Njaa Mali na Mamlaka Vyote hivi ni vya Duniani Tu

 


Adeladius Makwega-MBAGALA

Siku ya Jumapili ya Februari 22, 2026 ilianza kwa Mji wa Musoma mkoani Mara nchini Tanzania Mvua kubwa kunyesha, ardhi ilikuwa imeloana mno, huku Mwanakwetu hakufahamu aina ya mvua hii kama ni ya masika au vuli.

Hata Mwanakwetu alipoamka alipoitazama kamba yake ya kuanikia nguo, alizoanika siku iliyotangulia nguo zote zilikuwa mbichi kana kwamba zimefulia muda mfupi. Mvua ilisababisha Mwanakwetu alishindwe kuwahi kusali Misa ya Kwanza ya saa 12.30 ya asubuhi kwa kuwa hakuwa na mwamvuli ndani kwake, hivyo basi akakata shauri asali ibada ya misa ya pili.

Wakati akisubiri mvua kupungua alitazama utabiri wa hali ya hewa huku ukibainisha kuwa Mji wa Musoma joto ni sentigredi 22, unyevunyevu ni wa asilimia 70, ujirani na mvua ni wa asilimia 78 na upepo ukivuma kwa KM 6 kwa saa. Hapa Mwanakwetu akabaini kuwa kama asilimia za unyevunyevu na zile za ujirani na mvua zikiwa ni kubwa kuelekea asilimia 100 mvua huwa inanyesha.

 

Mwanakwetu alifunga safari kuelekea Kanisa la Mtakatifu Agustino Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma ibada ya pili ambapo alipofika Kanisani misa hii ilikuwa inaongoza na Padri Julius Ogolla huku akiwaambia waamini wake kuwa misa hii ni Jumapili ya kwanza Kwaresma huku majina waamini marehemu walioniuwa kuombewa katika ibada hii yakitaja likiwamo jina la Polycarp Kadinali Pengo.

 

Wakati wa mahubiri ulifika huku Padri Ogolla alitumia dakika 36 kuyajenga mahubiri ya dominika hii ambapo kwanza aligusia juu mwanamke namna alivyodangaywa na nyoka hadi kulila tunda la mti wa katikati.

“Dhambi ipo tangu Adamu na Eva lakini sheria haiwezi kutusaidia kupambana na dhambi maana dhambi ilianza kabla ya sheria, Mungu alipomuumba binadamu Bustani ya Edeni alimpa jukumu la kuwapa majina wanyama wote, baadaye alimuona Adamu ya pweke akamletea mwanamke, mwanamke alipofika pale bustanini akaleta balaa. Wewe mwanamke umemkuta Adamu anaishi vizuri na wanyama wake wewe unafika unaleta mafarakano, badala ya kutengeneza mahusiano mema, wewe unashirikiana na nyoka. Swali la kujiuliza nyoka kwanini hakumuendea Adamu ili amuadae? Nyoka alijua mwanamke anaingilika. Awali Mungu alipomuumba Adamu alimwambia waweza kula matunda yote hapa bustanini ila usiguse usichume na wala usile tunda la mti wa katikati na hata alipokuja Eva aliambiwa juu ya katazo ili. Wakati Adamu anamwambia Eva katazo ili Nyoka alisikia ndipo Nyoka akamfuata Eva na akisema Eva ukila tunda ili haufi bali utafanana na Mungu. Eva hakujua kuwa awali Mungu wakati anamuumba Mwanadamu alimuumba kwa mfano wa Mungu Mwenyewe. Eva aligusa, alichuma na kulila tunda hilo na kisha akachuma na kumpa Adamu.

Kishawishi hiki cha Eva kipo hadi leo hii, wanawake bado wanapokea vishawishi hivi. Inawezekana hawapokei kutoka kwa nyoka lakini wanapokea kutoka kwa WASHAWISHI, Vishawishi vya leo kwa wanawake ni vingi miongoni mwao ni NJAA mama akiwa na njaa anaweza kufanya jambo lolote lile.

Kishawishi wa pili ni MALI, mwanamke anaweza fanya lolote ili kupata mali. Kishawishi cha tatu ni MAMLAKA. Mathalani …mama akisikia mume wake anatembea na mwanamke mwingine ni balaa anaweza kufanya lolote kwa kuwa huyu mwanamke mwingine ameingilia utawala wake, ameingilia himaya yake. Dunia ya leo ina visa vingi hasa mauwaji mengi yanafanyika leo kisa NJAA, MALI na MAMLAKA , hapa Mkoa wa Mara tuna madini mengi watu wangapi wanauwawa kisa watu wapate madini? Mnasikia sasa kila pahala hapa Mara machimbo ya madini yanafumuka, huko wanauwawa watu wangapi?

NJAA, MALI na MAMLAKA yanawasumbua sana wanawake yanamsumbua sana mwanadamu.”

Padri Julius Agolla aliwaambia waamini wake kuwa katika maisha ya mwanadamu vishawishi vipo vingi, huu wakati wa Kwaresma tujihadi kuvishinda vishawishi hivyo akiwaomba waamini wake wafunge na wasiwe na visingizio vya hapa na pale maana iwe NJAA, iwe MALI na hata MAMLAKA haya yote ni duniani tu. Mahubiri haya yalimalizika na misa kusaliwa hadi mwisho huku hali ya hewa ya unyevunyevu ikiupamba Mji wa Musoma.

Mwanakwetu alipofika Kwake alimsikiliza pia Luis Kadinali Tagle ambaye ni Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki inayojihuisisha na Uinjilishaji wa Watu Ulimwenguni nayeye aliyasema haya:

“Tumeingia katika kipindi kitakatifu cha Kwaresima. Katika Jumapili yake ya kwanza, tunaalikwa kutafakari juu ya majaribu ambayo Yesu alikabiliana nayo. Baada ya ubatizo wa Yesu, Roho alimwongoza jangwani ambako aliomba na kufunga kwa siku 40. Huko, shetani alimjaribu athibitishe kuwa yeye ni Mwana wa Mungu kwa kushibisha njaa yake na kwa kujaribu uaminifu wa Mungu kwa ahadi yake. Shetani alimpa mali zote za dunia, nguvu, na falme, ikiwa Yesu angemwabudu yeye. Ndugu zangu, tunafahamu simulizi hii ya Injili. Jaribu ni mwaliko wa kuyaenga maisha yetu juu ya nafsi zetu wenyewe. Yesu alipambana na majaribu kwa kujikita katika Neno la Mungu. Hivyo, Yesu alibaki na ujasiri na akamshinda shetani. Lakini je, tunafuata njia ya Yesu? Tunapokabili majaribu kila siku, na tujijenge juu ya Neno la Mungu. Tuitikie kama Bwana alivyofanya: Ondoka, Shetani. Neno la Mungu huleta uzima. Mungu ni mwaminifu na hakuna Mungu mwingine ila Yeye. Ee Mungu, utujalie neema ya kutegemea Neno lako katika nyakati za majaribu. Kwa maana wewe ni mwaminifu na wewe peke yako ndiwe Mungu. Amina.”

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Njaa, Mali na Mamlaka vyote ni vya Duniani tu.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments