Mwanangu Mbona Umekata Nywele?

 



Adeladius Makwega-MBAGALA.

Katikati ya mwezi wa Januari 2026 Mwanakwetu alitembelea ukurasa wa mitandao ya kijamii wa mama mmoja anayeitwa Maria Mlyuka aishie Area D Dodoma nchini Tanzania.Mwanakwetu akiwa hapa alikutana na bango moja ambalo lipewa maneno haya:

“Jamani kumtetea rucy ni kazi , hahahaha ! Padri Dkt Kitima Siyo Baba Askofu wewe dada hahahaha ! Huyu ni Padri na ndiye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hahahaha!”

Mwanakwetu aliposoma bango hili akacheka sana kisha akaendelea kuukagua ukurasa huu wa Maria Mlyuka . Mbele kidogo Mwanakwetu akakutana na bango la pili likawa na maneno haya:

“Wamepigwa upofu, wakaondolewa ufahamu, wakakosa maelewano kama wale wa Babeli wakaanza kuongea vitu visivyoeleweka- PENTESTESHENI hahahahaha!”

Mwanakwetu akawa anacheka tu kisha akakutana na picha moja na mama mmoja mweupe amekata nywele, hapa hapa Mwanakwetu akachukua simu yake akanakili namba ya Maria Mlyuka na kisha kuiweka vizuri ili aipigie aongee naye.

Msomaji wangu natambua unajua kuwa Mwanakwetu yu katika ukurasa wa Maria Mlyuka na kwa faida yako msomaji wangu fahamu kuwa Maria Mlyuka alizaliwa huko Mkoani Iringa ambapo alisoma Shule ya msingi Nduli jirani na uwanja wa Ndege wa  Iringa na kisha mwaka 2005 alijiunga na Shule ya Sekondari Isimani Tarafani kwa kidato cha kwanza akiwa miongoni mwa wanafunzi wa Mwanakwetu aliowasomesha shuleni hapa kati yam waka wa 2004- 2009 ambapo Maria Mlyuka alipokelewa na kupangiwa kidato cha kwanza C mwaka 2005.Mwanakwetu anakumbuka mambo kadhaa juu ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wa Isimani Sekondari mwaka huo wa 2005:

“Wanafunzi wengi wa kike walipata ujauzito na kuacha shule, huku wanafunzi wengine wa kike wa kidato cha kwanza na walikweneda kufanya kazi za ndani maeneo kadhaa ya Tanzania huku walimu wakihangaika kuhakikisha wale waliocha masomo na kwenda kufanya kazi za ndani wazazi wao wanakamatwa na kisha wanaeleza walipo mabinti zao na kurudishwa vijijini kwao na kuendelea na masomo. Walimu walishirikiana na Afisa Tarafa ya Isimani aliyefahamika kama MAKENDI na Afisa Mtendaji wa kata ya isimani aliyefahamika kama KISEWE, huku mabinti wote wa shule ya sekondari Isimani walipewa makazi ndani ya Kanisa Katoliki Parokia ya Isimani enzi ya Padri Muitaliano aliyefahamika kama Padri Anjelo.Huku Maria Mlyuka alisoma vizuri na kuhitimu shuleni hapa.”

Kumbuka Mwanakwetu ameshainukuu namba ya simu ya Maria hapo hapo akampigia simu. Haya Maria hujambo? Akajibu Sijambo Shikamoo Baba, Shikamoo Mwalimu, Mwanakwetu akajibu Marahaba. Haya Mwanangu Maria Mbona Umekata nywele? Maria akajibu:

“Ni kweli baba nimekata nywele, mambo ni mengi , hata huo muda wa kwenda saloon sina, nikaamua nizikate nywele zangu.”

Mwanakwetu akasema ni sawa lakini marafiki zako wa saloon watakuchukia wanatambua kuwa sasa wewe siyo mteja wao na hauwapatii pesa tena. Maria Mlyuka akajibu ni kweli pesa zangu wamezikosa.

“Mwalimu Makwega nikikuona mtandaoni nakumbuka mengi sana, nakumbuka mbali sana baba yangu, lakini mwalimu mimi siku hizi nimekuwa mkubwa ukiniona utashanga, nimekuwa mkubwa.”

Mwanakwetu akacheka sana kisha kuagana na mwanafunzi wake huyu ambaye kwa hivi sasa ni mjasiriamali huko jijini Dodoma.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu siku ya leo ameamua kukueleza namna alivyokuwa na furaha alivyoutembelea ukurasa wa Mwanafunzi wake Maria Mlyuka aliyemfundisha miaka 21 iliyopita kwa mwaka 2026 huko Mkoani Iringa na huku ameelezea namna mabinti wa Iringa walivyosoma kwa changamoto tele enzi zile. Msomaji wangu pia tambua kuwa wanafunzi wa Mwanakwetu wana akili sana huyu ni mmoja wao anaitwa Maria Binti wa Mlyuka wa Nduli Uwanja wa Ndege.Mwanakwetu upo?Je makala haya yaitwaje?Watu Wamepigwa Upofu?Au Mwanangu Mbona Umekata Nywele? Mwanakwetu anachagua Mwanangu Mbona Umekata Nywele?

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257









 

0/Post a Comment/Comments