Adeladius Makwega MBAGALA.
“Wazee watano wamekaa katika viti vya chuma, mmoja kavaa shati, koti na suruali ya rangi ya udongo na ameketi kiti cha kwanza, kiti cha pili kipo tupu lakini yupo mzee mwingine anakitazama kiti hiki cha chuma huku akiwa amesimama na mguu wake mmoja umefungwa POP nyeupe, mikono yake miwili imepajika magogo mawili ya mbao yanayomsaidia kutembea, huku mzee huyu anaongea na wazee wenzake, kiti cha tatu ameketi mama mmoja mtu mzima, amevaa vitenge huku akitupa maneno mawili matatu na wazee wenzake , kiti cha nne yupo mzee mwingine mwanaume lakini taswira yake haionekani vizuri kutokana na miti kumziba na kiti cha tano yupo mzee mwingine kakaa akiwa amevalia suti maridadi na kofia kama Lodi Lofa.”
Haya ni majira ya asubuhi ya siku hii Mwanakwetu anakutana na taswira hiyo kama ilivyo mbele yake. Swali la Mwanakwetu likawa hawa wazee wana shida gani?
“Hawa wazee huwa wanakuja kuhakikiwa na ni watumishi wa umma wastaafu, huu uhakiki wao unafanyika kwa mwaka mara moja na kama mtumishi yu hai na asipofanya hivyo hili linaweza kusababisha kukosa haki zake.”
Hawa watumishi wanahakikiwa iwe PSSSF au Hazina Ndogo, pale unapofanyika uhakiki lazima wafanye hivyo ili kujihakikishia usalama wa haki yao. Mwanakwetu akaagana na ndugu huyu aliyemjibu haya yote kisha kwenda pahala kwingine na kuambiwa haya:
“Makwega mimi nyumbani ni Tukuyu, uhakiki ulikuwa unafanyika PSSSF Mbeya Mjini, mwanzoni kazi ilikuwa nyepesi, maana kaka yangu alikuwa na motokali yake ndogo, ilikuwa inawekwa mafuta, sisi ambao tupo kazini tunachangia mafuta ya Tukuyu hadi Mbeya na kurudi na kisha mtoto wa kaka ambaye ni mjukuu wa wazee wetu ndiyo akawa anamkokota baba hadi PSSSF Mbeya . Hali hii iliendelea hadi mzee alipozidiwa. Hapa tuliwasiliana nao wakasema tuende hospitali ili kutambua hali hiyo kisha mimi nilienda PSSSF mzee alihakikiwa lakini baadaye alipokuwa na hali tete tulishindwa hadi mzee anafariki”
Mwanakwetu alifanya mawasiliano na mama mmoja mstaafu na yeye aliyasema haya:
“Uhakiki kwa Wastaafu ni mzuri kama ukiwa na hali nzuri, maana utakutana na wenzako uliyofanya nao kazi, lakini hali yako inapokuwa mbaya inakuwa na ni aibu, kero kufika katika uhakiki huo maana ulikuwa unavaa vizuri sasa unajifunga funga nguo kutoka na na hali yako ya kiafya kudhorota, kuwa mbaya, kila dakika unapelekwa uani. Mimi nashauri uhakiki ungefanyika katika ofisi za Wakuu wa Wilaya.”
Mara baada ya Mwanakwetu kuyapata haya yote ndipo alipoamua kuyaweka haya yote katika makala haya unayoyasoma msomaji wangu.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika uhakiki huu shabaha yake ni nzuri, kujua watumishi wetu waliostaafu wana hali gani? Wana changamoto gani?
Mwanakwetu kwa makala haya anashauri uhakiki huu ni vizuri kufanyika maeneo walipo wastaafu hao iwe ngazi ya mtaa/kijiji au kata na siyo sahihi mhakikiwa asafiri KM 70 kuhakikiwa wakati hali yake ya kiafya ni mbaya, mathalani mhakiki asafiri kutoka Tukuyu hadi Mbeya KM 70 au asafiri kutoka Mahenge Ulanga hadi Morogoro Mjini, huu ni uonevu kwa wastaafu wetu. Wapo wastaafu wenye watoto waliozaa, kuzaa watoto ni majaliwa.
“Wapo wastaafu hawakujaliwa watoto kazi za umma ndiyo ilikuwa mtoto wao, nani atawapa motokali , nani atawanunulia mafuta, mjukuu watamtoa wapi ili awasindikize?”
Kinachoweza kufanywa iwe kwa PSSSF au Hazina Ndogo watumishi wake kama uhakiki ni mara moja kwa mwaka basi wawekewe mafuta katika magari yao ya umma, wapewe posho kisha wazunguke kuwafuata wastaafu majumbani na hili linawezekana.
“Mtumishi kastaafu kwa mujibu wa sheria maana yake hawezi kuifanya kazi ya umma vizuri, sasa inakuwaje tena aanze kusumbuliwa katika baiskeli , bodaboda, mabasi na magari kisa haki yake? Hili halikubaliki.”
Je shinda ni PSSSF? Shida ni Hazina? Shida ni Wizara ya Fedha? Shida ni Wizara ya Utumishi wa Umma ya Tanzania? Shida ni Bajeti Bungeni? Shida ni Baraza la Mawaziri?Lazima tumjue mchawi ni nani katika hili au kama ni Shida ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali tumjue kwa jina lake ili nayeye akija kustaafu akija kuhakikiwa tuwaambie wajukuu zetu huyo msimangeni maana ndiyo chanzo cha hizi shida zote za leo za wastaafu.
Kwa hawa watumishi wa Hazina, PSSSF na hata mahospitalini Mwanakwetu anawaomba watoe huduma hii vizuri kwa wazee wetu kwa moyo wote na hizi mamlaka zilizotajwa awali zilifanyie kazi jambo hili haraka kila mmoja ni mstaafu ajaye.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Kila Mmoja Ni Mstaafu Ajaye.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
.gif)







Post a Comment