Mchungaji Asione Gere

Adeladius Makwega MBAGALA.

“Haya jamani tukae hapa au tuhamie chumba kingine? …tuhamie chumba kingine hapa yupo Mwanakwetu… ili asijue tunachojadiliana… hili ni jambo letu wenyewe akina mama…”

Haya ni majira ya asubuhi ya Februari 9, 2026 Mwanakwetu anayasikia maneno haya, akina mama wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara wakiingia na kutoka Ofisi ya Maendeleo ya Jamii ya Mkoa huu , huku kana kwamba wana jambo lao.

“…jamani tuhamie ukumbi mdogo…pale papo wazi hata Mwasamira hawezi kufika…”

Kweli akina mama hawa, wafanyakazi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara walihamia ukumbi mdogo na kujifungia humo wakijadiliana jambo lao.

Februari 9 ya 2026 huku Mwanakwetu akiwaona wanawake hao bize hekaheka tele, vitenge mabegani , mikoba kwapani, ingia toka hapa na pale, milango ikifungwa kwa nguvu.

Mwanakwetu akisema moyoni:

“Kama shamba limepata mkulima-shughuli imepata watu.”

Mwanakwetu alipochunguza alibaini kuwa kumbe hawa akina mama walikuwa wakijadiliana juu ya kuchagua kitengo hasa kwa kusikia simu zikipigwa huku na kule’

“… hiki hapana, nakwambia tunataka hiyo rangi nyingine, kile kilikuwa kinawaka sana, tunataka hiki doti 500…kwani kile cha jana una doti ngapi?”

Haya yakiwa mazungumzo ya simu ya Bi Upendo Kiswaga-Afisa Maendeleo ya Jamii Ofisi ya Mkoa wa Mara na mtu mwingine ambaye hakufahamika jina lake na hata bila ya kujua kama yu Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro au hapa hapa Mara.



Mwanakwetu akawa anaendelea kufuatilia kimya kimya.

Mwanakwetu akiwa katika utafiti huu akakumbuka jambo moja ambalo alijifunza akiwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania pale Mtumba Jijini Dodoma:

“Unapochagua Kitenge bora kunahusisha kuangalia viashiria maalum vya ubora na miundo inayolingana na mahitaji yako. Kitenge bora ni imara, kinapumua, na kina rangi ang’avu. Katika ubora wa muundo wa kitambaa inashauriwa kiwe cha pamba kwa asilimia 100 ambayo huhakikisha upumuaji mzuri na faraja kwa anayevaa.

Hapa epuka mchanganyiko wa nyuzi za sintetiki, ambazo huhisi kama plastiki, hazipitishi hewa vizuri na hufifia haraka. Mwanamke anayeva kitenge lazima awe huru na awe na amani akivaaa kitenge chake katika mtindo wowote ule.”

Haya Mwanakwetu aliambiwa na Bi Amne Kassam ambaye ni Afisa Sanaa Mwandamizi wa Wizaraa ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo ya Tanzani .

“Kitambaa cha ubora wa juu huhisi laini lakini imara, si chepesi kupita kiasi au chenye kuonekana hadi upande wa pili au ndani, kikionekana hadi upande wa pili hili silo jambo la staha maana mwanamke staha.

Hapa inashuriwa utafute kitambaa cha uzito wa wastani gsm 120–160 ni nzuri kwa mavazi yanayoteleza; gsm 150–175 ni bora kwa uimara. Kiwe na muundo huonekanao wenye rangi ang’avu sawa upande wa nyuma kama ilivyo mbele.

Kitenge kisiwe na madoa madoa yaliyopishana sana hadi nyuki wakuvamie –wakidhani wewe ni mti wenye maua maua mengi ya rangi fofauti. Kagua ukingo wa kitambaa kwa majina ya mtengenezaji, mihuri ya chapa, au saini, ambazo mara nyingi huonyesha uhalisi.”

Hapa hapa Mwanakwetu pia alimkumbuka Bi Hadija Kisubi- Afisa Utamaduni Mwandamizi wa Wizara ya Habari ya Tanzania aliwahi kumwambia maneno haya:

“Katika tamaduni nyingi za Kiafrika, michoro na rangi fulani hubeba ujumbe muhimu kwa mfano: umoja, utajiri, maarifa, dini nakadhalika. Siyo kila mchoro wa kitenge huvaliwa tu hapa lazima uangalie tukio lako- je michoro ya kitenge ulichochagua unalingana na tukio? Mathalani mna tukio la akina mama wa Wakikristo Kanisani kisha kitenge mlichochagua kina mwezi na nyota zile alama za msikitini.

Hapa inahitaji umakini mno. Pia zingatia je tukio hilio linalofanyika je kitenge hiki kinakwenda kushonwa suti blauzi au kinavaliwa kwa kujitanda? Kama kwa akina mama 500 je wengi watashona magauni au suti au watajitanda tu? Kama watashona suti na magauni na blauzi hakikisha kitenge chako ni kizito lakini kama kwa kujitanda hilo halina shida huku ukizingatia hali ya hewa ya mji mlipo.”

Bi Amne Kassam alimuongeza na hili nduguye Mwanakwetu;

“Unapotafuta kitengo bora tambua kuwa kinavaliwa na akina mama, akina mama wana hekaheka nyingi ziwe za kibailojia na kimazingira, chagua rangi isiyochafuka kwa haraka. Pia zingatia bei ya kitenge isiwe ya chini sana maana mara nyingi bei ikiwa ya chini maana yake kitenge lazima hakitakuwa na ubora. Mwisho hakikisha rangi hazitachuruzika, kuchujuka na kufubaa haraka hapa unaweza sugua kitambaa cheupe kilicholoweshwa maji kidogo kwenye sehemu ndogo isiyoonekana sana katika kitenge wakati unanunua rangi ikihamia katika kitambaa hicho kitenge achana nacho. Hakikisha muuzaji anakuonesha sampuli ya kitenge kwa kuiona na kuigusa kabisa na siyo kutumia picha na simu tu. Hapa utakwepa kuuziwa mbuzi katika gunia.”

Mwanakwetu kwa kuwa siyo mchoyo aliamua kumpa hivi vigezo vyote Bi Upendo Kiswaga kama vilivyo ambaye kwa siku mbili alikuwa bize na kikao hicho cha uchaguzi wa kitenge kisha kumwambia vizingatieni ili mje na kitenge bora.

 

Bi Kiswaga alipokea maelezo haya ya Mwanakwetu na kwenda katika kikao chao cha mwisho cha Februari 10, 2026 na kuchagua kitengo chao kwa ajili ya shughuli yao na hadi jioni walichagua kitenge kimoja kati ya sampuli 10.

Walipochagua kitenge chao tu ndipo Upendo Kiswaga akamuonesha Mwanakwetu sampuli ya chaguo lao.

“…tumechagua kitenge hiki…na ni kwa ajili ya Siku ya Wanawake Dunia Machi 8, 2026…hapa Mkoani Mara.”

Mwanakwetu alipotazama chaguo la doti hii ya kitenge alisema naam imezingatia vigezo vyote alivyoambiwa na Hadija Kisubi na Amne Kassam wakati ule.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika Siku ya wanawake Dunia imekaribia huku wanawake wa Mkoa wa Mara wamechagua kitenga chao. Je wewe mwanamke wa mikoa mingine ya Tanzania hapo ulipo mmechagua kitenge cha aina ipi? Je mnavijua vigezo va Hadija Kisubi na Bi Amne Kassam kutoka Wizara ya Habari, Utamadauni, Sanaa na Michezo?

 

Msomaji wangu makala haya ya Mkoa wa Mara yanakupa jibu.

Kwa hakika Machi 8, 2026 si mbali hata kama akina mama wa Ofisi ya Mkoa wa Mara wasipomualika Mwanakwetu lazima ataidoea shughuli hii ili aje kumuona Bi Neema Ibamba (Mke wa Mchungaji) ambaye ni Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Jamii atavyopendeza na kitenge chake chaguo la Mkoa wa Mara- Mchungaji Kanisani Asione Gere.

Kwa wanawake wote wa Tanzania:

 

“Sisi wanaume wa Kitanzania tunawapenda sana, mtake msitake, kama roho mbaya muifanye nyie wenyewe kwa hila zenu.”

Ndiyo maana Mwanakwetu amewaandikia makala haya.

Mwanakwetu upo ? Kumbuka

“Mchungaji Asione Gere.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 















0/Post a Comment/Comments