CCM Isitishe Mara Moja Zoezi Lake la Kuwapokonya Madiwani Wake Pikipiki.

 

 

Adeladius Makwega-MBAGALA

“Makwega unakumbuka vile visa vya vijana wa zamani unamtaka mwanamke, anakusumbua wee kisha unampa kitu bila ya kumpa hati au kadi kisha baadaye mapenzi yamechujuka unapokonya!”

Mwanakwetu akasema hayo mapenzi ya watoto, mapenzi wa watu timamu wanaojiamini kama Mwanakwetu wakimpa kitu anayempenda anampa na hati iwe ni gari anampa na kadi, haya ni mapenzi ya kweli.

Jamaa akauliza ati kaka Mwanakwetu wapo wanaofanya hivyo?

Mwanakwetu akajibu naam, wapo maana kila mmoja anahonga kulingana na uwezo wake, mwenye baiskeli anahonga baiskeli, mwenye bodaboda anahonga bodaboda na mwenye nyumba anahonga nyumba na mwenye gari hivyo hivyo, wewe unahonga nini?

Jamaa akawa anacheka sana.

Awali kabla na maelezo haya Mwanakwetu alikuwa kikaoni simu ilipigwa sana kisha Mwanakwetu akaipokea na kusema kwa sauti ya chini.

“Kaka Nipo Kikaoni, Tuma meseji.”

Jamaa huyu akatuma meseji, Mwanakwetu bize na kikao, meseji hajaisoma, jamaa akapiga tena simu, Mwanakwetu akapokea, jamaa huyu akasema:

“Makwega soma meseji, Nyinyi mliosoma mtusaidie ndugu zenu, tunapata fedhea.”

Mwanakwetu akasoma meseji hakuielewa vizuri akaweka simu kando akaendelea na kikao, kikao hiki kikafanyika hadi majira ya mchana. Mwanakwetu alipotoka kikaoni akasoma tena ule ujumbe, ulikuwa maneno haya:

“Wanahabari mnatusaidiaje Madiwani wa CCM Kupokonywa Pikipiki?”

Gafla Mwanakwetu akapata mgeni hivyo suala la ujumbe huu hakuhangaika nalo tena, akawa bize na huyu mgeni ambaye alikuwa na malalamiko yake pahala fulani, akapelekwa akaongea na wahusika kisha mgeni huyu kuondoka zake.

 

Baada ya muda fulani jamaa huyu alituma ujumbe na kupiga simu mara kadhaa, Mwanakwetu akapiga lakini simu yake haikuwa na vocha, jamaa akampigia simu Mwanakwetu kisha akakata, akapiga tena na kuyasema hayo maelezo yale ya awali ya kuhonga gari na kuhonga nyumba. Jamaa huyu akaenda mbali akisema kuwa mwaka wa 2025 CCM kilitoa pikipiki kwa viongozi kadhaa wakiwamo madiwani wa CCM lakini cha kushangaza CCM imeagiza pikipiki zirejeshwe kwa makatibu wa CCM wa Wilaya.

“Kaka pikipiki yenyewe imechoka kweli, watu washakalia sana, Mungu kamjalia binadamu makalio tofauti (ashakumu si matusi) vile viti vyake vimejambiwa sana… vijambiwa mno aina zote za mashuzi …leo hii jamaa wanazitaka zile pikipiki! Sasa hawa jamaa wanashangaza sana hawajui kuwa kwa ngazi ya kata diwani ni mtu wa nne? Huku katika ngazi ya chama taifa kuelekea nafasi za dola diwani ni mtu wa tatu anaanza rais anakuja mbunge kisha diwani. Hawa jamaa hawana adabu wanatudhalilisha sana.”

Mwanakwetu akasema maneno haya kimoyo huku akihofia kuyatamka kwa nguvu yangeweza kumtia machungu diwani huyu wa CCM aliyepokwa pikipiki:

“Katibu wetu Mkuu Dkt. Asha Rose Mingiro yeye ni mama, Asha Rose alikuwa Binti Kigori labda alipokuwa binti aliwahi kupewa kitu bila hati, kisha jamaa akaja kukichukua, ndiyo maana madiwani wake wa CCM sasa mnarudisha pikipiki…”

Jamaa huyu hakuyasikia maneno haya kisha akawa anasema:

“Kuna maneno mengi, wanasema sijuhi Tundu Lissu kafanya ili na lile Tundu Lissu kafanya hiki na kile…”

Mwanakwetu akasema hapana, Tundu Lissu yupo korokoroni anahaingika na kesi yake uhaini, habari za pikipiki za CCM walizopewa madiwani na kurudisha wapi na wapi? Tundu Lissu mtoto watu naona hausiki. Nyinyi si mpo mliofunga ramadhanina Kwaresma Litazameni jambo hili kwa haki.

 

Jamaa huyu akasema kweli Mwanakwetu kweli Mwanakwetu.

Kisha Mwanakwetu akamwambia huyu jamaa naomba uniachie kama saa mbli nilifanyie kazi kisha nitarudi kwako.

Baadaye Mwanakwetu alibaini kuwa ni kweli maeneo kadhaa madiwani wa CCM walipewa pikipiki kisha kuzitumia wakati wa kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 nchini Tanzania huku hawakupewa kadi za pikipiki hizo, lakini baadaye kumekuwa na heka heka za kuzirudisha pikipiki hizo na ndiyo maana huyu diwani wa CCM alilalamika kwa nduguye Mwanakwetu.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Katika hili Chama Cha Mapindizi Taifa kijitafakari, wewe kama mzazi unapoamua kwa matakwa yako kumnunulia mtoto wake nguo ili ajisitiri , iweje tena azivae nguo hizo wakati wa sikukuu ya Krisimasi kisha sikuu inaisha unampokonya, ili halikubaliki , ili halikubaliki.

Mwanakwetu anasema CCM Taifa isitishe Zoezi la Kuwapokonya Madiwani wake Pikipiki.

Mwanakwetu Upo?Kumbuka:

“CCM Isitishe Mara Moja Zoezi Lake la Kuwapokonya Madiwani Wake Pikipiki.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

 


 

0/Post a Comment/Comments