Mwenyenzi Mungu Atunusuru na Unafiki wa Hii Dunia-Hakuna Kitu Pale

Adeladius Makwega-MBAGALA

“Tulipokuwa wadogo nyumbani kwetu Mbagala kulikuwa na Baa moja maarufu mno wakati huo ikifahamika kama KWETU BAA. Hii Baa ilikuwa pale Mbagala Kipati kama unaingia njia ya kwenda Mbagala kwa Mangaya, yaani ukitoka nyumba iliyokuwa Mashine ya Kusaga Unga ya KIPATI, unavuka Barabara ya Mangaya sasa pana mzunguko, kisha unakutana na nyumba ALLY NISI yule chotara mwenye asili ya MAFIA alafu nyumba iliyofuata ilikuwa na Selemala na kisha iliyofuata ilikuwa ndiyo KWETU BAA.

Hii ilikuwa Baa maarufu sana Mbagala enzi hizo, unaweza kulinganishwa na EQUTA GRILL kwa wakati huo. Hapa KWETU BAA siku ya Jumamosi, Jumapili na Sikukuu hasa mchana hadi jioni kulikuwa na vikundi kadhaa vya ngoma, Disco Toto , sarakasi, vichekesho na maigizo vikifanya maonesho haya-Kwa wakati ule vikundi kama vile Muungano Culture Troupe na hata DDC Kibisa Ngoma Troupe iliyokuwa mali ya Jiji la Dar es Salaam walikuwa wakifanya maonesha haya wakipeana zamu. Hata wasanii kama Hadija Kopa Nasma Khamis, Dkt. Remmy Ongala wa Super Matimila na Afriso Ngoma walifanya maonesho yao hapa na ikishafika saa moja usiku michezo ya sanaa inawekwa kando watoto waliofika wanatolewa nje, kisha muziki kamili iwe dansi au taarabu mambo yanapamba moto.

Haya maonesho yote hayakuwa bure bali yalikuwa na kiingilio ambapo zipo familia ambazo zilikuwa na kipato huku watoto wao walipewa pesa za kiingilio waende kuona michezo kadhaa ikiwamo kucheza na nyoka, mashindano ya disko na kumbuka enzi zile kulikuwa na NYOKA wa KIBISA- Yaani Nyoka wa DDC Kibisa Ngoma ambao walikuwa wakichezeshwa kama wanavyofanya Wasukuma.

Katika harakati hizo Mwanakwetu sikubahatika hata mara moja kupewa pesa nyumbani nikaangalie haya maonesho , kwa haki ya Mungu sikumbuki hata mara moja lakini mara zote Mwanakwetu nilikuwa nje ya ukumbi huo wenzangu waliopewa pesa na wazazi wao wakiwa ndani na muda wa kutoka wananikuta nje kisha tunarudi nyumbani pamoja mwili mzima umetapakaa vumbi. Wale waliokuwa ndani wanaanza kusimulia kilichokuwa kinatokea…‘Yaani yule jamaa hatari yaani yule jamaa anakimeza kichwa cha chatu mdomoni, yaani jamaa alikuwa anaumeza hadi moto…’ Mpaka tunafika nyumbani kila mmoja anajua kilichotokea, aliyeingia ndani na hata tuliyokuwa nje. Huku sie wa nje tulikuwa tunasikia sauti na kilichokuwa kinatokea. Maana wamezibwa kwa ukuta lakini sauti inasikika, inawezekana aliyeingia ndani akawa siyo msimuliaji mzuri lakini huyu aliyebaki nje akawa msimuliaji mzuri wa maonesho haya. Sote tunakipata kile kilichotokea .”

Kwanini Mwanakwetu ameikumbuka KWETU BAA ambayo ni baa maarufu ya zamani kwao Mbagala?

Vijana wawili walikuwa wanahitimu Chuo Kikuu wanaongea, binti akasema mimi nikimaliza chuo nitaingia katika siasa maana yule jamaa anatoka kijijini kwetu, lakini yeye na mimi ni dini moja , huyu jamaa ananivutia mno na misimamo yake ngoja nifuate nyao zake, nijaribu katika siasa. Kweli huyu msichana akaingia katika siasa na akaaminiwa kweli kweli huku akishiriki mikutano mikubwa mikubwa ya chama hiki. Akiwa katika siasa nyota yake ikang’aa mno huku mjadala wa binti huyu agombee jimbo au angoje vitu maalumu ulipamba moto.

“Binti huyu anapaswa kuzunguka nchi nzima ili aziongeze kura za Mgombea Urais asigombee ubunge wa jimbo.”

Viongozi wanaongea.



Binti huyu mwenye weusi wa asili, jina lake linawika mno kila kona jina lake linatajwa, jina lake linawaka mithili ya nyota ya jaa huku akiwa na jina linalofanana na jina la mke mmojawapo wa mtume wa dini ya Kiisilamu(Mtume Mohammed). Dada huyu akitoka katika familia masikini sana, mama mpika vitafunio baba fundi nguo. Mwaka wa uchaguzi ukafika kumbuka binti huyu yupo chama cha upinzani watu wanajipanga namna ya kushirki uchaguzi.

Wakubwa wa chama hiki wakapiga mahesabu kukawa na makubaliano fulani ya siri baina ya chama tawala kuwa kitawapa msaada wa fedha ili angalau chama pinzani wawe na wagombea. Chama tawala wakasema pesa ipo njooni mchukue, pesa ni keshi hatuwezi kuituma katika akaunti yoyote ili linaweza kuleta maneno.

Jamaa wa chama pinzani wakapiga mahesabu sasa tumekaribia uchaguzi tukisema tunakwenda pale makao makuu ya chama tawala iwe mchana au usiku watu watatuona ili litaleta shida, tuchague wanachama wetu wasiofahamika waende na kiongozi mmoja ambaye siyo maarufu wakachukue mzigo huo, sisi maarufu tubaki ofisini wakija tutapokea mzigo. Kweli jamaa walifanya hivyo miongoni mwa walioteuliwa kwenda kuchukua pesa hizo alikuwepo binti aliyemaliza chuo kikuu ambaye nyota yake inang’aa, wakafika makao makuu ya chama tawala wakapewa masanduku ya fedha, wakamshukuru aliyekabidhi ambaye alikuma Msaidizi wa Mwenyekiti kisha kurudi kwa viongozi wao wa chama pinzani na mzigo kufika salama kama ulivyo.

“Yule kiongozi wa chama pinzani akawashukuru mno kwa kazi hii kukamilika bila kushitukiwa, kisha wale walioshiriki zoezi wakapewa pesa na wakasema uchaguzi ukiisha salama wote watapewa nafasi.”

Baada ya kazi hii kufanyika vizuri yule binti aliyemaliza chuo kikuu dhamiri ikawa inamshitaki, akawa anajiuliza:

“Hivi huku mimi naongea kama mpinzani, juzi juzi nimetumwa kwenda kuchukua fedha kwa chama tawala hivi mimi nina akili kweli?Mimi nitakuwa Muisilamu wa namna gani siku kiyama cha wafu nitajibu nini mbele ya Mungu?”

Yule binti akamfuata baba yake mzazi yule mzee fukara sana ambaye ni fundi mshona nguo akampa robo tatu ya pesa yote aliyoipokea baada ya kukamlisha kazi ile ya chama pinzani na robo ya pesa akampa mama yake mpikaji vitafunwa, kisha huyu binti akasema jamani hizo pesa ongezeni mtaji wetu, binti hakubaki hata na senti moja.

Kisha binti huyu akasema maneno haya kwa wazazi wake:

“Baba mimi siendi tena kwenye siasa, maana kule kinachofanyika ni batili hakuna haki hata kidogo, nitabaki nyumbani huku nikitafuta kazi.”

Wazazi wake hawakuamini kilichosemwa lakini walikuwa wakidhani binti huyu alikuwa anasumbuliwa na wanaume huko katika siasa kumbe kilichomtoa siyo hicho.

Kweli binti yule wa Kiisilamu akakacha siasa huku chama pinzani kiliendelea kumtafuta hadi kufika nyumbani kwao lakini wapi alikuwa anajificha na simu akabadilisha huku alikuwa akivaa baibui mwanzo mwisho akificha sura yake. Mungu bahati baadae serikali ilitangaza kazi binti huyu aliomba kwa kuwa alikuwa na sifa na uwezo mzuri kuongea na Kiswahili na Kiingereza binti huyu aliajiriwa serikalini. Binti wa watu akiwa serikalini, sasa akiwa kazini ofisini runinga inamrusha mwanasiasa yule chama pinzani, Binti huyu alisema maneno haya:

“Mwenyeezi Mungu atunusuru na unafika wa hii dunia pale hamna kitu.”

Maneno haya yakisemwa huku akisondwa kidole mwanasiasa yule katika runinga.

Watu pale ofisini wakashangaa mbona huyu jamaa anaaminika sana, hapa hapa ndipo akasimulia kisa chote tangu anahitimu chuo kikuu hadi anaikacha siasa ya upinzani na hadi anapata ajira serikalini.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Msomaji wangu kumbuka watoto wa Mbagala walivyokuwa wanakwenda kuangalia maonesho ya DDC Kibisa Ngoma pale KWETU BAA Mbagala , kumbuka wapo walioingia ndani na wapo waliobaki nje akina Mwanakwetu, lakini aliyeingia ndani na aliyebaki nje wakitoka wanaungana na kusimuliana mambo yalivyokuwa mle ndani maana hawa watoto wanatoka mtaa mmoja/kijiji kimoja hata kama wengine ni mafukara hawakuwa na pesa za kiingilio wale waliongia ndani waliingia kwa niaba ya jamii nzima lazima wasimuliane kilichotokea, yale ya ndani na ya nje yanaunganishwa.Kwa hakika ukumbi wa KWETU BAA ulikuwa na ukuta wa tofali za saruji lakini ukuta sarufi hauwezi kuficha sauti kupita juu angani na hauwezi kuzuia vijana hawa kusimuliana yaliyotokea baada ya maonesho. Katika makala haya kiongozi wa chama pinzani yeye alihofia kwenda yeye mwenyewe kuchukua lile sanduku la fedha, akiamini wale waliotumwa hata akiwaamini wale waliompa pesa, akidhani atabaki kuwa salama, hilo hapana.

Mwanakwetu Upo? Kumbuka:

“Mwenyeezi Mungu Atunusuru na Unafiki wa Hii Dunia Pale Hamna Kitu.”

Makala haya ni maarufu kwa rafiki wa Mwanakwetu Bruce Amani ambaye ni mtangazaji wa DW KISWAHILI mwenye asili ya Kenya.

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 


0/Post a Comment/Comments