Adeladius Makwega-MBAGALA.
“Unajua suala la fedha ni gumu sana, ebu fikiria mtu akija kwako kukuomba pesa unamtazamaje? Uwe na fedha hiyo hata kama uwe hauna, Pesa haitoki kwa wepesi.
Shida kumbwa ya vijana leo hii hawana pesa, vijana wanataka pesa.”
Huu ni mjadala wa asubuhi ya Februari 9, 2026 Musoma Mjini baina ya Fidel Balaghaye Afisa Vijana Mkoa wa Mara na Rechol Lazaro ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Bunda.
“Kwa hakika vijana hawataki maneno mengi, vijana wana nguvu ya mwili na akili na ndiyo maana akija kwako anataka umpe pesa na siyo kingine. Unaweza kusema lazima tuzibadilishe akili za vijana hili ni sahihi lakini umbali kutoka ujana kuwa utu uzima ni muda mfupi sana, umbali mrefu ni kutoka utoto kuwa kijana na ndiyo vijana lazima wapende mambo ya haraka na harakati nyingi kupambana ili kuwa salama wakiwa watu wazima na hata uzee.”
Mjadala huu uliendelea huku Mwanakwetu akisikiliza hatua kwa hatua.
“Pesa kwa sasa ndiyo kila kitu, kijana akikosa pesa tusipokuwa makini anaweza kujiingiza katika mambo kadhaa mabaya yasieleweka hadi kupata pesa haramu. Pesa inapokuwa katika matumizi unaweza kuitambua kuwa hii ni halali au hii ni haramu?
Kwa hiyo umakini unahitaji hili kuhakikisha vijana wanafikia malengo yao, pahala walipo na kuwasaidia kwa wakati ili wasiingie katika mikono haramu, shughuli haramu maana wakijiingiza katika shughuli haramu kuwatoa huko ni kazi ngumu.”
Mazungumzo haya yalikuwa mazuri sana kwa Mwanakwetu yalikuwa mithili ya kifungua kinywa cha chai iliyoweka viungo vyote na kipolo cha wali na maharage kwa Mwanakwetu aliyelala njaa siku mbili. Ndugu hawa walipomaliza mazungumzo haya ndipo Mwanakwetu akaamua kuyaandika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Siku kadhaa nyuma Mwanakwetu alikuwa katika bodaboda na huyu dereva wa bodaboda alisema maneno mengi mazito juu ya maisha ya vijana wa Kitanzania kwa sasa.
“Unajua mzee! Mimi najuta kuzaliwa hiki kipindi maana naona mambo ni magumu hayaeleweki, kila kukicha sioni mwanga, nitaendesha hii bodaboda hadi lini?Namfanyia kazi mwenye pikipiki na mimi napata pesa ya kula tu je nitaweza kupata maisha yoyote kwa kazi hii?Kaka mimi sina matumaini kabisa…”
Mwanakwetu amekumbuka kisa hiki cha kijana wa bodaboda ili kuhimiza utatuzi wa changamoto za vijana nchini Tanzania. Kwa hakika lazima watu wenye akili walishughulikie suala hili la vijana wa Kitanzania maana udhohofu wa vijana wengi ni hatari kwa taifa. Mambo ya vijana yafanyiwe kazi haraka, hakuna kijana dhohofu li hali akaja kuwa na familia imara, kijana huyo hayupo, fukara atamza masikini, hakuna fukara aliyemzaa tajiri.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Fukara Atamzaa Masikini.”
Nakutakia Siku Njema
0717649257


.gif)

.gif)
Post a Comment