Amepata Ajali Ya Kisiasa Katikati ya Taa ya hatari

 


Adeladius Makwega-MBAGALA.

“Hana mvuto wowote wa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje; mtu huyu anapoteza pakubwa katika masuala ya taifa na hali hiyo imefungamana sana na urais. Kwa kweli Chinua Achebe angekuwepo angetumbia ‘Kichwa chake hakiko sawa.’ Huwezi kuwadharau wananchi wenzako na kutaka kuharibu au kuichafua International Criminal Court, Vatican City, African Union, pamoja na ulimwengu kwa ujumla. Hatuko pale kuonesha sura zetu—ni aibu kubwa...”

Haya yalikuwa maoni ya Raphael Ondengo katika mojawapo wa makala za Mwanakwetu zilizokuwa zikijadili juu ya nafasi ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania ndugu Mahamoud Thabiti Kombo. Hivyo ndivyo Waziri wetu anavyopimwa na ndugu Andengo.

Maoni mengine yalikuwa haya :

“Na hata bado amini usiamini Mahamoudu Thabiti Kombo ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa mwaka 2030 tukijaaliwa. Asiyependa ahame nchi. Tanzania itatawaliwa na Wazanzibar mpaka mwisho wa Dunia tukijaaliwa.”

Haya yakiwa maoni ya ndugu anayeitwa Tanzania Pemba na huku maoni zaidi yaliongezeka baada ya Mwanakwetu kutoa makala tisa; tatu za maandishi, tatu za sauti na tatu za video juu ya Mheshimiwa Mahamoud Thabiti Kombo ambaye ndiye Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania.

Msomaji wangu maoni ni mengi lakini nimeamua kukupitisha katika maoni mawili ya ndugu Raphael Andengo na ndugu wa pili anayejiita Tanzania Pemba baada ya makala za Mwanakwetu kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

 

Mwanakwetu aliweka bayana kuwa Waziri Mahmoud Thabiti Kombo ambaye ni miongni mwa watoto wa Marehemu Thabit Kombo kwa ishara za Mwanakwetu anaona ndiyo amefikia mwisho wa kushamiri kisiasa katika taifa la Tanzania na Mwanakwetu anaona Mahamoud hawezi kupata nafasi nyingine kubwa tena na anguko la Mahamoud Thabiti Kombo linafanana na anguko la Ahmed Hassan Diria enzi za Rais Mwinyi miaka ya 1990.

 

Historia inadokeza haya:

“Kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Ahmed Hassan Diria aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa eneo la Pemba, alibaki katika nafasi hiyo hadi mwaka 1965, alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Tanzania, hapa alikuwa Balozi wa Tanzania kwanza nchini Kongo mwaka 1970 hadi 1972; Kamishna Mkuu huko New Delhi, India kuanzia 1971 hadi 1978; baadaye Baloziwa Tanzania nchini Japani kuanzia 1979 hadi 1984; na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani mwaka 1984. Baada ya kuhudumu katika Balozi kadhaa za Tanzania alirejea Tanzania na kuwa mbunge wa Raha Leo ambapo alishika nyadhifa mbalimbali za uwaziri. Mwaka 1989 alijiunga na Baraza la Mawaziri la Tanzania, akihudumu kama Waziri huku mwaka 1990 hadi 1993 Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awali alikuwa Waziri wa Habari na Utangazaji ambapo kipindi hiki ndipo sakata la OIC linaibuka na kumpoteza Ahmed Hassan Diria na John Samweli Malecela katika siasa za Tanzania.”

Msomaji wangu nakuomba nikuongezee jambo moja, katika jambo hili moja yako mawili kama mheshimiwa mwenyewe Mahamoud Thabiti Kombo kama angesema neno juu ya hoja hizi za Mwanakwetu hapa angelisema jambo pacha la hili moja lakini kwa kuwa Mahamoud Thabiti Kombo Kaka yake Mwanakwetu amekaa kimya na Mwanakwetu analiweka kibindoni jambo hilo pacha lakini analisema jambo moja tu. Ili Mtanzania aweze kuwa Rais wa Jamhuri a Muungano wa Tanzania lazima pande hizi mbili za Muungano kusiwe na tuhuma yoyote ile inayooanishwa na kiongozi yake mathalani kuonekana kuukandamiza upande mmoja, jina lako likiwa katika mapendekezo na upande mmoja ukikulalamikia waziwazi ili kulinda Muungano lazima wewe unayelalamikiwa ukae kando ili kulinda umoja wa taifa .

“Salim Ahmed Salim wakati Nyerere anaondoka mwaka 1985 Upande wa Unguja ulikuwa unamkataa kabisa, japokuwa huku Tanganyika alikuwa anapendwa. Mwalimu akasalimu amri na hata mwaka 2005 akina Jakaya Kikwete walijua kuwa tishio ni Salim Ahmed Salim, hapa fitina zilipigwa na hadi mwisho Jakaya Kikwete akapenya.”

Kigezo hiki cha lawama nyingi za upande mmoja ndicho kinamzamisha Mahamoud Thabiti Kombo hata kujaribu kuutafuta Urais wa Zanzibar kwake itakuwa ngumu, upande wa Tanganyika ndani chama watu watakuwa na yao ya moyoni. Watu kwa sasa wanakaa kimya lakini ikifika wakati wa mambo yamotomoto yote haya yataweka hadharani. Mwanakwetu anasisitiza kuwa ndugu yake Mahamoud Thabiti Kombo sasa ndiyo amefika ukingoni mwa siasa za Tanzania, anaweza akabaki kama mbunge tu na hata huu Uwaziri wa Mambo ya Kigeni mwezake Ahmed Hassan Diria alikaa muda mrefu kidogo lakini kwa Kombo kipindi chake ni kidogo sana maana sababu kila mmoja anaifahamu.Ndiyo Kusema Mahamoud Thabiti Kombo amepata Ajali ya Kisiasa Katika  ya Taa ya Hatari.

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Amepata Ajali ya Kisiasa Katikati ya Taa ya hatari.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


















 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments