TANZANIA INAVYOJIKONGOJA KILIMO CHA UMWAGILIAJI

 




Adeladius Makwega-Musoma MARA

Hii ni Ijumaa ya Januari 9, 2026 Mkuu wa Mkoa wa Mara yu ofisini kwake, mara anaupokea ugeni wa Waziri Mdogo wa Kilimo wa Tanzania David Silinde akiwa na maafisa kadhaa wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara yake. Mkuu wa Mkoa wa Mara alianza mazungumzo yake kwa kugusia kilimo cha umwagiliaji huku akinadi kuwa hiki ni kilimo cha uhakika maana Mkoa wa Mara Ziwa Victoria lipo kila kona huko akiomba Wizara ya Kilimo isaidie hili.

“Mathalani Bonde la Bungwema halijatumika vizuri kwa muda mrefu na hata kuna maeneo ya Bonde la Mto Mara pia hayatumika vizuri, wapo watu walitamani kulima miwa na kufungua kiwanda cha sukari na walitaka kuwashirikisha wananchi walime miwa, jamaa hawa mmoja kutoka Kenya na mwingine kutoka Kenya mwnye asili ya Bulgaria nia ni kuweka kiwanda cha miwa, haya nayaweka mezani kwenu najua yameshafika huko lakini naomba muyafanyie kazi haraka.”

Mara baada ya maelezo haya Waziri Mdogo wa Kilimo wa Tanzania alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa mapokezo mazuri na kumpongeza kwa kazi nzuri anayofanya hapa Mkoani Mara tangu aungoze mkoa huu, kisha kuagana naye kuelekea ziarani.

Waziri Silinde alitembelea miradi miwili, mradi wa mwisho ulikuwa ni Bonde la Bugwema ambapo Mamlaka ya Kilimo inamiliki eneo hili.

Kwanza wananchi walitoa malalamiko kadhaa ya kusumbuliwa, kupigwa na kuharibiwa mazao yao na Mamlaka ya Kilimo Tanzania huku wakiomba hata kama serikali inatekeleza miradi yake ni lazima itoe taarifa kwa wananchi mapema maana ardhi ya Bugwema ni mali ya Watanzania na Wana wa Bugwema ni sehemu ya Tanzania.

“Hiyo Bodi ya Pamba imekuwa hodari wa kubadilisha majina, leo Bodi ya Pamba, kesho Mamlaka ya Pamba watu wale wale tabia zile zile-mnaweka mvinyo mpya katika chupa ya zamani. Hili eneo ni letu tangu mwaka 1967 na siyo mwaka 1974 Mwalimu Nyerere alisisitiza kilimo cha umwagiliaji huku akisema ili Watanzania tuendelee tunahitaji mambo manne: ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Kwa sasa watu wapo lakini mambo matatu yaliyosalia hayako sawa mathalani ardhi ndiyo hiyo Mamlaka ya Pamba inatuyumbisha na hayo mengine hali ndiyo maututi, sasa tunafanyaje?

Mawaziri Wakuu wote tanga Sokoine, Warioba na Salimu Ahmed Salimu walitulinda kwa hili la Bugwema kwa nini sasa mambo yamebadilika?”

Haya yalikuwa ya mkazi mmoja wa Bugwema mbele ya Waziri Mdogo.

 

Waziri Mdogo wa Kilimo alifanya mawasiliano na Waziri wa Kilimo wa Taifa hili Daniel Chongolo ili kupata mwongozo wa namna ya kulitatua jambo hili la Bugwema na kisha kusema haya:

“Tunafeli kwa sababu kilimo tunachokitegemea ni cha mvua, hata Mamlaka ya Pamba imeshindwa kulima vizuri, mvua zilipokuja. Sasa dunia nzima haitegemei kilimo cha mvua sasa ni kilimo cha umwagiliaji. Ukiweka miundombinu ya kumwagilia utavuna tuu, hii ndiyo shabaha ya serikali ya Tanzania…

Wizara yangu imefanya upembuzi yakinifu kwa mabonde yote 22 na hata Bonde la Bugweni ni miongoni mwayo na mwezi wa pili mtaanza kulima mwaka mzima.”

Awali akizindua Programu ya Umwagiliaji nchi nzima kwa wakulima wa Musoma Mjini ambao walipata eneo Musoma Vijijini eneo la Etaro, Naibu Waziri wa Kilimo alisema wakulima wote watawezeshwa ili waweze kufikia shabaha ya kulima kiimo cha uwagiliaji ambapo mikoa 15, Majimbo 65 ekari 8000 na kwa wakulima zaidi ya 4000 watanufaika na mpango wa kilimo cha umwagiliaji wa kupewa zana za kisasa ambapo Kijiji Etaro zimefika ili Watanzania waache kulima kilimo cha kutegemea mvua.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kulingana na takwimu za taifa hili yakadiliwa kuwa asilimia 75 ya Watanzania ni wakulima huku asilimia 4.6 tu ndiyo wanaotumia kilimo cha umwagiliaji zana hafifu, nayo Moroko, Afrika ya Kusini na Misri ndiyo mataifa pekee yanayofanya vizuri katika kilimo cha umwagiliaji na cha kuchekesha Misri wanatumia maji ya Mto Nile yanayotokea Ziwa Victoria lililopo Kenya Uganda na Tanzania ambapo kwa Tanzania kilimo cha umwagiliaji kipo chini ya asilimia 10 Tanzania Inajikokongoja Kilimo cha Umwagiliaji.

Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Tanzania Inavyojikongoja Kilimo cha Umwagiliaji.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257












 

0/Post a Comment/Comments