Noti Zenye Saini ya Mwigulu Zinaendelea Kutumika

 

Adeladius Makwega-Musoma MARA

Ni majira ya asubuhi ya Januari 13, 2026, Ofisi ya Msajili wa Hazina Ndogo hapa Musoma Mara inapokea ugeni kutoka Benki Kuu Kanda ya Mwanza, ukiongozwa na Bi Rosemary Palagha ambaye ni Meneja Msaidizi -Kitengo cha Huduma na kufanya mazungumzo kadhaa:

“Kwa hakika sisi na Hazina Ndogo tunafanya kazi kwa karibu, huku malipo yote yakifanyika sisi na wao kwa pamoja tunashirikiana kukaimilisha kazi hii, hivyo basi ushirikiano wa karibu baina ya Benki Kuu na Hazina Ndogo ni wa lazima, sisi mapacha tunaofanana.”

Bi Palagha alisema kuwa Benki Kuu inaendelea na majukumu yake vizuri na ujio wao Musoma ni sehemu ya kazi zao na siyo pikiniki, akijibu swali la Mwanakwetu juu ya noti za Benki Kuu na saini zake alisema:

“Kwa sasa noti zao ni zile zile zenye saini ya Mwigulu Nchemba pahala pa Waziri wa Fedha na Emmanuel Tutuba pahala pa Gavana, zinaendelea kutumika.”

Mwanakwetu kutokana na utomaso wake hapa hapa aliitazama noti ya shilingi 2000 aliyekuwa nayo mfukoni pia ilionesha hivyo.



 

Mwanakwetu akisema moyoni kumbe saini ya Mwigulu Nchemba itaendelea kujidai katika noti zetu, japokuwa sasa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Hazina Dogo hapa Mara Henry Mishwaro alisema kuwa ameupokea ugeni huu kutoka Benki Kuu vizuri, wamefanya mazungumzo ya kina ambayo yamelenga kuboresha ufanisi wa kazi maana wanategemeana:

“Kwa sasa malipo yote ili yafanyike na kukamilika sisi ni miongoni kwa timu ya kufanikisha hili kwa haraka kupitia mifumo ya malipo ya fedha. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ina miradi mingi na mikubwa katika maeneo yote ya Kanda ya Ziwa, makampuni ya Wazawa na Kigeni yakifanya kaz, hivyo basii mawasiliano ya simu ya kila mara, vikao vya hapa na pale ni jambo la kawaida na hili ndilo tulilolifanya leo hii hapa Musoma.”

Mazungumzo haya yaliwakutanisha pia maafisa wengine kadhaa wa taasisi hizi mbili zilizo chini ya Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwanakwetu akiwa hapa alivutiwa na sare za Benki Kuu hasa wafanyakazi kazi wake wa kike waliovalia suti nyeusi blauzi za rangi ya dhahabu ambapo walipendeza mno, kwanza Mwanakwetu aliomba namba zao za simu huku akilini mwake alikumbuka ile rangi ya dhahabu ilifanana na kizibao cha Mwanakwetu alichokivaa mwaka 2009 wakati akifunga ndoa. Mwanakwetu alipewa namba zao za simu na kuziandika na kwa heshima ya rangi ya dhahabu iliyofanana na Jamba Koti lake harusini mwaka wa 2009 akaamua kuyaandika makala haya ya taasisi hizi mbili za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati haya yakifanyika hapa Musoma Mjini ofisi ya Hazina Ndogo, hali ya hewa ya Mji wa Musoma ni nyuzi joto 26, unyevunyevu ni wa asilimia 10 ujirani na mvua ni wa asilimia 62 na upepo ukivuma kwa KM 14 kwa saa.

Mwanakwetu upo? Kumbuka

“Noti Zenye Saini ya Mwigulu Zinaendelea Kutumika.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257 

 









0/Post a Comment/Comments