“Leo ni Jumapili ya tatu ya Mwaka A wa liturujia ya Kanisa. Injili inasimulia mwanzo wa huduma ya hadharani ya Yesu.Yesu alibatizwa na Yohane, ambapo Mungu alimfunua Yesu kuwa Mwana wake. Kisha Yesu alijitenga akaenda jangwani kujiandaa kwa utume wake na akashinda majaribu ya shetani. Aliporudi, Yesu alisikia kwamba Yohane alikuwa amekamatwa. Injili inatuambia kwamba tangu wakati huo Yesu alianza kuhubiri akisema, ‘Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia.’
Kisha Yesu aliwaita wanafunzi wake wa kwanza, wavuvi Petro, Andrea, Yakobo, na Yohane, ambao tangu hapo wangekuwa wavuvi wa watu. Wao wakamfuata bila kusita. Pamoja nao, Yesu alizunguka Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, akihubiri Injili ya Ufalme, na kuponya kila ugonjwa na maradhi miongoni mwa watu.”
Haya ni Kadinali Luis Antonie Tagle Mkuu wa propaganda Fide ya Kanisa Katoliki Ulimweguni inayojihusisha na Uinjilishaji wa watu sehemu ya tafakari yake kwa jumapili ya Januari 25, 2026.
Mwanakwetu alitembelea pia Redio Vatikani wao walikuwa na tafakari ndefu kidogo iliyofanywa na Padri Bonaventura Maro kutoka huko Austria huku alianza tafakari yake kwa kukirusha kishada chake hewani juu ya maelezo ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwa dominika hii;
“Dominika ya Tatu; Dominika ya Saba ya Neno na Siku ya 59 ya Kuombea Umoja wa Wakristo. Papa Leo XIV anawahamasisha waamini wa Kanisa Katoliki kujibidiisha kusali kwa ajili ya kuombea Umoja wa Wakristo, ili umoja kamili na unaoonekana wa Wakristo wote uweze kupatikana. Anasema, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, anazungumza na wanadamu kama mtu anavyo zungumza na rafiki yake. Ni mwaliko kwa waamini kujenga utamaduni wa kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao pamoja na sala.”
Padri Bonaventura Maro pia aliyataja mambo manne ambayo ni ya kuzingatia katika masomo yote matatu ya dominika hii, nayo ni:
“Kwanza: Ni wapi bado katika maisha yangu ninatembea gizani? Mwenyezi Mungu anakuita sasa kubadilika na kuanza upya. Somo la kwanza limeeleza hali ya ta taifa hili la Israeli waliokuwa utumwani kwa Waashuru, hali ya hofu, mashaka, giza, mkato wa tamaa, maumivu na kudharauliwa.
Pili: Giza la Majivuno na wivu na ubinafsi. Katika maisha yangu/yetu moyo wangu unatawaliwa mara kwa mara na giza la majivuno na wivu. Mwenyezi Mungu anatubariki nyakati fulani ili kupima mtazamo wetu. Anatuinua ili kutupima, namna tutakavyoziishi baraka za Mungu, kwa ajili ya Mungu mwenyewe na kwa ajili ya watu. Tatu: Wongofu wetu sio kwa ajii yetu sisi wenyewe, bali ujenge umoja na upendo katika familia na Kanisa. Taifa la Israeli waliinuliwa na Mungu na kwa njia yao walipaswa kuwa nuru na mwanga kwa watu wa mataifa mengine. Mitume wa Kristo hali kadhalika waliitwa na Mungu, wakaacha vyote si kwa ajili yao, bali kwa ajili ya kuendeleza kazi ya kueneza Injili kwa watu wa mataifa yote. Nne na mwisho Padri Bonaventura Maro anasema Tuwe na Ujasiri na Matumaini. Kristo anatuita kila mmoja katika ukawaida wake, anatustahilisha kwa kuwa Bwana ni nuru na wokovu wetu, tusiogope. Zaburi ya 27 katika Dominika hii ya tatu inatupa moyo na matumaini kwamba, ‘Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani, Bwana ni ngome ya uzima wangu nimhofu nani?’ Kristo hatuiti kwa kuwa sisi tu wakamilifu bali anastahilisha sisi aliotuita, kutoka katika ukawaida wetu kama alivyowaita Mitume lakini hili linahitaji utayari wetu.”
Wakati haya yakiendelea ndani ya kuta za kanisa hali ya hewa ya Mji wa Kigoma ni nyuzi joto 27, unyevunyevu ni asilimia 5, ujirani na mvua ni asilimia 77 na upepo ukivuma kwa KM 8 kwa saa. Huku mji wa Masasi una nyuzi joto 32 unyevunyevu ni wa asilimia 20 ujirani na mvua ni asilimia 50 huku upepo ukivuma kwa KM 5 kwa saa na kwa mji wa Bukoba hali ya hewa ni ya nyuzi joto 26 unyevunyevu ni nyuzi sufuri ujirani na mvua kwa asilimia 65 na upepo ukivuma kwa KM 13 kwa saa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka.
“Jibidiesheni Kuomba Umoja wa Wakristo.” Papa Leo XIV.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257





Post a Comment