. Kijana huyu anaishi Morogoro,
Kijana huyu akamwambia Mwanakwetu kuwa anagombea udiwani hii ni septemba ya mwaka wa 2025 Mwanakwetu akauliza kwa chama gani? Kijana akajibu ACT Wazalendo, Mwanakwetu akamwambia huyu kijana maneno haya:
“Kwa umri wangu nilionao leo nikisikia mtu ninaheshimiana naye anahamia ACT Wazalendo kwa Tanzania Bara ninamwambia ukweli kuwa ACT mimi sikiamini kabisa…”
Msomaji wangu ili kuweka kumbukumbu sahihi kijana huyu anaitwa JAMALI, nikamwambia maneno haya wakati Zitto anatoka CHADEMA mimi nilikuwa mtumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania, Zitto Kabwe ni Mtanzania mwenzetu, wakati ule japokuwa CHADEMA walimfurusha lakini Zitto Kabwe alibaki bungeni, kile kitendo cha kubaki Bungeni hadi Bunge linavunjwa kilinipa mashaka kwake mia kwa mia, hasa juu uthabiti wake katika siasa za upinzani.
JAMALI aligombea udiwani na siku ya uchaguzi alikutana vitu vya ajabu na hata kushuhudia mwalimu wake aliyemsomesha akivifanya vituko hivyo. Mwanakwetu nilitayarisha makala baadaye huku kukatokea mabishano ya maneno baina ya JAMALI na Msimamizi wa uchaguzi. Siku chache baada ya uchaguzi akawekwa korokoroni karibu siku 30. Katika simu akawa hapatikani kwa kuwa ni kijana anayetafuta maisha Mwanakwetu akajua kuwa JAMALI anahangaika tu na maisha pengine yupo salama. Baada ya mwezi JAMALI akatoka korokoroni akampigia simu Mwanakwetu na kueleza kilichomkuta.
Mwanakwetu niliudhunika sana kisha kumuuliza swali moja tu JAMALI, chama chako cha ACT WAZALENDO walifuatilia suala lako?
Jamali alijibu:
“Kaka Makwega wapi? ACT hawakufanya hivyo. Hapa alihangaika mama tu nenda nenda rudi nenda rudi hata hii simu ninayoitumia leo hii ni ya mama.”
Mwanakwetu nilimpa pole huyu kijana mwenye shahada ya ualimu na mtoto wa Profesa Juma Mikidadi.
“Ndiyo maana Mwanakwetu anakuwa mkali hata kwa CCM haiwezekani Humphrey Polepole mwanaCCM mwenzetu, kawa kiongozi serikalini, kawa kiongozi ngazi ya juu CCM katekwa kisha CCM kimya. Hivi tunatambua maana ya chama? Chama ni mimi wewe na yule, kukiwa na heri tuwe pamoja na kukiwa na shari tuwe pamoja. Chama Cha Mapinduzi kinakuwa chama kwa sababu wazazi wanaruhusu watoto wao wafanye siasa ndani ya CCM, kinyume chake kama hali ni ya hatari hivyo nani atakayekubali kuwepo sehemu isiyo salama?”
Kwa hiyo Mwanakwetu anasema maamuzi ya mheshimwa Seleiman Bwege kwenda CHADEMA yapo sahihi, tazama namna CHADEMA inavyofuatilia kesi ya Tundu Lissu mahakamani, lazima chama cha siasa kiwe jirani na familia ya mpendwa wao, jirani na mpendwa wao katika shida yoyote ile anapokuwa na tatizo hadi mwisho mnakuwa naye, jamii ya Watanzania siyo wajinga ni watu wanaotambua kila kitu, wanaona na kujifunza mengi.
“Hakuna chama cha siasa kinachozaa binadamu, bali wote wanaofanya siasa ni watoto wa watu, wanatoka katika viuno vya wanaume na matumbo ya wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lazima tuwe makini.”
Kwa hakika Seleiman Bwege amefanya maamuzi sahihi.
Mwanakwetu kwa Makala haya pia ameukumbuka wimbo huu wa UJAMAA.
“Nitakwenda na Jembe Langu , Kutangaza UJAMAA Tanzania Kote, NItakwneda na Jembe langu ,Kutangaza UJAMAA Tanzania Kote. Hata Kibiti Nitakwenda -Tanzania Kote,
Hata Ulanga Nitakwneda –Tanzania Kote
Hata Iringa Nitakwenda –Tanzania Kote
Hat Songea Nitakwned Tanzania Kote .
Hata Mbagala Nitakwenda Tanzania Kote.
Nitakwenda na Jembe Langu , Kutangaza UJAMAA Tanzania Kote, NItakwenda na Jembe langu ,Kutangaza UJAMAA Tanzania Kote.”
Mwanakwetu Upo?Kumbuka:
“Seleiman Bwege Kwenda CHADEMA Amefanya Maamuzi Sahihi.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257





Post a Comment