Anafanyiwa Upasuaji wa Henia

 




Adeladius Makwega-MBAGALA

Ni majira ya alasiri ya saa 9.29 ya Februari 18, 2026, Mwanakwetu amefika nyumbani kwake ili akasali Ibada ya Jumatano ya Majivu, ile anaingia tu ndani kwake anapokea simu kutoka kazini kwake na mpigaji akiagiza haya:

“Makwega upo ofisini? Na hata kama umefika nyumba rudi hapa ofisini haraka kuna ugeni …”

Kweli Mwanakwetu alirudi ofisini ili kuifanya kazi hiyo. Kazi ikafanywa tangu ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na baadaye Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere Kwaangwa Musoma Mjini.

Kazi hii ilifanyika tangu saa 10 ya jioni hadi saa mbili usiku wa Februari 18, 2026 na kisha Mwanakwetu kutoka nje ya Hospitali hii ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuipanda Boda boda ili kurudi kwake.

Mwanakwetu akiwa amepanda bodaboda hii majira ya usiku mvua ikinyesha akitoka kazini alimuuliza maswali kadhaa, naye bodaboda huyu alijitambulisha kwa majina mawili akiitwa Davidi Chilima ambaye ni Mjita akifanya kazi ya bodaboda Musoma Mjini.

“Mzee ratiba yangu huwa ninaamka asubuhi na mapema nafanya kazi hadi saa 4 ya asubuhi, kisha narudi nyumbani, naoga kisha nakwenda shuleni, ninasoma masomo ya kidato cha nne tangu saa nne hadi saa kumi jioni, narudi nyumbani, nakula naoga, nachukua bodaboda yangu narudi hapa Kwaangwa kubeba abiria hadi saa 5 ya usiku , hapa bado saa tatu nirudi nyumbani.”

Kumbuka Mwanakwetu anarudi kazini alipokuwa akifanya kazi tangu jioni na usiku huu.

“Hapa mimi nabeba sana abiria wanaokuja kupata huduma za tiba ambao ni wagongwa, safari nyingi ninazo fanya ni kutoka Kwaangwa kwenda Hospitali a Manispaa ya Musoma na kurudi ambapo abiria akiwa mmoja ni shilingi 3000 na kurudi hadi 6,000 wakiwa wawili hadi shilingi 6,000 na mara mbili ni shilingi 12,000 lakini hapa nabeba wagonjwa na wengine hawana pesa hivyo hivyo hauwezi kumkataa mgonjwa maana hata mimi ni mgonjwa kwa kesho. Shida ya Hospitali hii ni wagonjwa wengi wakipata huduma wanaambiwa wakapige X rays Manispaa ya Musoma hivyo ndiyo maana safari hizi ni nyingi. Hapa X rays yao haijaanza kufanya kazi. Tena na hata maiti nimeshuhudia mara kadhaa mtu akifariki maiti inabebwa na kukimbizwa Hopsitali ya Manispaa kwa kutumia gari ya wagonjwa, lakini mzee hii hospitali ikikamilika itakuwa msaada sana.”

Mwanakwetu alifika kwake na kuagana na Davidi Chilima bila ya ndugu huyu kujua kuwa hata Mwanakwetu alikuwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara Afya Dkt Seif Shekalage ambaye alifika hapo kukagua hali ya ujenzi wa Hospitali hii unaendeleaje .

Mwanakwetu alikumbuka awali Dkt Shekalage akipokelewa Katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi alisema kuwa Hospitali ya Kwaangwa imetengewa karibu Bilioni 10 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo hadi sasa wameshatumia karibu bilioni mbili tu huku Kanali Mtambi akihimiza Wakandarasi waliopewa kazi wafanye kazi zao ili walipe pesa zao kwa wakati.

Mwanakwetu alikumbuka kuwa Katibu Mkuu Dkt. Shekalagejioni hii alitembelea Hospitali hii na kukagua ujenzi wake na huku akiongea na wafanyakazi .

 

Baadaye Dkt. Seif Shekalage alitoa maagizo haya ya Serikali kwa wizara yake na Uongozi wa Hospitali hii ya Rufaa.

“Siyo jambo zuri kuwasumbua wagonjwa wafunge safari kwenda kupiga X rays Hospitali ya Manispaa ya Musoma wakati hii ni Hospitali ya Rufaa naagiza viongozi wote walio chini yangu kikosi cha wataalamu wa Wizara ya Afya waliopo katika ziara hii waangalie shida ni nini na kisha muushauri cha kufanya mapema sana.”

Awali katika ziara hii Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mara Dominicus Lusasi ndiye aliyeambata na kiongozi huyu hatua kwa hatua katika vikao vyote vya nje na ndani hadi Katibu Mkuu anamaliza ziara yake saa 2 ya usiku ya Februari 18, 2026 hapa hapa hadi Mwanakwetu anakutana na yule Bodaboda ndugu Davidi Chilima ambapo yale malalamiko aliyotaja ndiyo yalikuwa yanafanyiwa kazi na Serikali.

Mwanakwetu alipofika kwake ndipo akaamua kuyaandika makala haya.

Wakati yanaandikwa makala haya ikabishwa hodi mlangoni, Mwanakwetu kisha kuambiwa maneno haya.

“Kaka njoo ufunge mlango, mimi leo silali kwangu, nakwenda kulala nyumbani kwa rafiki yangu maana mumewe kesho anafanyiwa upasuaji wa henia katika Hospitali ya Kwaangwa hivyo basi watoto wao hawapo wenyewe bali kuna jamii kubwa ya hawa wao wamebaki wenyewe.”

Mwanakwetu alikwenda kuufunga mlango huu. Mwanakwetu alimalizia kuyatayarisha haya makala majira ya saa tano ya usiku.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere hapa Mkoani Mara ni muhimu sana kwa kulinda afya za Watanzania wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa angalia hivi visa viwili kile cha jirani wa Mwanakwetu anayefanyiwa upasuaji wa henia na pia huyu dereva wa bodaboda huku serikali ikipambana kuboresha hali ya hospitali hii.Kwa hakika lazima juhudi ziongezwe ili hospitali hii iwe bora, huduma ziwe bora nia ni kuboresha maisha ya Watanzania.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Baba Yao Anafanyiwa Upasuaji wa Henia.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.om

0717649257

 

0/Post a Comment/Comments