Japokuwa Kanisa la Tanzania Tumezika Makadinali Wawili Lakini Ili Hatujalifanyia Kazi

 


Adeladius Makwega-Tarime MARA

Wakati Polcarp Kadinali Pengo anafariki, taratibu za mazishi zinafanyika na hadi kuzikwa pale Pugu nje Kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kiongozi huyu wa Kanisa la Katoliki la Tanzania, Mwanakwetu alikuwepo Musoma Mkoani Mara ambapo ni Jimbo Katoliki la Musoma, nchini Tanzania.

Kwa hakika wiki hizo za mwishoni mwa mwezi wa Februari mwaka wa 2026 zilikuwa na majukumu mengi kazini kwa Mwanakwetu na hasa juma la kuhitimisha mwezi Februari ambapo kulikuwa na vikao vingi na ziara kadhaa za viongozi wa Mkoa wa Mara na hata wa kitaifa kufika mkoa huu nyumbani kwa Mwenyeheri Julius Kambarage Nyerere, naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi wakati huo ambaye ni Muangalikan alitembelea Wilayani zake mbili: Serengeti Februari 25 na Tarime Februari 27, mwaka 2026. Huku Mwanakwetu kwa kazi aliyekuwa anafanya ziara zote hizo alipangiwa awepo katika maeneo haya.

Awali Mwanakwetu alipanga katika ratiba yake mwezi ya mwezi Machi, 2026 awepo jijini Dar es Salaam huku ratiba ya mazishi ya Kadinali Pengo ilikuwa Februari 28, 2026. 


 

Kwa bajeti ya Mwanakwetu na mambo mengi ya Mwezi Januari, Februari na Machi kama vile malipo ya karo za watoto na jamaa zake kadhaa, miezi hii huwa migumu kidogo kwa wazazi wenye watoto wengi, hivyo ni miezi ambayo Watanzania wengi wanawekeza katika malipo ya karo na siyo kitu kingine na maisha yao huwa magumu lakini kupanga ni kuchagua. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mwanakwetu. Kwa hiyo Mwanakwetu alikuwa na bajeti ya kuwa Dar es salaam kufika huko kwa njia ya basi na siyo ndege au chombo kingine chochote ambapo nauli ya basi ilikuwa kama shilingi lakini moja za Kitanzania sawa na dola 40 za Kimarekani kwa mwaka wa 2026, hivyo basi Mwanakwetu japokuwa alitamani kumzika Polcarp Kadinali Pengo Mwanakwetu alishindwa kwa hoja ya wa kufika huko Dar es Salaam, kazi tele zilizomzunguka na gharama ya yeye kushinda kukata tiketi ya ndege.

Mwanakwetu siyo mgeni wa Pugu ambapo pale kuna familia kadhaa za Wakatoliki wa enzi hizo wa eneo hilo na hata kama Mwanakwetu angefika Pugu katika maziko haya na familia yake nzima angewekewa chumba cha kulala yeye na familia yake, familia mojawapo ni ile ya marehemu Samjela pale Pugu mjini ambaye aliwahi kuwa Afisa Elimu wa Mkoa wa Dare es Salaam ambaye alimuoa Dada wa Kingunge Gombale Mwiru na familia nyingine ya Wakatoliki wa zamani wa Pugu ni ya Peter Pinda huyu Waziri Mkuu wa pili wa Serikalia ya awamu ya nne.Pia Pugu siyo mbali na nyumbani kwa Mwanakwetu pale Mbagala.


 

Kwa hiyo Mwanawetu kwa hoja ya kipato hakuweza kwenda kumzika Kadinali Pengo pale Pugu lakini Mwanakwetu alijawa na matumaini makubwa na furaha tele kwa uwepo wa Wakristo kadhaa kutoka Parokia ya Mbagala na parokia zote zilizozaliwa kutoka Parokia ya Mbagala ambayo ni Parokia ya asili ya Mwanakwetu kwa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Kwani ukoo wa Makwega ndiyo mojawapo ya Wakristo wa awali waanzilishi wa Parokia ya Mbagala iliyoanza mwaka 1975 na hata wanakwaya wa kwanza kwanza wa Kwaya ya Mtakatifu Antony wa Padua walikuwa ni akina binti Makwega shangazi wa Mwanakwetu ambapo kiongozi wa kwaya hii alikuwa huyu huyu Peter Pinda awali parokia hii ilikuwa pale Kituo cha Kiroho Mbagala.

“Kwa hakika Kadinali Pengo hajakwenda mkiwa, watu wa Mbagala walioshiriki mazishi haya mmeniwakilisha vema ndugu yenu Mwanakwetu. Hata watani wa Mwanakwetu Wafipa wote  mmeniwakilisha vema.”

Kwa kuwa kiongozi huyu mwili wake umelazwa kaburini Februari 28, 2026 yako mambo mengi yamefanywa na kiongozi huyu na sie Wakristo wa Tanzania ikiwamo Ukristo kuweza kufikia maeneo yote ambayo hayakuweza kufikiwa awali na kazi hii siyo tu Kanisa Katoliki la Tanzania tu bali Kanisa zima la Ulimwenguni maana kwa sasa huyu Yesu Kristo Mfufuka anatajwa kila kona ya Tanzania .

Kwa hakika Februari 28, 2026 Tanzania imeuweka kaburini mwili wa Kadinali wa pili mzalendo, ukitanguliwa na marehemu Laurean Kadinali Rugambwa ambaye nayeye aliliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Tunapomaliza kumzika Kadinali Pengo huku mafanikio kadhaa yakitajwa Mwanakwetu anaona lipo jambo moja ambalo Kanisa la Tanzania hatujalifanya vizuri nalo ni hakuna uwekezaji mkubwa wa kuwatambua Wakristo walioishi maisha ya utakatifu, kwa hakika ukiitazama michakato ambayo imefanywa ni wale waliyokuwa watawa na au watu maarufu ambao wanatambulika kwa haraka swali ni je Kanisa la Tanzania kwanini hatufanyi uwekezaji wa kuwatambua wale Wakristo wa kawaida ambao maisha yao yanaweza kuigwa na Wakristo wengine kama tukiyafuatilia maisha yao?


 

Kwa hakika ukisema hakuna Wakristo walionesha uhodari maisha yao na kuyaisha na kuwa kioo kwa wengine ili litakuwa siyo kweli, wapo wengi lakini je jambo ili limetiliwa maanani?

Kwa hakika uwekezaji mkubwa wa ufunguzi wa Majimbo mapya, Parokia mpya, Vigango vipya na Jumuiya mpya zinafanyika na kuongeza idadi ya Wakristo, majengo makubwa makubwa shule, hospitali na miradi kadhaa ya kijamii ikijengwa, swali linalobaki je tunawatambua ndugu zetu katika maisha yetu wanayoishi walionesha uhodari wa maisha yao kulingana na Imani yetu? Au hoja zetu ni zile zile kama za Mwanakwetu anavyodai kuwa;

“Kwa bajeti ya Mwanakwetu na mambo mengi ya Mwezi Januari , Februari na Machi ikiwamo malipo ya karo za watoto, miezi hii huwa migumu kidogo kwa wazazi wenye watoto, hivyo ni miezi ambayo Watanzania wengi wanawekeza katika malipo ya karo na siyo kitu kingine hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Mwanakwetu. Kwa hiyo Mwanakwetu alikuwa na bajeti ya kuwa Dar es salaam kufika huko kwa njia ya basi na siyo ndege au chombo kingine chochote ambapo nauli ya basi ilikuwa kama shlingi lakini moja za Kitanzania sawa na dola 40 za Kimarekani kwa mwaka wa 2026, hivyo basi Mwanakwetu japokuwa alitamani kumzika Polcarp Kadinali Pengo Mwanakwetu alishindwa.”

Kama uwekezaji huu wa kuwatambua ndugu zetu hao utafanyika vizuri utasaidia mno waamini kuweza kujifunza kwa karibu maisha ya ndugu zao walioishi katika ardhi yao katika nyakati tofauti.

Maana kujifunza kwa mtu aliyeishi mbali na ardhi yako, utamaduni tafauti kidogo inakuwa vigumu, japokuwa lazima ujifunze maana hakuna namna.

“kujifunza kwa mtu aliyeisha katika utamaduni wako, changamoto zako, eneo lako, akila vyakula vya aina yako na unaona namna anavyojitahidi kulikabili jambo na kulishinda kama ilivyokuwa kwa wale Mashahidi wa Uganda inajenga ujirani na wewe.”

Kwa hakika sasa Tanzania tumezika makadinali wawili huku Tanzania tukiwa hatuna mtakatifu zaidi ya yule Muzeeyi Kiwanuka ambaye mchakato wake ulifanyika Uganda.

Mwanakwetu kwa bahati nzuri aliwafahamu kwa karibu Laurean Kadinali Rugambwa na hata Polcarp Kadinali Pengo, kwa hiyo katika makala haya Mwanakwetu aliamua kuiweka tafakari yake katika maandishi ili nduguze katika Imani waisome wakati wakimsindikiza kaburini.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika sisi Wakristo wa Tanzania tutafakari katika ili kama ni uwekezaji ufanyike katika kuwatambua ndugu zetu hawa katika imani,najua tunaendelea kutegemea kujifunza mengi katika watakatifu wa maeneo mengine huku muda mwingine hata kuyatamka majina yao inakuwa kazi ili siyo kosa lakini kutofanya mchakato wa waamini wetu hadi kufikia utakatifu ni kosa kubwa tutakuwa kama Mwanakwetu alivyotegemea Wakristo wa Parokia zilizoanzishwa na Parokia ya Mbagala kwenda kumzika Kadinali Pengo.

Kwa hakika na kweli kabisa Kanisa lina Watakatifu wengi na mengi ya kujifunza katika maisha yao lakini ni vizuri kuwa na watakatifu wa nyakati zetu, maeneo yetu, ujirani nasi na hata ukiyasoma au kusimuliwa maisha yao kama ni mama basi unamuona namna anavyolea watoto wake wakati mumewe haeleweki, mumewe kamtelekeza huku akiendelea kushika Imani yake kama ni baba unamuona namna anavyoishi huku akipambana na maisha ya kuitunza familia yake , namna anavyoanguka kisha anasima kutatua changamoto za ndoa yake.

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Japokuwa Kanisa la Tanzania Tumezika Makadinali Wawili Lakini ili Hatujalifanyia Kazi.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

Frbruari 27, 2026



 

 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments