
Adeladius Makwega-MBAGALA
“Novemba 19, 2011 Serikali ya mpito ya Tripoli ilisema mwana wa Muammar Gaddafi alikamatwa alipokuwa akijaribu kukimbilia nchi jirani ya Niger. S aif al-Islam Gaddaffi, aliyekuwa akitoroka amewekwa kizuizini bila kujeruhiwa katika kambi ya jeshi mjini Zintan, maili 90 kusini-magharibi mwa Tripoli.
Ilisemekana Saif alikuwa katika afya njema, kulingana na waziri wa haki Mohammed al-Alagi, ingawa picha zilionyesha vidole vilivyofungwa bandeji. Saif alikamatwa karibu na mji wa kusini wa Sabha akiwa na wasaidizi wawili, wakijaribu kumsafirisha kisiri kwenda Niger. Saif al Isilamu alizaliwa mwaka 1972 na ndiye mtoto mkubwa kati ya watoto saba wa Muammar Ghadaffi.”
Hii ilikuwa ni taarifa katika vyombo vya habari ulimwenguni Novemba 19, 2011 juu ya mtoto huyu wa Ghadadff, miaka 15 iliyopita.
Miezi minne baadaye yaani Machi 2012 Mwanakwetu akiwa chumba cha habari cha DW Kiswahili pale Bonn akiwa na ndugu Abdul Mtulya uliibuka mjadala mmoja wa namna kijana huyu wa Ghaddaffi alivyokamatwa mwaka wa 2011.
“Wakati Saif Al Isilamu anataka kuvuka nchini kwao kwenda Niger kwanza walitumwa wasaidizi wake wakazungumze na jamaa wanaofanya biashara ya kubeba abiria kama taksi za jangwani ambapo huweza kuwa magari au wakati mwingine ni wanyama kama vile punda, ngamia na farasi hii huwa ni misafara mirefu.
Wale wasaidizi wa mtoto wa Ghaddaffi wakaongea na jamaa wa Taksi na wakamwambia dereva huyu kuwa watasafiri mida ya usiku wanakwenda Niger.
Huyu dereva wa taksi Jangwani alitaja pesa nyingi kwa kuwa alipowatazama hawa wateja wake aliwatilia shaka, ili kumkataa mteja unataja dau kubwa, dau la juu, wateja wakakubali dau hilo la juu, dereva akasema sawa lakini nilipwe nusu ya nauli hiyo jamaa wakakubali na dereva akalipwa ya nusu ya fedha hiyo.
Dereva huyu wa misafara jangwani akawa na mashaka zaidi huku hata muda wa safari nao ukawa tatizo la kumpa uwoga tele, alitetemeka sana kama kondoo ndani ya barafu.
Wateja wakaondoka zao wakajiandaa na dereva wa misafara ya jangwani hivyo hivyo.
Huyu dereva akajihoji mno akasema kama hawa abiria ni hatari ninaweza kuwabeba kisha nikimaliza kazi wataniua ili nisije kutoa siri zao , ngoja nitoe taarifa kambi ya kijeshi ili kama wakiwa hatari mimi nitabaki salama na hii nusu ya pesa inanitosha.
Dereva wa taksi jangwani akafanya hivyo hivyo akawaambia wale askari ndani ya kambi ya kijeshi wakatengeneza mtego mzuri wa kufuatilia msafara huo .
Huku mtego ukategwa katikati ya safari. Hakuambiwa hilo huyu dereva lakini alihakikishiwa usalama wake tu
Dereva wa taksi jangwani akatoka kambi ya jeshi kisha kwenda kupumzika kidogo na kisha kuwachukua abiria wake na kuanza safari.
Wakiwa safarini huyu dereva alibaini kuwa kuna abiria mmoja alikuwa sura yake imefunikwa sana na ni vigumu kumtambua hilo likampa mashaka zaidi huku wakichanja mbuga jangwani .
Wakaenda jangwani karibu nusu ya safari gafla wakavamiwa wakiambiwa mikono juu na wanajeshi wenye silaha kubwa kubwa, wale wanajeshi wakawakamata wote na kuwaweka chini ya ulinzi kisha kuwakagua mmoja baada ya mwingine na kuwatambua na ndipo ilipobainika kuwa aliyekuwa amebebwa alikuwa nia Saif Al Isilamu Gaddaffi mtoto miubwa wa Mummary Gaddaffi wa Libya ambapo kipindi hiki mtoto huyu wa Gaddafi alikuwa anatafutwa na dongo nono lilikuwa ubaoni.”
Katika ule mjadala pale DW Kiswahili ikaja hoja je huyu dereva wa taksi za jangwani alifanya sahihi?
Mjadala ulikuwa mzuri na wakasema kama asingalifanya vile mara baada ya kuwavusha mpakani tu huyu dereva wa taksi angeuwawa ili kuficha siri kuwa kuna watu waliovuka kutoka Libya kwenda Niger kutambulika.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwanza msomaji wangu fahamu kuwa huyu Saif Al Isilamu ndiyo ameuwawa kwa kupigwa riasasi Februari 3, 2026 akiwa na umri wa miaka 54 ambaye ndiye alikuwa mtoto kipenzi wa Mummar Gaddaffi, akiwa ni msomi wa shahada ya uzamifu.
Jambo la pili na mwisho ni moja tu, hawa wanaoshiriki katika harakati na hekaheka za watu wasiojulikana mwisho wa siku lazima wanapotezwa maana wao ndiyo wanajua kipi kilitokea, nani yu wapi. na nani aliyewatuma kwa hiyo usalama kwao haupo kwani walitakiwa kuwa wajanja wenye hekima mapema sana kama ilivyokuwa kwa dereva huyu misafara jangwani kule Libya mwaka wa 2011.
Mwanakwetu upo?Kumbuka
“Dereva wa Misafara ya Ngamia Jangwani.”
Nakutakia siku njema.
0717649257


Post a Comment