TUNZA WANAO LAKINI USITARAJIE WAO MSAADA

Adeladius Makwega-MBAGALA

“Yaani kaka wanawake ni hatari sana, nimejenga nyumba zangu tano nikasema mambo ya kupigiwa simu mara karo za watoto mara nini staki, nikaamua mke wangu uwe unakusanya kodi, tembelea nyumba zote, chukua majina ya wapangaji wote kisha kusanya kodi. Zoezi hili limefanyika vizuri sasa mke wangu anakusanya kodi huku pesa hizo pia zikitumika katika matumizi mengine ya familia hapa nyumbani kwangu.”

Jamaa wawili wanaume wanatembea barabarani kwa miguu wakitoka kazini huku wakiongea maisha ya familia na changamoto zake. Jamaa aliyeshika usukani wa mazungumzo akasema:

“Jamaa huyu mwenye nyumba zake tano siku kaishiwa pesa, hana kitu, akapiga simu kwa mkewe akimwambia mke wangu leo sina pesa na sijakula tangu asubuhi hapa nimerudi nyumbani naomba niingizie laki moja nitairudisha.”

Yule mama akajibu sawa, sasa kumbe wakati simu hii inaongea ilikuwa katika sauti ya juu mtoto wao wa kiume wa mwisho mwenye umri kama wa miaka 12 akasema:

“Mama hiyo pesa yako baba hairudishi.”

Huyu baba hakuweza kuyasikia vizuri maneno ya mwanawe lakini mama mtu aliyekuwa jitana alisikia kisha kamtaja jina mtoto wake alafu akamwambia mumewe unasikia mwanao hapa anasema Mama hiyo pesa yako hairudi. Huyu baba akacheka moyoni kisha kukaa zake kimya huku akitafakari kumbe kutoa ridhaa ya huyu mama akusanye kodi mwanangu ananiona mie lofa? Kumbuka jamaa hawa wawili wapo njiani wanatoka kazini, wanaongea changamoto za maisha ya ndoa . Jamaa wa pili akasema mbona hilo dogo sana ngoja nikusimulie kisa hiki:

“Kuna jamaa yangu anafanya kazi ya kuunganisha intaneti katika taasisi ana kampuni yake inayofanya kazi hizo. Akapata kazi nzuri wakaifanya mpaka wanamaliza alibaki na shilingi milioni 16 sasa akazichukua zile pesa anamwambia mke wangu nakuomba tunza hizi fedha hapa katika biashara yako lakini punde nitakapo zihitaji unipe sasa mimi ngoja niendelee na kazi.  Huyu jamaa akaacha furushi hilo la shilingi milioni 16 na kuondoka zake, jamaa akafanya kazi kama kwa muda wa miezi kama sita kazi ikakamilika na jamaa wengine wakaipenda kazi yao akapata mkataba mwingine kama ule wa awali lakini akaambia aanze kazi akishaanza ndipo ataandika madai yake, kweli akawachkua vijana wake wakaikagua kazi ili kesho yake waanze. Jioni yake kwa mkewe akasema mke wangu naomba zile fedha nikalipea vifaa nimepata kazi nyingine.  Lo salale!Huyu mwanamke akasema yeye hana hata shilingi. Jamaa akapigwa na butwaa hapo hapo akaamua mkewe afunge duka na arudi kwao mara moja.

Kweli huyu Mwanamke akafunga duka na kuondoka zake kwao.Jamaa karudi kwa Baniani akakopa vifaa na kupewa kisha kuendelea na kazi kumbe kuwa ukweni huyu mkewe wakati anaondoka ana ujauzito. Wakati ile kazi ya kufunga intaneti ya pili jamaa ndiyo anakutana na huyu ndugu anayesimulia na kumuueleza vituko vya mkewe, jamaa akasema kama unampenda mkeo na mimba kama ni yako mrudishe uishi naye lakini kwenye biashara na fedha usimuishe kabisa ili kuepusha migogoro. Kweli jamaa alifanya hivyo.”

Msomaji wangu kumbuka hawa jamaa wawili wanatembea majira ya jioni wanarudi nyumbani kwa mguu wakitokea kazini kwao huku simulizi ni za bandika bandua. Jamaa wa kwanza akasimulia kisa kingine.

“Nina kijana wangu namsomesha, sasa nimetafuta karo nimelipa vizuri nikasema sasa nitafute pesa ya nauli na ya matumzi shuleni, hali ikawa mbaya hivyo hadi unafika wakati wa kufungua shule sina pesa. Mama yake kila nilipomwambia mpe mtoto pesa ya nauli na ya matumizi mama mtu anasema yeye hana pesa. Baba mtu akasema basi mwanangu subiri kaa nyumba hadi nitakapopata pesa. Mama alipoambiwa hili akachanganyikiwa akasema inakuwaje hivyo baba akajibu kwa sasa sina lakini juma moja mbele nitampatia kijana wangu fedha na atakwenda shuleni. Mama akasema sawa na mtoto akasema sawa. Baada ya siku moja kijana yule mwanafunzi akatuma ujumbe kwa baba yake akisema baba unajua simu yangu mbovu ukizipata hizo fedha usitume katika simu yangu mtumie mama. Baba yake akajibu sawa kweli baada ya siku mbili ya tatu kabla wiki haijakamilika baba milango ikafunguka akapata pesa akatuma kwa yule mama. Baba akauliza mtoto anaondoka lini? Mama akajibu anaondoka kesho jioni yaania baada ya kupokea fedha baba akasema sasa kabla ya kuondoka shuleni mwambie mwanangu naomba niongee naye maana nimepiga simu yake kijana hapatikani. Mama akajibu yupo bali nimemtuma kazi kidogo akirudi ataongea na wewe.

Siku hii ilipofika mama kila alivyopigiwa simu hapokei na wala mtoto simu yake haikupatikana. Baba akafanya utafiti alibaini kuwa mtoto yule alisharipoti shuleni na mama alimpa mtoto pesa siku ile ile. Baba huyu akawa anajiuliza kwanini hawakuniambia ukweli mapema mimi kama mzazi nijue na nisidanganywe hivi kama kijana akipata ajali njiani watasemaje?”

Kumbuka kisa hiki kinasimuliwa hawa jamaa wanarudi nyumbani ,huyu jamaa mwingine kando akasema:

“Sisi kama wanaume tunapaswa kusomesha watoto wetu vizuri, watoto wapewe huduma zote lakini baba mwenye akili usiweke akilini mwako kuwa ipo siku watoto hao au mama yao watakuja kukusaidia, hili la kusaidiwa jitahidi kama una rasilimali zako jitahidi uwe na rasilimali zako wewe mwenyewe ziwe zinakuingizia pesa, hawa watoto kama Mungu akiwajalia wakiwa na moyo wa kukusaidia sawa lakini kama hawatofanya hivyo wewe usiumize kichwa mshukuru Mungu tu.Wewe kama baba umetimiza wajibu wako.”

Kumbuka jamaa hawa wanarudi nyumbani kwao wakitoka kazini mara kila mmoja alifika kwake na kuingia katika mji wake huku wakiagana kuwa watakutana kesho yake kazini

Mwanakwetu upo? Kumbuka

“Tunza Wanao lakini Usitarajie Wao Msaada.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257










 

0/Post a Comment/Comments