Adeladius Makwega-MBAGALA
Ilikuwa Januari 12, 2026, kwa Tanzania Taifa la Afrika Mashariki ni siku ya mapumziko ambapo shughuli za serikali zile zisizo za dharura hazifanyika lakini hospitalini, polisi na kazi zingine za dharura mambo yaliendelea ambapo Watanganyika na Wazanzibari (Watanzania) wanakumbuka siku Zanzibar ilipokombolewa kutoka katika makucha ya Sultan Jamshidi Bin Abdulah.
Mwanakwetu akiwa kwake alitazama baadhi ya makala zilizoandikwa / kutayarishwa siku hii na wanahabari wa Watanzania, aliona makala kadhaa lakini alivutiwa na makala moja ya Majjidi Mjengwa ambapo Blog ya Full Shangwe waliitumia kama ilivyoandikwa. Siku moja nyuma yaani Januari 11, 2026 Majjidi Mjengwa alimpigia simu Mwanakwetu na walizungumza mambo kadhaa, huku msomaji wangu naomba utambue kuwa Mwanakwetu na Mjengwa ni watu wanaofahamiana sana. Kumbuka hapa Mwanakwetu ndiyo ameamka sasa lazima apike kifungua kinywa, akakagua jikoni kwake akabaini kuwa hana majani ya chai, haraka haraka akanunua katika duka jirani kisha kurudi na kuanza kupika chai yake ya rangi huku akilini mwake anajiuliza leo ni MAPINDUZI watanzania wenzake wapo majumbani, je inapita bure bila ya yeye kuandika chochote? Chai ili ikapandikwa mekoni, Mwanakwetu akachukua chapati mbili mezani, akatengeneza kachumbari maridadi akaanza kuinywa chai yake.
Mwanakwetu akanywa mafundo matatu ya chai na vipande vya chapati kadhaa kisha akilini mwake yakamjia majina matatu wa Watanzania ambao ni marehemu nao ni marehemu Thabiti Kombo, marehemu John Gudinita na marehemu Richard Tambwe Hiza. Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anakunywa chai yake katika kikombe chake cha plastiki na cha rangi ya kijani ikiwa top cup. Kichwani kwa Mwanakwetu akakumbuka kisa hiki:
“Nyie vijana sikilizeni, hapa wapo Wasomari, hapa wapo Wamanga, hapa wapo Waarabu na hapa wapo jamii ya Wazungu ambapo jamii zote wote hapa sote ni Watanzania. Nyinyi weusi msijifanya bora kuliko wenzenu. Sisi sote ni sawa, sote ni Watanzania. Hili siyo hapa kwa CCM tu, iwe katika kugombea uongozi, iwe katika kazi, iwe shuleni kama mnamchagua kaka mkuu au dada mkuu, Sisi sote ni sawa.”
Haya maelezo anayatoa John Gudinita katika eneo la Umoja wa Vijana CCM -Jengo la Makao Makuu ya Umoja huo pale Dar es Salaam, kwa chini jirani na Shule ya Sekondari Agakhan Mzizima katika kiwanja kilichokuwa wazi, vijana wengi wamekaa chini, yeye kiongozi kasimama mbele, hii nadhani ni mwaka 187/1988 nadhani maandalizi ya miaka 10/11 ya CCM. Wakati Gudinita anaongea wakaja jamaa wa Bakhresa wakatuletea Ice Cream nyingi katika madeli mengi vijana umero ukatujia.
Naomba niongeza na hili, Mwanakwetu alishiriki katika shughuli hii kwa kulazimishwa sana na marehemu mama yake Doroth Mlemeta ambaye alikuwa Mwalimu Shule ya Msingi Mnazi Mmoja Dar es Salaam akisema mikishiriki mtapata traki suti, kofia na laba bure.
Kumbuke Komredi Gudinita yupo mbele akasema:
“Msiwape vitu vya baridi, msiwagawie, hawajakunywa chai hao, kwani yao bado?Wapeni chai na mkate mmoja wawili wawili, mikate ile kama soli ya kiatu, kisha wapeni hizi Ice Cream maana wametoka kufanya mazoezi.”
Gudinita akasema namaliza sasa hivi:
“Sultani na jamaa zake walikuwa washenzi, walikuwa washenzi sana alikuwa anawachukua vijana anawapa kazi ya kuchimba mashimo ya minazi, hili wapande minazi.
Kwa desturi mnazi unachimbiwa shimo refu kidogo ambalo lilikuwa ni kama urefu wa nusu binadamu yaani tangu nyayoni hadi kiunoni. Vijana wa Zanzibar wenyewe na vijana wageni waliokwenda Zanzibar kutafuta maisha walifanya kazi hizo huku ili kupata pesa ya kuishi. Hapa wanafanya kazi hiyo kwa ujira mdogo. Kumbe katika kazi hii kulikuwa na ushenzi unafanyika wakiwa kazini. Unapewa kazi mbali na wenzako kisha unachimba mashimo yako kadhaa, ukishakuwa unakaribia kumaliza labda kwa hesabu umechimba mashimo mia ili siku nyingine mje kupanda anakuja mjinga mmoja –mpumbavu mmoja , mshenzi mmoja, wewe upo shimoni anakuvamia na wenzake wanakuvua nguo kichwa kipo chini ya shimo kisha wanakulawiti, kwa kuwa upo ndani ya shimo hauwezi kupambana nao, wakishafanya hivyo sasa wanakwambia tuwe tunaendelea na huu mchezo. Vijana wengi mara baada ya kufanyiwa hivyo walikasirika na kutokwenda kufanya kazi katika viunga vya minazi Sultan. Hilo liliongeza chuki kwa utawala wa Sultan na hapa ndipo Afro Shirazi Party iliungwa mkono mno maana Ubaya wa Sultan Ulikuwa na Ushahidi Mioyoni Mwa Vijana.”
John Gudinita anaongea mbele, Mwanakwetu siku hii yupo na kundi la vijana wamekaa chini wanamsikiliza, John Gudinita akauliza haya mambo ni mazuri?
Vijana wakajibu:
“Siyo Mazuri.”
Akauliza haya mambo ni mema? Vijana wakajibu:
“Siyo Mema.”
Haya mambo ni ya heshima?Vijana Wakajibu:
“Siyo ya Heshima.”
Haya mambo ni ya haki ? Vijana Wakajibu
“Siyo ya Haki.”
John Gudinita akaendelea kuongea:
“Ndiyo maana ASP, TANU, Kuba, Misri na wenzetu wengine waliungana na Wazanzibar wanyonge kupambana na Sultan hadi akaondolewa madarakani. Hawa Kuba akina Fidel Castro ni weupe, Misri hivyo hivyo lakini walikuja kutusaidia kama binadamu wenzetu na wenzao walikuwa wakionewa na ndiyo maana hapa mpo rangi zote na makabila yote ya Tanzania, sisi ni Watanzania.”
John Gudinita akasema yeye hakuwepo Zanzibar lakini kisa hiki alisimuliwa na Waziri Thabiti Kombo. Baada ya maneno haya akawaaga vijana wale na kuondoka zake. Pale mbele ukatolewa utaratibu wa chai, vijana wakanywa chai hiyo ya mkate mmoja watu wawili, kisha kila mmoja kupewa Ice Cream za Bakhresa na kugawiwa traki Suti na Kofia na moja moja kwa zoezi lililokuwa mbele yetu.
Msomaji wangu nakuomba ukumbuke kuwa Mwanakwetu anakunywa chai ya Januari 12, 2026 na huku akikumbuka chai ile ya CCM na mkate mmoja vijana wawili mwaka 1988 na haya anayakumbuka tu akilini mwake pia akimkumbuka mama yake mzazi alivyokuwa akilmlazimisha kwenda kule:
“Adeladius(mwanangu) nenda mwanangu nenda utapata traki suti.”
Mwanakwetu pia akamkumbuka marehemu Richard Tambwe Hiza ndugu yake wa Temeke na Mbagala –Dar es Salaam. Siku moja kwenye kampeni za Ubunge CCM jimbo la Mbagala mwaka 2015 akasema maneno haya:
“Viongozi wa sasa wa CCM hawakuona ule uchungu na hekaheka na kudai uhuru na Mapinduzi, hawajui kuwa mambo haya yalianza kama utani; malalamiko, jamani mnafanya hivi, jamani mnafanya vile. Watu wakawa wanaacha kazi kwa mkoloni kama utani, hadi mwisho mabadiliko yakawaidia. Viongozi wa sasa wanaongea sana, vitendo kidogo na kusikiliza hakuna, wakati wenzao akina Julius Nyerere walikuwa wanasikiliza mara 365 na kuongea mara moja tu-sasa wewe unaongea mara 365 kisha kusikiliza mara moja, hauwezi kufanikisha mambo ya watu, maana mambo ya watu huyajui. Mie nipo nao CCM, Mkuu Propaganda nikiongea wanasema Rais usimsikilize Tambwe usimsikilize, huyo ni CUF, Tambwe huyo CHADEMA, sasa unawashangaa mimi nipo na nyinyi bado mnasema mimi ni mpinzani sasa kule wapinzani mimi wananiita msaliti, haya maneno yakijirudia lazima niende hukohuku si ndiko mnaponinasabaisha na pengine huko ndipo Mungu anataka niwe.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anakunywa chai yake hii ya Januari 12, 2026 ambapo haya anayakumbuka na lile la awali alimkumbuka John Gudinita na kisa kile cha Thabiti Kombo na mwisho hiki kisa cha Richard Hiza Tambwe. Mwanakwetu chapati zake mbili, kachumbari na kikombe chai kiliingia tumboni mwake na kumtia nguvu ndipo alipoamua kuyaandika makala haya ambayo unayasoma msomaji wake.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika kisa cha marehemu Thabiti Kombo juu ya tabia mbaya za Sultan na jamaa zake kinajieleza vizuri na viongozi wa leo wafahamu MAPINDUZI ya kweli siyo kwenda uwanjani na watu kuvaa suti kulingishiana, huyu kapembeza, huyu hajapendeza, magwaride au huyu kawa wa kwanza kuingia na huyu kawa wa pili kuingia hayo siyo MAPINDUZI ya kweli, mapinduzi ya kweli ni kutatua yale mambo yanayolalamikiwa na wananchi. Ndiyo maana TANU, ASP, Kuba, Misri na wengine hawakuungana kumtoa Sultan kwa hayo ya sherehe kwa hayo ya mikogo na gwaride bali shabaha, nia ni kuwasaidia wanyonge waliyokuwa wakinyanyaswa na kulawitiwa na Sultan na washirika wake.
“Hapa haiwezekani tunasherekea Mapinduzi ya Zanzibar huku Katibu Muenezi wa CCM Taifa yupo, huku Mtanzania mwenzake aliyewahi kushika nafasi hiyo hiyo na Msimamizi Mkuu wa Kampeni wa Urais wa Serikali iliyopita hivi punde ya John Pombe Magufuli katekwa na hajulikani alipo, sasa kama Katibu Muenezi mstaafu, Balozi wa nchi kadhaa katekwa, Mbunge wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania , mwana CCM katekwa wewe mlinzi wa Katibu Muenezi wa sasa upo salama ? Wewe Katibu Muenezi wa CCM Taifa wa sasa upo salama? Wewe mwananchi wa kawaida upo salama? Ndugu Humphrey Polepole kaongea, kayasema ya moyoni, yeye ni Mtanzania, yeye ni kiongozi, wapo watu ni viongozi leo hii Polepole kawatengeneza, sasa akaongelee wapi ? Kule Kuba au Malawi? Kutekwa kwake hakukubaliki.
Hapa tukisema ndiyo yale yale ya kuchimba mashimo na minazi na kulawitiana itakuwa siyo sahihi? Wazanzibari walivunja ukimya, wakaungana na jamaa zao hadi Sultan akaondolewa. Hapa CCM lazima itambue ni chama cha namna gani? Hali hii siyo nzuri, haya yanayoonekana mitaaa na vijijini Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ni ushahidi wa hali ilivyo. CCM ilipaswa kuyaona mapema na kuyafanyia maamuzi haraka, siyo kugoja kamati, kamati ya nani? Tume tume ya nani? Kwani kwa sasa CCM hakina macho basi tukinunulie miwani ili kiweze kuona maana hiki ni chama cha mapinduzi. Rejea maswali ya John Gudinita kwa vijana wale siku ile: haya mambo ni mazuri? Haya ni mambo ya heshima? Haya ni mambo mema? Haya ni mambo ya haki? Kiongozi mzuri lazima uwapende vijana wako, chochote utakachowafanyia vijana ni hatari maana vijana wana nguvu ya mwili na akili, wewe ni mtu mzima, akili imechoka na nguvu hauna labda kuwatumia vijana wengine, je utawatumia vijana wengine hadi lini?
“Kiongozi mzuri anawapenda vijana wake, Kiongozi mzuri anawatendea Haki raia wake, Kiongozi mzuri anaongea mara moja na kiongozi mzuri anasikiliza Mara 365.”
Kama unasikiliza mara 365 hauwezi kuwapigwa vijana wako risasi, hawezi mtu yoyote kubakwa wala kulawitiwa, hawezi mtu yoyote kutekwa, hawezi mtu yoyote kufungwa gerezani na vyombo vya ulinzi na usalama haviwezi kuchukiwa na raia wake.
“Ebu tujiulize mtu anaweza kuwa yupo katika majukumu lakini kama binadamu timamu anajiuliza hapa ni salama? Yasije kunikuta na Mdude, yasije kunikuta ya Ali Kibao, yasije kunikuta ya Humphrey Polepole. Jiulize hawa watu wananifikiriaje? Hawa watu Wananionaje? Hawa watu Wanaamani na mimi? Hawa watu Wananiombea nini? Omba Mungu akufungulie mioyo ya binadamu wenzako, utaliona hili.”
Mwanakwetu upo?Je makala haya yaitwaje?Nenda Mwanangu Nenda Utapata Traki Suti,Ungesikiliza Mara 365? Au Gudinita , Tambwe Hiza na Thabiti Kombo? Mwanakwetu anachagua Nenda Mwanangu Nenda Utapata Traki Suti.
Nakutakia siku njema
0717649257-NB Makala haya ni maalumu kwa ndugu yangu Majjidi Mjengwa.
.gif)























Post a Comment