Pete ya Harusi Ikivaliwa Kidoleni Hairudi Kwa Sonara

 






Adeladius Makwega-MBAGALA

“Unawezaje kuuza pete ya harusi wakati wewe bado upo katika ndoa? Pete ya harusi haiwezi kuondolewa katika kidole pete hadi pawe na makubaliano ya wenza hao katika ndoa kama ni talaka au kifo. Siyo unakurupuka unakwenda kwa sonara hoo mimi nauza pete yangu harusi.

Ukienda kwa sonara kwa kuwa yeye anauza na kununua dhahabu ataipima uzito wake, kisha atakupa pesa hiyo huku bei ikiwa ya chini.

Inawezekana unauza pete yako ya ndoa kisa hali yako ya uchumi mbaya, hili ni sawa lakini sasa katika maisha ya ndoa hali ya uchumi itakuwa mbaya mara ngapi?

Kwa hiyo hali ya uchumi ikiwa mbaya maana yake mwendo ni kuuza pete ya harusi? Mambo yakiwa magumu maana yake ndoa yako imeingia rehani?Lazima kupambana na hali hiyo kutafuta vyanzo vingine na lazima ujiulize kwani hali inafikia huko?”

Haya maneno yanaongelewa na jamaa wanaokunywa chai mkahawani mbele ya Mwanakwetu na huku Mwanakwetu ndiyo anaingia waliopo ndugu hawa,hapa mjadala mkubwa , mjadala makini unaendelea:

“Unajua nyinyi sikilizeni, taifa la Marekani linashikilia rekodi ya akiba rasmi ya dhahabu iliyo kubwa zaidi duniani kwa tofauti kubwa, ikiwa na tani 8,133.5 zinazohifadhiwa hasa katika maeneo kama Fort Knox na Hifadhi ya Shirikisho ya New York (NY Federal Reserve). Kiasi hiki kinawakilisha takribani 17% ya jumla ya dhahabu duniani na kimebaki kuwa hivyo kwa muda mrefu maana yake hakijabadilika kwa miongo kadhaa.Wakati Ujerumani, Italia, Ufaransa, Urusi, na China hufuata, kila moja ikiwa na zaidi ya tani 2,000. Unajua hii dhahabu inaendelea kuwa mali kuu ya hifadhi salama katika akiba za benki kuu.”

Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu nayeye yu mkahawani akaagiza chai na chapati moja, mhudumu akaenda kumchukulia na kumpatia huku akiendelea kunywa chai hii ya rangi.

 

Hawa jamaa aliowakuta wakawa wanaendelea na soga zao

“Dhahabu haipo kwa ajili ya kutumiwa kununua vitu madukani. Ni mali ya akiba, kama akiba ya dharura kwa siku za shida. Benki kuu hushikilia akiba ili ziweze kulinda sarafu zao, kulipia uagizaji wa bidhaa wakati wa dharura, au kuwapa uhakika wakopeshaji. Akiba nyingi huwa katika sarafu za kigeni na hati fungani za serikali, lakini hizo hutegemea ahadi za nchi nyingine. Dhahabu ni mojawapo ya mali chache zisizo na mhusika wa pili (haiwezi kushindwa kulipa) na huwa inahifadhi thamani yake wakati wa migogoro, hivyo husaidia kugawanya hatari katika akiba.

Pia ni rahisi kuuzwa na kusafirishwa. Benki Kuu ya taifa lolote inaweza kuuza dhahabu, kuitumia kama dhamana, au kufanya ubadilishanaji wa dhahabu ili kupata fedha za kigeni haraka. Kwa kuwa uzalishaji wake huongezeka polepole na inaaminika duniani kote, kuwa nayo hutuma ujumbe wa uthabiti kwa masoko na kwa wananchi. Akiba kubwa ya dhahabu ya leo kwa kiasi kikubwa ni mabaki ya kihistoria kutoka nyakati ambazo fedha zilikuwa zimefungamanishwa na dhahabu. Mara baada ya kuwa nayo, hakuna sababu kubwa ya kuitumia yote mara moja, na baadhi ya nchi hata zinaongeza akiba yao ili kujikinga dhidi ya vikwazo, hatari za kisiasa, na changamoto za majanga.”

Hawa jamaa mabao walionekana ni wasomi wakasimama na kuondoka zao, kisha Mwanakwetu kubaki mwenyewe pale mkahawani akanywa chai yake na alipomaliza akarudi alipotoka ndipo akaamua kuyaandika makala haya kama yalivyo unayoyasoma msomaji wangu.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu alibaini kuwa kumbe wale ndugu walipokuwa wanazungumzia juu ya kuuzwa kwa pete ya hurusi walikuwa wakilinganisha na suala la kuuzwa kwa hifadhi ya dhahab.

Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu naomba nisema maneno haya : Mwanakwetu amesoma Shahada ya Uzamili ya Uongozi wa Biashara (MBA) miaka karibu 18 iliyopita kwa mwaka 2026 na baadahi ya maprofesa waliomsomesha ni Profesa Mwafwenga(Marehemu) na Profesa Ngowi(Marehemu). Kati ya hawa wasomi wawili Profesa aliyenifundisha vizuri sana na kwa umahiri mkubwa ni marehemu Profesa Honest Ngowi huku maksi alikuwa akitoa kwa haki.

Sasa msomaji wangu naomba umuelewe Mwanakwetu jambo ili analotoka kulisema kama alivyofundisha na Profesa Ngowi:

“Wakati nchi inapouza akiba yake ya dhahabu, kwa kawaida huwa inabadilisha mali ya muda mrefu na mali iliyo thabiti kuwa fedha taslimu za haraka hasa sarafu za kigeni shabaha kushughulikia shinikizo la kifedha, kufadhili miundombinu, kuimarisha sarafu, kukamilisha miradi inayohitaji fedha nyingi.

Kitendo hiki pia kinaweza kuashiria matatizo ya kifedha kwa taifa husika, kupunguzwa kwa misaada au dhahabu hiyo inauzwa kutoka na bei ya dhahabu kupanda sana ulimwenguni ili mchukue ile faida.”

 

Katika hili hoja kadhaa zinaweza kutolewa wakati taifa fulani linauza akiba yake ya dhahabu hoja moja ambayo huwa si ya kweli kuwa bei ya dhahabu imepanda. Hii hoja si ya kweli maana bei ya dhahabu kwa miaka huwa haipandi sana, inapanda kidogo kidogo na ndiyo maana madini haya yanayohifadhiwa katika akiba ya mataifa mengi- rejea ili aslimia 17 ya akiba ya dhahabu yote ulimwenguni ni ya Marekani ambalo ni tiafa imara katika uchumi wake.

“…nchi inapouza akiba yake ya dhahabu, kwa kawaida huwa inabadilisha mali ya muda mrefu na mali iliyo  thabiti kuwa fedha taslimu za haraka (sarafu za kigeni) ili kushughulikia shinikizo la kifedha, kufadhili miundombinu, kuimarisha sarafu, kukamilisha miradi .

Kitendo hiki pia kinaweza kuashiria matatizo ya kifedha na uchumi…”

Haya ndiyo niliamu kuyasema katika makala haya siku ya leo kwa heshima ya mwalimu wangu Profesa Ngowi ambaye sasa amelala kaburini. Pete ya harusi ni ishara ya ndoa ni dhamana ya ndoa, ni uimara wa ndoa hauwezi kuipeleka sokoni maana pete ya Harusi ikashakaa kidoleni Hairudi kwa Sonara.

Mwanakwetu Upo? Je Makala haya yaitwaje?Mwanafunzi wa Profesa Ngowi au Pete ya Harusi Ikikaa Kidoleni Hairudi kwa Sonara. Vichwa vyote kavipenda wewe msomaji wangu chagua kimoja lakini kumbuka Pete ya Harusi Ikivaliwa Kidoleni Hairudi kwa Sonara.

Nakutakia Siku Njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments