Adeladius Makwega-MBAGALA
“Mnamo mwaka 1934, wamisionari wa Kimenonite walifika Tanganyika (sasa Tanzania), Afrika Mashariki, na kuishi katika eneo la Shirati.
Huku wenyeji wa eneo hili wakitaabika kwa kwa malaria, kuhara damu, na homa za kitropiki hivyo kulihitaji kutumwa mapema kwa timu ya kitabibu katika eneo hili. Chifu wa eneo hilo alisaidia juhudi hizo kwa kujenga vibanda vya kwanza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa. Miundo rahisi ilijengwa na huduma za afya zikaanza kutolewa.
Baada ya ujenzi wa majengo ya kwanza ya kudumu ya hospitali miaka 19 baadaye yaani mwaka 1953 na miaka saba baadaye shule ya mafunzo ya wauguzi ilifunguliwa mwaka 1960. Kufuatia kufunguliwa kwa uwanja wa ndege mwaka 1960, uhusiano wa Shirati na huduma za kitabibu za African Medical and Research Foundation (AMREF) mjini Nairobi uliimarika sana huku siha za watu wa Shirati Rorya na Mara nzima ziliimarika huku Kliniki Tembezi ikiwahudumia watu wa eneo hili ambapo huduma hizi zilikuwa mara sita kwa mwaka mzima.”
Msomaji wangu haya ni maelezo ya Kanisa la Menonite Tanzania, Dayosi ya Shirati inayoongozwa na Askofu John Ojalla ambapo Mwanakwetu alifika Januari 31, 2026 katika Hospitali hii inayotoa huduma kwa watu karibu 354,490 kwa hesabu ya watu ya mwaka wa 2022 huku wanawake ni 184,572 na wanaume 169,913.
Huku Wilaya ya Rorya inayoongozwa na Dkt. Khalifan Haule inayokadiliwa kuwa na ongezeko kubwa la watu karibu 100,000 tangu sensa ya mwaka wa 2012 na ile ya 2022.
Hapa Shirati kunafanyika shughuli ya kukabidhi vifaa vya tiba kadhaa kutoka benki ya NMB na shughuli hii ilifunguliwa kwa sala na Askofu Mkuu wa Kanisa la Menonite Tanzania Nelson Kisare huku aliwapongeza NMB kwa kuwa benki rafiki kwa Watanzania na kuwashukuru NMB kwa kuwa na moyo wa upendo kwa Hospitali ya Shirati kwa kutoa mashine ya kupumulia na kuwaongezea joto watoto wanaozaliwa njiti na kutoa Inkubeta kadhaa:
“Kwa niaba ya Kanisa letu nasema NMB mmepanda mbegu ili izae matunda mema na sisi tuliyopokea tutavitunza vizuri.”
Akizungumzia Hospitali za Kanisa popote pale duniani Askofu Kisare alisema zimejaa UPENDO na HURUMA kwa wagonjwa.
“Mgonjwa anakutana na Yesu Kristo tangu getini, kwa walinzi, pale mapokezi, pale kwa daktari , pale kwa muuguzi , pale wodini akilazwa na hadi siku anatoka hospitalini.”
Akimalizia maelezo yake Baba Askofu Nelson Kisare alisema kuwa yeye ndiye mwanzilishi wa kwanza wa Kitengo cha Hazina cha Benki cha NMB ambayo ndiyo benki inayofanya vizuri kwa sasa nchini Tanzania.
“Benki yetu inapata faida kubwa huku na sisi tukikumbuka kurudisha faida hiyo kwa Watanzania katika elimu, afya na sekta zingine nchi nzima huku mkoa wa Mara ni wanufaika wa kwanza na leo hii nimekabidhi inkubeta nane mashuka 20 vitanda 20, magodoro 20, na mashuka 400, madawati, mbao na mabati kadhaa ambapo Mkoa wa Mara umepokea vifaa vya karibu shilingi milioni 230 ambapo ni sehemu ya shilingi bilioni 23 ya faida yake.”
Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi, Mkuu wa Wilaya ya Rorya Dkt. Khalifan Haule alisema kwamba anawapongeza sana NMB kwa moyo huo huku akiwaomba taasisi zingine ziige mfano kwa NMB.
“Serikali inawashukuru sana NMB kwa moyo huu. Pia nalipongeza Kanisa la Menonite Tanzania kwa kutoa huduma kadhaa kwa jamii na kuendelea kushirikiana na Serikali katika huduma kadhaa za wananchi.”
Dkt Haule alisema kuwa Kanali Mtambi kamwambia aseme kuwa Vifaa Hivyo Amevipokea kwa Mikono Miwili.
Wakati haya yakiendelea hapa Rorya Mkoani Mara hali ya hewa ya Mji wa Shirati ni nyuzi joto 27 ,unyevunyevu ni wa asilimia 10, ujirani na mvua ni asilimia 68 na upepo ukivuma kwa KM 11 kwa saa.
Mwanakwetu Upo?Kumbuka:
“Tunapokea Misaada ya NMB Kwa Mikono Miwili.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257


Post a Comment