Adeladius Makwega-MBAGALA.
Mwishoni mwa Januari 2026 vyombo va habari vya Tanzania vimeripoti kifo cha Kamishna Msaidizi wa Polisi Mstaafu Michael Kamuhanda, aliyestaafu utumishi wa Jeshi la Polisi Tanzania mwaka 2014, alifariki dunia Januari 29, 2026, alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Kanda Bugando, mkoani Mwanza. Kutokana na kifo hiki mwanzoni Mwanakwetu hakukitilia maanani sana kutokana na mitandao ya Kijamii kuutazama msiba huu kwa namna mbaya na hili linatokana na hali ya matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata, huku Jeshi la Polisi Tanzania likiwa na mzigo wa lawama. Katika hali ya kushangaza kidogo katikati ya Januari, 2026 Mwanakwetu alitayarisha Makala ya sauti, video na maandishi iliyopewa jina Afande RCO Acha Gere . Katika aya mojawapo ya mwisho mwisho alimtaja Afande Advocate Nyombi ambaye aliwahi kuwa RPC wa Iringa na baadaye RPC wa Mbeya akiwa askari mwenye mahusiano mazuri sana na watu wa Iringa wakati huo.
“Hata mauwaji wa mwanahabari Daudi Mwangosi yalifanyika mara baada ya Afande Nyombi kuhamishiwa Mbeya huku Iringa ikipata RPC Mpya. Mauwaji ya Daudi Mwangosi ilikuwa vigumu kutokea kipindi cha Afande Advocate Nyombi.”
Katika makala haya ya Afande RCO Usione Gere, Mwanakwetu alikwepa kumtaja huyu RPC Mpya baada ya Afande Advocate Nyombi kuondoka mkoani Iringa, kutolitaja jina la RPC Mpya kulikuwa na sababu nyingi mojwapo akifahamu kuwa RPC Mpya wa Iringa baada ya Afande Advocate Nyimbo alikuwa ni Afande Michael Kamuhanda na wakati huo ndipo Daudi Mwangosi aliuwawa huku Afande Kamuhanda akiwa mita chache tukio lilipotokea. Mwanakwetu akitambua kuwa UPOLISI unahitaji ukakamavu lakini ukakamavu wa wewe uliye polisi siyo ukakamavu wa familia nzima, hivyo jina la ndugu mmoja linapotajwa kwa mabaya katika jambo lolote lile linaacha kidonda kikubwa cha ndugu, familia na hata ukoo mzima. Maana punde mauwaji ya Daudi Mwangosi yalipotokea Mwanakwetu anakumbuka baadhi ya watu walimuhusisha afande Michael Kamuhanda na nasaba na Katibu Mkuu Wizara ya Habari ya wakati huo ndugu Sethi Kamuhanda bila ya kufahamu kama walikuwa ndugu kweli au la.
“Mbona Sethi Kamuhanda mahusiano yake na wafanyakazi WIZARANI ni mazuri? Kwanini Afande Michael Kamuhanda anasemwa vibaya hadi kuhusishwa na mauwaji ya Daudi Mwangosi Septemba 2, 2012?”
Wakati huo kesi ya mauwaji ya Daudi Mwangosi ilikuwa ndiyo ipo katika hatua za uchunguzi huku Jaji mstaafu, Mheshimiwa Amir Manento katika uchunguzi wake alisema kuwa mkusanyiko wa CHADEMA haukuwa kinyume cha sheria na kwamba kwa kuutangaza kuwa ni haramu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa (RPC), Kamishna Msaidizi wa Polisi, Michael Kamuhanda, alitenda kinyume cha sheria yeye mwenyewe.
“Amri aliyotoa Afande Michael Kamuhanda ilikuwa kinyume cha sheria kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka ya kutoa amri hiyo. Hayo ni matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora,”
Jaji Mstaafu Manento alisoma muhtasari wa matokeo ya tume yake kwa vyombo vya habari Jumatano, Oktoba 10, 2012. Huku tamati ya kesi hii kijana Picificus Simon ambaye alikuwa askari FFU ndie pekee aliyetiwa hatiani kwa mauwaji wa Daudi Mwangosi na kufungwa miaka 15 jela katika shauri lililoamuliwa na Jaji Paulo Kihwele ambaye sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto–IJA.
Kikubwa Afande Michael Kamuhanda amefariki dunia Januari 29, 2026 huku Daudi Mwangsi alifariki dunia Septemba 2, 2012. Daudi Mwangosi alifariki akiwa kazini kama mwanahabari akiripoti mkutano wa CHADEMA huku akiwa pia ni Mwenyekiti wa Kilabu ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Iringa Afande Kamuhanda amefariki dunia miaka 11 baada ya kustaafu salama kazi yake na miaka 13 baada ya kifo cha Daudi Mwangosi.
Kwa heshima ya wasomaji wa Mwanakwetu naomba nitaje mambo makubwa matatu ya Daudi Mwangosi ambayo yalimgusa moja kwa moja Mwanakwetu akiwa mkoani Iringa wakati huo.
“Mwaka wa 2005 Mkuu wa shule ya Sekondari Isimani Tarafani wakati huo Bi Dainess Semuyala alimpigia simu Mwanakwetu na kumwambia kuwa kuna barua yake hapa kwa karani wa shule hii ya umma aende akaichukue. Mwanakwetu alitoka Iringa Mjini akiwa mwanachuo wa chuo Kikuu cha Tumaini Iringa na kwenda kuichukua barua hii na punde alipofika kwa karani barua hiyo ilikuwa na maudhi haya.
…sisi wanachama wa Kilabu ya Wanahabari Iringa tumeona mchango wako katika tasnia ya habari iwe katika redio na magazetini ,hivyo basi hivyo Iringa Press Club inakukaribisha ujiunge na kilabu yetu japokuwa wewe bado ni wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa, upatapo barua hii naomba utembelee ofisi zetu zilizopo Iringa Mjini ili tuwe pamoja katika tasnia ya habari nchini Tanzania Asante sana Daudi Mwangosi Iringa Press Club.”
Mwanakwetu alitemblea ofisi ya Iringa Press Club ambayo ilikuwa jirani na Benki ya Posta Iringa Mjini jirani na Manispaa ya Iringa, hapo ndipo aliifahamu Iringa Press Club na wanahabari wake wengi wakiwamo Daudi Mwangosi , Frank Leonard, Friday Simbaya, Eliasa Ally, Majjid Mjengwa, Temmy Mahondo, Rose Majani, Mpoki Mwakapisu na wengine wengi.
Mwaka wa 2006 mvua kubwa zilinyesha Mkoani Iringa huku eneo la Ipogoro likajaa maji hata Stendi ya Mabasi ya Ipogoro ikawa imefunikwa na maji Mwanakwetu na wahabari kadhaa walishuka hadi Ipogoro madhumuni ni kuandika habari hiyo na kweli kazi hii ilifanyika vizuri na mwisho wa siku wakatafuta usafiri ukawa mgumu kurudi Iringa Mjini, hivyo basi wakatembwa KWA MGUU hadi wakawa wanaanza kuupanda huu mlima kwa kuelekea Iringa Mjini nia waende kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa wakati huo Bi Teresia Mbano ambaye angeweza kutoa chochote kitu lakini kueleza upande wa serikali juu ya utatuzi baada ya mafuriko haya. Njiani ikaja gari la Polisi Defender Land Rover kwa mbali , kwa mbali hivi .
Waandishi wa habari kadhaa wanatembea kwa miguu hawana kitu. Blandina Semaganga akasema maneno haya,
“Defender hiyo ya Polisi inakuja , Kaka Daudi Mwangosi wewe unafahamiana nao vizuri ipige mkono hiyo defender tupande.”
Daudi Mwangosi akasema haya ni magari yetu ngoja nifanye hivyo akaipiga mkono Defender hiyo Polisi wakasimamisha gari yao na kuwapakia wanahabari hao hadi Kituo cha Kati kisha wanahabari hao kushuka na kwenda kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Bi Mbano. Hapa Teresia Mbano alishapigiwa simu na Daudi Mwangosi juu ya uwepo wake na Meya wa Iringa Mjini wakati huo Mtoto Said Abdallah Mwamwindi
“Tukapokelewa Ofisini kwa Bi Mbano vizuri, tukawahoji na namna ya kuwasaidia wananchi wa Ipogolo. Tulipomaliza Bi Mbano akatoa shilling 30,000/= kwa mwanahabari wote tuliokuwapo na kisha kwenda kuandika habari hiyo.”
Jambo la tatu na mwisho lilikuwa ni siku ya Septemba 2, 2012 siku Daudi Mwangosi anauwawa:
“Siku hii Mwanakwetu alikuwepo Mkoani Iringa ambapo mkewe alikuwa anamalizia Shahada yake ya Uzamili ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Ruaha (Saint Augustine ) Iringa huku mahafali ya mama huyu yalikuwa jirani. Siku hii Mwanakwetu hakutoka katika makazi yao pale TRM waliyokuwa wakiishi maana Iringa Mjini kulikuwa na Mvua, hivyo yeye aliamua kuandika makala juu ya Shule za Kata katika Gazeti la Kwanza Jamii ambapo mhariri wake alikuwa ni Simon Mkina ambaye awali alikuwa THISDAY &KULIKONI na hata MAWIO. Jioni ya siku hii ndipo Mwanakwetu alipojulishwa kupitia kwa mwanahabari Greson Mgoi miongoni mwa wanahabari wa Kwanza Jamii wakati huo kuwa Daudi Mwangosi amefariki dunia katika ghasia.”
Haya msomaji wangu Mwanakweu amejaribu tu kuyakumbuka kwa uchache mara baada ya kusikia Afande Michael Kamuhanda amefariki dunia maana sisi wanahabari unapomtaja Afande Michael Kamuhanda tunamkumbuka ndugu yetu Daudi Mwana Mwandosi.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Anapotajwa Michael Kamuhanda Tunamkumbuka Daudi Mwangosi.”
0717649257
.gif)



Post a Comment