Adeladius Makwega MBAGALA.
Haya yalikuwa majira ya asubuhi ya Februari 27, 2026 , Mkuu wa Mkoa wa Mara nchini Tanzania, Kanali Evans Alfred Mtambi anafika Wilayani Tarime akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, hapa kwanza wanaingia na kufanya kikao cha ndani, huku hali ya hewa ya Mji wa Tarime ikiwa ya nyuzi joto 24, unyevunyevu ni wa asilimia 60, ujirani na mvua ni kwa asilimia 92 na upepo ukivuma kwa KM 3 kwa saa.
Kikao hiki cha ndani kilijumuisha kamati mbili za usalama ile ya Mkoa na ya Wilaya ya Tarime ambapo kilidumu kwa dakika 45 , kisha kumalizika na Mkuu wa Mkoa wa Mara aanze ziara yake wilayani humo.
Mwanakwetu alikuwa mwanahabari peke yake muda huo, hivyo basi alisogelea gari nyeupe Toyota Land Cruzer akiwa kando na Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kisha kuomba kupanda gari hilo ambalo lilijulikana baadaye kuwa ni la Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mara.
“Wewe ingia tu, sisi sote tumekuja kwa ajili ya ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, ingia haraka tuanze ziara…”
Haya yalisemwa na kijana mmoja mweupe dereva wa gari hili la Kamanda TAKUKURU mkoa wa Mara. Jambo hili lilimvutia Mwanakwetu huku akisema moyoni kuwa TAKUKURU wametimiza jukumu lao la kusimamia utawala bora.
Kwa hakika ziara ilikuwa ndefu ambapo kwa sehemu kubwa Kanali Mtambi alitembelea na kukagua Mgodi wa Nyamongo hasa ndani ya mgodi ambapo kulikuwa na eneo lililoongezwa baada ya mpaka wa awali kulikuwa na wakazi kadhaa ambapo baadhi walihama baada ya kupokea malipo yao na wengine wamegoma kutokana na kupinga makisio yao ya malipo ambapo kesi kadhaa zilipelekwa mahakamani.
Kanali Mtambi hapa alisema haya:
“Jamani tunatambua nyinyi ni Watanzania wenzetu lakini uwekezaji huu katika Mgodi wa Nyamongo wapo Watanzania wenzetu na Serikali yetu ambapo fedha zinazopatika zinatumika kwa maendeleo yetu, hivyo basi ni vizuri kukwepa migogoro kama hii na hili nchi ipate maendeleo lazima tusiwekeane vikwazo. Naagiza Mwanasheria wa Mkoa wa Mara kuhakikisha mashauri haya yapekewe hati ya dharura ili yasikilizwe haraka , yaishe hili kazi hapa mgodini zifanyike.”
Kwa upande wa wananchi waliogomea malipo haya kwa tathmini zilizofanyika awali walisema kuwa ni kweli walisaini fomu kadhaa zenye tathmini hizo lakini malipo waliyopimiwa ni chini maana gharama ya ardhi katika eneo la Nyamongo ni kubwa sana na hili ndiyo chanzo cha migogoro yote hiyo.
Safari ilikuwa ndefu sana katika makazi haya ambayo wananchi waliogoma kutoka huku Mwanakwetu akiona watoto wadogo kadhaa wakiishi katika makazi haya duni na machafu na yalikuwa umbali mrefu na huduma za jamii maeneo hatarishi, huku watoto hawa hawakuwa na uwoga wowote hata kwa askari kadhaa wenye silaha nzito waliombatana na Mkuu wa Mkoa wa Mara siku hii.
Awali ziara hii ilianza katika Shule moja ya Sekondari ambayo ipo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime , hapa Mkuu wa Mkoa wa Mara aliingia katika ukumbi wa shule hii na kukutana watu wamejaa ukumbini na hapa alianza kikao kilichokuwa na ajenda ya utatuzi wa mgogoro wa mgawanyo mrahaba na asilimia moja ya mgao wa Kijiji cha Msege kilichogomea asilimia 40 ya fedha zake kutika Kijiji cha Genkuru karibu milioni 400 na ushehe ambapo Kijiji Msege walitaka pesa yao ihamishiwe katika akaunti yao na siyo kupelekwa katika miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru ndugu Elias Mwela aligomea utaratibu wa fedha hizo kuhamishiwa akaunti nyingine na hilo kuleta maneno tangu ngazi Kijiji na Kijiji , ndani ya Chama Cha Mapinduzi, Kata na Kijiji na Halmashauri ya Wilaya hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, hivyo basi Mkuu wa Mkoa Mara alienda kuutatua mgogoro huo Februari 27, 2026 baada ya hatua zote hizo zilizotajwa kugonga mwamba, mfupa huu alikabidhiwa Kanali Mtambi.
Tamati ya yote Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru alionekana yu sahihi na hivyo Kanali Mtambi alitoa maagizo haya kwa vijiji hivyo viwili,Kata, Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Wilaya na kwa Katibu Tawala Mkoa wa Mara:
“Utaratibu wa kugawanya mrahaba huo kwa asilimia 60 kwa 40 uzingatiwe, Halmashauri izingatie vijiji vinavyoibua miradi na miradi yao ilingane na asilimia yao ya mgao, Vijiji viibue miradi na Halmashauri ya Wilaya Tarime itapitisha miradi hiyo, fedha hizo zibaki katika akaunti iliyoingia na iende kulipia miradi hiyo iliyoibuliwa, Halmashauri ya Tarime isimamie kwa karibu na kiuadilifu kulingana na taaluma zao na kwa uwazi mkubwa, vijiji vyote vinavyohusika vifanye vikao stahiki na kutoa taarifa kwa miradi hiyo na thamani yake kwa wananchi, Katibu Tawala Mkoa hakikisha unafanya ukaguzi kazi na miradi na fedha za mirahaba na thamani ya mradi ilingane na fedha iliyotumika, Mkuu wa Wilaya Tarime fanya vikao mara kwa mara ya fedha kutoka migodini kwenda vijijini na kutatua changamoto zao huku ukisikiliza hoja za pande zote , sikiliza hoja hizo ukiwa na wataalamu wa Halmashauri, wahusika wote hasa viongozi wa vijiji chini ya diwani hakikisheni mnashirikiana kwa karibu wakati wa utekelezaji wa miradi hii.”
Msomaji wangu nakuomba nikueleza kuwa maagizo haya ya Mkuu wa Mkoa wa Mara yalitolewa mara baada ya pande hizi mbili kila mmoja kutoa hoja zake, awali Mwanakwetu alidhani kuwa siku hii huyu Mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru angewekwa ndani lakini baadaye ilikuja kuonekana huyu mwenyekiti alikuwa sahihi kwa asilimia 100 na alikuwa mtu makini sana na mvumilivu huku akijibu hoja moja baada ya nyingine iliyolewa na bila kukata tamaa hadi Mkuu wa Mkoa alipolifanyia maamuzi na kutoa maagizo yake hayo kama yalivyo.
Baada ya kutoka katika ukumbi huu ndipo Kanali Mtambi alikagua nyumba zile zilizo ndani ya mgodi ambapo baadhi wananchi wamegomea malipo na kugoma kuondoka.
Ziara hii ilikamilika majira ya saa ya moja ya usiku nayeye Mwanakwetu kupanda lile gari la Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Mara ambapo ndani yake alikuwepo Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji kwa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara , Mkuu wa Uhamiaji Mkoa wa Mara, Mwanasheria Mkoa wa Mara, Mwanakwetu na Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Mara na kisha wote hao kurudi Musoma Mjini na Mwanakwetu alipofika kwake aliyaandika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu anampongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara namna alivyousikiliza mgogoro huu hadi alipoutatua na kutoa maagizo yake hayo tisa.
Pia Mwanakwetu anampongeza sana mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru Elias Mwela kwa kuwa mtu mvumilivu, mtu msamilivu , huku akijibu hoja moja baada nyingine mbele ya uongozi wa Mkoa wa Mara katika kikao hiki, awali kikao hiki kilionekana ni kigumu mno lakini baadaye mambo yalitengemaa.
Mwanakwetu anasema kuwa kwa hakika Elias Mwela mwenyekiti wa Kijiji cha Genkuru atafika mbali.
Mwanakwetu Upo?Kumbuka:
“Mwenyekiti Kijiji Cha Genkuru Mfano wa Kuigwa.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257












Post a Comment