Hapo zamani za kale, Kijana mmoja Mkatoliki wa Jimbo la Dar es Salaam aliomba kujiunga na Upadri baada ya kuhitimu kidato cha sita ambapo kijana huyu awali hakusoma shule za seminari.
Yale maombi yake yakatumwa kwa Padri mmoja aliyekuwa na cheo kinachoitwa Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa maelezo aliyoyapokea Mwanakwetu, kijana huyu wakati huo alipoomba kujiunga na mafunzo haya jukumu lilibaki kwa Mkurugenzi wa Miito kupitia maombi haya kwa kuangalia je maisha ya kijana huyu na familia yake, je yanafaa kuingia mafunzo ya malezi ya utawa na kisha ajiunge na mafunzo ya Ukasisi?
Mkurugenzi wa Miito wa wakati huo alifanya kazi yake vizuri na hadi kutembelea Parokia, Kigango na Jumuiya na kukusanya taarifa zote muhimu na baadaye kumuita kijana huyu kupitia kwa Paroko wake katika matangazo ya Jumapili.
“Fulani Bini Fulani aende Kanisa la Mtakatifu Yosefu gorofa ya Pili, Ofisi ya Mkurugenzi wa Miito siku ya Jumatano tangu asubuhi hadi saa nane ofisi yake ipo wazi.”
Kijana huyu anadai kuwa alipofika pale kwa Mkurugenzi wa Miito akasema haya:
“Tumefanya ufuatiliaji wa maisha ya familia yenu inaonekana baba na mama yako hawakai pamoja,(kijana akajibu naam) wametangana lakini katika matokeo yako ya kidato cha sita una F moja, sasa kupata upadri kupitia jimbo itakuwa ngumu, labda ujaribu kuomba kupitia mashirika, nikupe anuani uombe?”
Kijana yule akasema anaomba kama dakika 10 akatafakari nje, kisha atatoa majibu. Kijana akatoka ofisi ya Mkurugenzi wa Miito, akashuka chini, hadi geti la Kanisa la Mtakatifu Yosefu, kisha akaamua kurudi kuketi katika ngazi za Kanisa la Mtakatifu Yosefu, akakaa ngazi ya kwanza ya kwanza kabisa kutoka chini,huku akizama upande Forodha ya Dar es Salaam akitafakari hilo. Dakika tano zilipita kisha kupata majibu na alafu akarudi kwa Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, hapa sasa katika dakika 10 sasa ni saba bado dakika tatu.
Akapiga hodi na kuitikiwa vizuri, kuufungua mlango kisha kueleza maamuzi yake:
“Nimetafakari sasa Baba Padri, nimeona, nimeona , nimeona kama Jimbo langu Katoliki limenikataa kwa hoja zake mbili ; F kwa somo moja la kidato cha sita na Wazazi wangu kutokukaa pamoja, nadhani nisiombe tena kujiunga na mafunzo haya kupitia Mashrika , pengine hii njia kwangu siyo sahihi.”
Kijana yule akapeana mkono na Mkurugenzi wa Miito ambaye alikuwa Padri mmoja, mzalendo, mrefu, mweusi kwa kumpa mkono kisha akatoka zake na kuondoka zake kurudi nyumbani kwao na kuangalia muelekeo mwingine wa maisha yake, utawa aliyoutamani umegonga mwamba, akachukua njia nyingine kabisa akawa mtu wa familia.
Mwanakwetu ambaye alikuwa na ujirani na ndugu huyu akamuuliza kwani ni kweli wazee wako hawakai pamoja? Jamaa huyu alijibu haya:
“Mama alipata Bwana mwingine akaachana na mzee, kisha kuanza maisha mapya kwa talaka za kimahakama. Baadaye kanisa likaingilia kati ili kutatua tangu baraza la walei, shabaha ni kuirejesha ndoa hii vizuri, hali ikawa inatia moyo wa kurejeshwa ndoa hii kabisa. Lakini ndugu wa mwanaume wakasema ni kweli kanisa ndoa haivunjiki lakini huyu mama mwanamue aliyekuwa alinachepuka naye alikuwa na ugonjwa wa kisasa ambao wakati huo ulikuwa ndiyo unaingia sasa kurejesha ndoa hii ni kuhatarisha uhai wa ndugu yao, hivyo basi sisi ndugu hatuoni salama ya ndoa hii kwa sasa lazima tulinde uhai wa ndugu yetu. Wakati maisha haya yanaendelea ndipo Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam anafanya uchambuzi wa taarifa za jina la yule kijana, jina la kijana yule kujiunga na mwaka wa malezi ili awe kasisi.”
Mwanakwetu akatoa pole sana lakini ndiyo ilikuwa hivyo kijana aliukosa upadri.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Maisha ya familia ni magumu sana, kijana yule wa zamani aliukosa Upadri kwa makosa ya wazazi wake, hasa mama yake aliyeanzisha mahusiano hatari kiafya na hatari kiroho kwa mwanaye,
“Padri wa Jimbo lazima wazazi wake wawe mfano wa familia zingine kiroho huku akiwa amefeli somo moja la kidato cha sita kwa alama F”
Familia hiyo walielewa zaidi ya maamuzi ya ndoa hii kurudishwa tena kwa hakika siyo jumuiya, wala Baraza la Walei walijulishwa hili la afya hili lilikuwa siri ya familia.
Yule mama alifariki na yule mwanaume wa kando walifariki dunia mapema, huku huyu mzee ambaye kijana wake aliukosa upadri yu hadi kesho.Waliofariki walifariki mapema kabla kijana yule hajaanza maisha ya ndoa na hakurudi tena kwa Mkurugenzi wa Miito wala Shirikani kuomba kujiunga na Upadri kitabu kilikuwa kimeshafungwa.
Swali ni je Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam kama angalijua hili la afya je angeweza kumruhusu kijana yule kwenda mwaka wa malezi na kusomea Ukasisi? Au hoja ya F ya somo lingine ingesimama?
Hii ni tafakari ya leo katika makala haya ya Mwanakwetu ambayo anaomba Wakurugenzi wote wa Miito wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni Waitafakari na kila wanapokwenda kuchunguza maisha ya miendo ya familia za Wakristo wao wawe makini mno ili waweze kupata taarifa zilizojificha katika maisha ya ndoa ya familia za wanadamu.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Mkurugenzi wa Miito wa Jimbo .”
Nakutakia Siku Njema.
makwadeladius @gmail.com
0717649257




Post a Comment