Haya yalikuwa ni majira ya mchana wa Februari 16, 2026 ambapo Mwanakwetu yu katika gari aina ya Toyota Land Cruzer nyupe akiwa na wataalamu kadhaa wa afya wakitokea Wilayani Bunda katika Uzinduzi wa Kampeni ya Umezeshaji wa dawa za Kichocho na Minyoo kwa mkoa huu.
Shughuli hii ilizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evens Alfred Mtambi huku viongozi kadhaa wa Wilaya ya Bunda wakishiriki akiwamo mheshimwa Enock Kaminyonge Mkuu wa Wilaya ya Bunda.
Ndani ya hili gari la serikali walikuwemo watu kadhaa, akiwamo Katibu wa Afya Mkoa wa Mara Godbless Utouh huku kando ya ndugu huyu alikuwepo Dkt Margreth Shaku na watu wengine kadhaa.
“Unajua hizi tembe za kichocho na minyoo zimesaidia sana kupunguza visa vya magonjwa haya hapa Tanzania, hali ya sasa ni nafuu ebu fikiria hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ilikuwaje?”
Haya yanasemwa na Dkt Shaku huku soga ndani ya gari hili zikipigwa.
“Hali ya maambukizo ya kichocho kwa sasa ni ya asilimia 26 huku kwa upande wa iliyokuwa Tanganyika ni kwa asilimia 28 na kuna wakati iliamnika kuwa nusu ya Watanzania walikuwa wakiugua kichocho na minyoo.”
Mazungumzo yanaendelea katika gari hili nayeye Mwanakwetu alipotazama hakumuona Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dkt. Zabron Masatu na baadaye alibaini kuwa alikuwepo katika gari linguine.
Hapa kila mmoja anapiga soga zake na aliye kando yake ajenda ni kichocho na minyoo.
“Ni kweli dawa hizi ukimeza hazina madhara wanashauri watoto wawe wamekula kabla ya kuzimeza. Mwaka jana kwetu walipewa, watoto wangu na jirani walikuwa hoi yaani bodabod aliwakuta njiani akawabeba na kuwaleta nyumbani hoi bini taabani. Mmoja alikuwa na nafuu ndiyo aliyefanikisha boda kufika kwangu, wanafika nyumbani namuuliza bodaboda wewe umewatoa wapi watoto wangu akasema mama wapeleke watoto wako hospitali. Niliwapa maji kidogo wakapata nafuu…”
Wakati mjadala huu umepamba moto, Mwanakwetu alikumbuka tukio moja la mwaka 1987 akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mnazi mmoja darasa la tano D huku mdogo wake anayefahamika kama Modestus Makwega akiwa darasa la pili.
“Ilikuwa ni mapumziko ya saa sita mchana anakwenda darasa alikuwa anafundisha mama yao mzazi Mwalimu Doroth Hezron Mlemeta ambalo lilikiwa darasa la pili. Madhumini ya safari hii yalikuwa ni kwenda kula chakula cha mchana ambapo mama yao alikuwa akibeba chakula tokea nyumbani kila siku na kula na wanawe na majira ya mchana alikuwa anakula na wanae wote hapo shuleni. Darasani la pili la mwaka 1987 kulikua na wanafunzi wengi wanaokumbukwa ni Jonhson Kwilasa na Modestus Makwega, ambapo huyu Johnson Kwilasa alikuwa mwanafunzi aliyekuwa akifanya vizuri darasani. Maana mitihani ya darasa hili ilikuwa inasimamiwa na kusahihishwa na mama wa Mwanakwetu ndiyo maana Jina Johnsoni Kwilasa linakumbukwa sana na wakati huo Johnsoni Kwilasa alikuwa anatokea Vingunguti akiwa yeye na mdogo wake.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yu ndani ya gari wanarudi Musoma Mjini wakitokea Bunda katika uzinduzi wa zoezi la umezeshaji dawa za kichocho na minyoo, huku Mwanakwetu akikukumbuka tukio la mwaka 1987 Shule ya msingi Mnazi Mmoja.
Kwa wale wanaokumbuka darasa la pili kwa kuwa huingia darasani baada ya kutoka nyumbani saa tano maana darasa la kwanza wanatoka saa tano , hawa darasa la pili huwa hawapumziki yale mapumziko mafupi ya saa sita hivyo basi mama wa Mwanakwetu akatoa chakula na watoto wake wakala nje ya darasa ili wamalize alafu mama huyu arudi darasani kufundisha darasa la pili.
Mwanakwetu akala wali na maharage harakaharaka na alipomaliza akaosha bakuli lake na kumpa mama yake na mama huyu akasema maneno haya:
“Wanangu kuweni makini kuna kichocho na minyoo siyo mnakuta maji mnachezea tu huku mnakula hovyo hovyo, ukiona dimbwi la maji pita kando… kuna watoto wengine wana michezo michafu wanatoa vindunduli vyao wanakojolea maji yalituama, nyinyi msifanye hivyo maana kuna mtoto mmoja wa kiume leo saa nne alikwenda kununua mihogo katika kibanda cha Mohamed Mihogo wakati anarudi alikutana na dimbi la maji machafu alitoa kidunduli chake akatoa sehemu zake siri(Kindunduli) kando ya dimbi hili ili ajisaidie haja ndogo alipotoa kindunduli chake akayakojolea maji, kumbe ndani ya dimbi hili kulikuwa na waya wenye umeme umeangukwa akapigwa shoti ya umeme hapo hapo amekufa, wanangu kuweni makini madimbi ya maji , maji haya ni machafu, yana kichocho mkikuta dimbi msichezee maji yake ni hatari kwa afya zenu.”
Kweli tulipomaliza kula kila mmoja alirudi darasani kwake na kuendelea na masomo hadi saa nane kengele ilipigwa na sie kurudi nyumbani kwetu Mbagala.
Kumbuka msomaji wangu haya yanamjia akilini tu Mwanakwetu akikumbuka tukio la miaka kadhaa nyuma akiwa mwanafunzi wa shule ya Msingi Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Safari ya kutoka Bunda kuelekea Musoma inaendelea hapa sasa gari hii inafika Kiabakari huku jamaa mmoja ndani ya gari akasema.
“Haya jamani anayetaka ndizi , matunda , karoti na karanga hapa mnunue.”
Kweli gari hii iliposimama wafanyabiashara walifika madirishani kila mmoja alinunua chake huku Dkt. Shaku aliwanunulia wale waliokaa kitu cha nyuma karanga mbichi, huku karanga hizi zikamfikia Sadiki Unga kutoka Star TV na Mwanakwetu.
“Hapa karanga mbichi zinaitwa mafuta ya bunduki.”
Kweli kila mmoja aliyenunua alipata alichotaka kisha kuendelea na safari hadi Musoma Mjini .
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Makala haya siku ya leo yamejaribu tu kumkombusha msomaji wake afahamu hali ya kichocho na minyoo ilivyokuwa mbaya nchini Tanzania na namna Watanzania walivyokuwa wakapambana navyo na hali ya uwoga ilivyokuwa.
Kwa makala haya Mwanakwetu anaamini kuwa kama jitahada za kupambana na kichocho na minyoo zikiendelea hivi hizi mwaka wa 2030 magonjwa haya yatakuwa yamefutika kabisa.
Mwanakwetu upo ?Kumbuka:
“Msitoe Vindunduli Vyenu Katika Madimbi ya Maji.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257







.gif)
.gif)
Post a Comment