Adeladius Makwega-MBAGALA
“Leo ni Jumapili ya sita ya mwaka A wa Liturujia ya Kanisa. Katika Injili ya leo Yesu anaweka wazi muelekeo wa maisha kwa wanafunzi wake. Hapa anathibitisha sheria na manabii; hakuna hata kimoja kinachopaswa kuvunjwa bali kutimizwa.
Hii ina maana ya kuuruhusu moyo kuingia katika kiini cha sakramenti na amri, kwenda zaidi ya kushika tu kwa nje. Anawaambia, ndiyo, usiue; lakini kuua si tu tendo la kuondoa maisha ya mtu. Kuhifadhi hasira moyoni mwako ni mwanzo wa kuua. Ndiyo, usizini.Tamaa ya macho ni mwanzo wa uzinzi. Kutii amri kunahitaji kushughulikia mzizi wa dhambi, si tu kuepuka tendo baya. Hakuna amri ya kutenda dhambi, bali ni amri za kuwa wema ili kutenda mema. Hii ni njia nzuri ya kujiandaa kwa kipindi kijacho cha Kwaresima.
Ee Mungu, tupe moyo mpya ili, tukitakaswa na tamaa mbaya, tuweze kutenda haki na kupenda wema. Amina.”
Haya ni maelezo ya utangulizi katika homilia ya jumapili hii kama yalivyotolewa na Kadinali Luis Antonie Tagle Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki Ulimwenguni inayoshughulika na Uinjilishaji wa watu.
“Yesu hakuja kutangua sheria bali kutimiliza, na amri zote ameziweka katika amri moja muhimu... kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Twaweza kufanya mengi na tukasifika lakini hayatakuwa na faida kama hayaongozwi na hekima ya Mungu na hayana roho ya upendo... Basi wapendwa, “Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu: roho, mioyo na miili yenu mbali na hatia yoyote, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo” (1Tes 5:23).
Leo dunia inakosa amani kwa sababu tunakosa upendo wa kweli: Migogoro ya kisiasa na vita, rushwa inayosambaa kama ugonjwa, Familia zinazovunjika Vijana wanaokatishwa tamaa Ubinafsi unaowatupa maskini pembeni, Maneno ya chuki, mitandaoni na majumbani. Msingi wa haya ni moja: tumeacha sheria ya upendo wa Kristo. Na ndiyo maana leo Yesu anatuita kwa sauti kuu: ‘Rudini kwenye upendo, rudini kwenye amani.’ Masomo ya leo yanatuambia kwa sauti moja: Sheria ya Kristo ni Upendo. Upendo ndio unaotengeneza haki. Upendo ndio unaotengeneza amani. Upendo ndio unaotengeneza familia, taifa na ulimwengu.”
Haya ni sehemu ya tafakari ya dominika hii kama ilivyotayarisha na Padri Joseph Herman Luhela na tafakari yake kutumika katika kurasa za Redio Vatikani. Haya ni machache kati ya mengi yaliyoijenga dominika hii kama yalivyokusanywa na Mwanakwetu .
Wakati haya yakiendelea katika kuta za kanisa hali ya hewa ya Mji wa Songea ni nyuzi joto 21 unyevunyevu ni wa asilimia 20, ujirani na mvua ni wa asilimia 88 na upepo ukivuma kwa KM 5 kwa saa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Hakuna Hata Kimoja Kinachopaswa Kuvunjwa Bali Kutimizwa.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
.gif)
.gif)
Post a Comment