Haya yalikuwa majira ya mchana ya Februari 20, 2026 Mwanakwetu yu pahala fulani na wenzake watatu. Hapa Mwanakwetu akilini mwake anataka kuandika makala ya Buriani ya Porcarp Kadinali Pengo ambaye alifariki dunia Februari 19, 2026 wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam.
Gafla pahala alipo Mwanakwetu wakaingia ndugu wageni wawili, ndugu hawa wakaongea na ndugu mmoja, kisha Mwanakwetu kuomba namba zao za simu, hapa akawa anaziandika namba hizi vizuri katika simu yake.
Wakati inaandikwa namba ya pili simu ya Mwanakwetu ikamponyoka puuu hadi sakafuni chini na kufunjika kioo.
“Lo salale simu yangu imevunjika kioo tena! Siwezi kuishi bila simu, ngoja nifunge virago vyangu niende kwa fundi kuitengeneza.”
Mwanakwetu akaagana na wenzake na kwenda kwa fundi umbali kama wa KM mbili hivi. Kwa bahati mbaya alipofika hapa fundi mwenyewe hakuwepo, bali alikaribisha na vijana wawili katika kibanda hiki caha fundi makini hapa walianza kumpa huduma.
Vijana hawa walikuwepo wawili wa kike na wakiume, kwa bahati mbaya huyu kijana wa kiume hakuwa na lugha nzuri kwa wateja wake. Mwanakwetu akasema moyoni, mwenyewe ni mwenyewe tu:
“…hawa vijana hawatambui kwanini sikwenda kwa fundi mwingine, vijana hawa hatambui namna fundi mwenyewe alivyo muungwana kwa wateja wake…”
Mwanakwetu akakaa katika dawati kando huku kijana huyu anatengeneza simu hii vizuri tu.
Mwanakwetu akiwa dawatini akasema kuwa kwa sasa ni saa 11.14 ya jioni lakini kama simu yangu ingekuwa nzima, saa hizi ningekuwa nimeshaimaliza makala ya Buriani Porcarp Kadinali Pengo, aaah lakini nitaindika baadaye nikiwa nyumbani.
Mwanakwetu akiwa katika dawati hili akawa anatafakari mambo kadhaa ya Kadinali Pengo:
“Kama Kadinali Pengo alizaliwa Agosti 5, 1944 maana yake wazazi wa Baba na Mama yake ni kizazi cha kati ya mwishoni mwa mwaka 1880 na mwanzoni mwa mwaka 1920 ambapo kipindi hiki ndiyo ujio wa Wamisionari na huku baba na mama yake wanaweza wakawa kizazi cha 1921-1930 ambapo ni kizazi cha awali awali kuuona Ukristo tangu utoto. Huku Kadinali mwenyewe ndiyo kizazi ya kati ya 1940-1959 ambapo kinaweza kuwa kizazi cha pili cha Wakristo na hata kizazi cha tatu mara baada ya ujio wa Wamisionari hapa Tanganyika.
Huku vizazi hivi vyote vilishuhudia ndoa la mitaala mtu mmoja kuwa na wake hata 10. Huku watoto wa baba mmoja wakiwa hadi 100 , familia zikikaa pamoja na zikiishi kidugu, baba na mama wakiwa pamoja hadi kifo chini ya tamaduni za Kiafrika. Jamii ya Kiafrika haikuwa na watoto wa mitaani.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anatengeneza simu yake kwa fundi na hapa amekaa katika dawati, binti mmoja mweusi aliyempokea Mwanakwetu awali kwa fundi huyu akasema baba tunaomba pesa ili tukalipie kioo kipya maana fundi mwenyewe hayupo na sisi dukani hawatuamini. Mwanakwetu akasema sawa lakini pesa yangu ipo katika simu, naomba simu ndogo niweke line zangu kisha nikutumia pesa yako.
Binti huyu akajibu hana simu ndogo lakini waende kwa wakala ili ni jambo dogo na litaisha. Kweli walifika hapo kwa wakala na hapa Mwanakwetu akapewa simu ndogo akaweka line zake mbili kisha binti wakala akamuongoza kutoa pesa maana mwanga wa kioo cha simu ndogo ya wakala ulikuwa hafifu na macho ya Mwanakwetu yalikuwa hayaoni kitu bali giza totoro.
Kioo kikalipiwa kama dola 12 kisha Mwanakwetu kurudi katika dawati alilokuwa ameketi awali ili fundi amalizie kazi yake.
Binti yule katika kibanda cha simu akaongea na kijana wa kiume katika kibanda simu ambaye ndiyo anaikarabati simu ya Mwanakwetu akisema:
“Jamani Fundi mmalizieni huyu baba kumtengenezea simu yake maana nataka niwahi kurudi nyumbani kumpika futari mume wangu saa hizi wateka hakuna hadi kesho mume wangu kafunga Ramadhani.”
Mwanakwetu akayaingilia mazungumzo haya na kusema haya:
“Mumeo amefunga Ramadhani na wewe umefunga nini?”
Binti akajibu kwa kucheka kuwa yeye amefunga Kwaresma, huku akisema kuwa wao wana ndoa ya mseto.
Mwanakwetu akiwa katika dawati ili akaendelea kumkumbuka Kadinali Pengo akiwa anafika tu Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam akiwa ana nguvu zake miaka 1990 huku Kadinali Laurean Rugambwa akiwa mzee sana na kila alipokuwa akifika Parokia ya Mbagala hasa pale Kituo cha Kiroho Mbagala, Kadinali Rugambwa alikuwa katika gari dogo likiendesha na masista.
Suala hili la ndoa ya mseto ya huyu dada katika kibanda cha fundi likamteka Mwanakwetu na kukumbuka namna Jimbo Katoliki la Dar es Salaam llivyokuwa linafungisha ndoa za mseto na kutoa ubatizo kwa watoto ambao wazazi wao hawakuwa pamoja , huku katika ndao za mseto waamini wale Wakatoliki walibaki na imani yao.
“…hoja ikiwa unampoteza au unabaki na mmoja? Ni heri ubaki na mmoja, baadaye Bwana Yesu anaweza kuambulia watoto…kuliko kumpoteza kabisa.”
Mwanakwetu akakumbuka Kadinali Pengo alisaidia sana ili jambo kwa maeneo ya Pwani ya Tanzania huku Mwanakwetu akishiriki ibada kadhaa za Misa za Ndoa za Mseto kama mwanamme ni mkatoliki alikomunika katika ibada hiyo ya misa yeye tu na mwanamke ni mkatoliki alikomunika yeye tu.
“…kwa maana yule anayebaki katika ndoa ya mseto anakuwa mmisionari, akiwa makini katika maisha yake anaweza kuifikisha Injili pahala ambapo ilikuwa ngumu kufika...maana yupo uwanja wa vita…”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yupo kwa fundi na simu yake inatengenezwa, akilini mwake likamjia na jambo lingine:
“Ukoo wa mwaka wa 1880 Baba Mpagani mama Mpagani, wanazaliwa watoto wapagani watupu, ukoo unakwenda wanakuja Wamisionari wanawabatizwa hadi miaka mwaka 1920 vijana wanakuwa wakubwa wanaoana wanazaa watoto wa miaka 1940-1955 hawa ndiyo akina Porcarp Kadinali Pengo huu uzao unabatizwa, hawa watoto wanasoma elimu wanakwenda hadi ya 1970-1980 wengine ni mapadri/wachungaji na wengine wanakwenda katika maisha ya ndoa wanakutana na wenzao waliosoma nao na kazini au vyuoni wanapendana wanaoana, hawa ndiyo wazazi wa akina Mwanakwetu- hapa unakutana huyu Mkatoliki yule Mwangilikana, huyu Mlutheri yule Moraviani, Huyu Mwangilikana huyu Mkatoliki wanafunga ndoa mseto. Wanaanza maisha wanazaa watoto katika mafungu mafungo wapo watakuwa Wakatoliki wapo watakuwa Anglikana na wapo watakuwa Walutheri wapo watakuwa Moraviani, watoto wanazaliwa wanakuwa wakubwa miaka ya 2000 na wao wanazaa watoto wanasoma wanafika mwaka wa 2026 wanakuwa wakubwa wanakutana wenza wao wanafunga ndoa wanazaa watoto maisha yanaendelea…”
Mwanakwetu yupo katika dawati la fundi…gafla akaambiwa simu yako imekamilika, hapa hapa alinyanyuka katika dawati na kwenda kuichukua simu na kubeba begi lake hadi kwake na alipofika kwake ndipo akakumbuka kuyatayarisha makala haya unayoyasoma msomaji wake.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika Porcarp Kadinali Pengo amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 81, huyu ni babu na huyu ni Baba kwa akina Mwanakwetu. Mwanakwetu anasema kuwa Kadinali Pengo alikuwa Kadinali aliyeweza kutambua changamoto za ndoa nyingi katika Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, awali mambo yalikuwa magumu, wapo vijana waliokataliwa kujiunga na mafunzo ya Upadri kisa wazazi wao hawakuwa pamoja.
Kwa hakika Kadinali Pengo alifahamu umuhimu wa wazazi kuwa pamoja, japokuwa wanatafautiana imani, mtoto anahitaji mahitaji mengi, ikiwamo malazi, mavazi, elimu na kadhaliki wazazi wakiwa wanawasiliana vizuri haya mambo yanapatikana kwa wepesi huku dini ikitumika kuwa daraja la kuwaunganisha na siyo kuwatenganisha.
Msomaji wangu niweke wazi hawa watoto ambao ni mazao ya ndoa za mseto ndiyo akina Mwanakwetu , hapa unakutana na Baba Mkatoliki Mama Muangalikana. Huyu Bwana Mkubwa Yesu Kristo anatupenda sana sote , hata wale wanaozaliwa na mzazi mmoja peke yake na huyu Bwna Mkubwa Yesu Kristo kaja kwa ajili yale wenye madhaifa ambao ni akina Mwanakwetu.
Katik hali hii Mwanakwetu anakumbuka hili:
“…Baba Yetu Uliye Mbinguni ya Kanisani kwa mama inasema Utupe Riziki Yetu Ya Kila Siku…lakini Baba Yetu Uliye Mbinguni Ya Kanisa la Baba inasema Utupe Mkate Wetu wa Kila Siku…zote hizo si Baba Yetu Uliye Mbinguni ileile .”
Mwanakwetu anasema wazi kuwa Kadinali Pengo ubini wa ukoo wake ni PENGO ambalo lilikuwa linatengeneza njia pahala palipokuwa vigumu kuwepo njia katika maisha ya ndoa ya familia nyingi ambapo maisha ya ndoa ni magumu sana yanahitaji neema kubwa kutoka kwa Mungu huku viongozi wa dini tukiombea kuwa na hekima ya Bwana.
Mwanakwetu anatoa pole kwa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa kufiwa na Kiongozi huyu ambaye alimpatia Kipaimara Mwanakwetu Parokia ya Mbagala mwaka 1993, Pia Mwanakwetu anatoa pole Kanisa Katoliki la Tanzania Kumpoteza Kadinali wao, Mwanakwetu anatoa pole kwa Kanisa Katoliki Ulimwenguni kwa msiba huu na pia Mwanakwetu anatoa pole kwa Wafipa wote wa Sumbawanga kwa kufiwa na ndugu yao.
“Raha ya Milele Uumpe Ee Bwana na Mwanga wa Milele Umuangazie, apumzike kwa Amani –Amina.”
Mwanakwetu Upo?Kumbuka:
“Buriani Polcarp Kadinali Pengo.”
0717649257







Post a Comment