Haya yalikuwa mazingira ya bucha ya nyama ya ng’ombe katika mkoa mmoja wa Tanzania Bara ile iliyokuwa Tanganyika taifa la Afrika ya Mashariki mwaka wa 2026. Binti mmoja anaingia na chupa ya chai na vitafunwa kaviweka katika kikapu maalumu, huku akisema nimeleta chai yako. Muuzaji wa bucha, jamaa mmoja mweupe mwenye uwalaza akakaa kimya, hakumjibu huku akiendelea kupima nyama ya mteja wake. Binti huyu aliyebeba chai akaingia buchani na kutua kikapu chake chini kisha kuwasalimu jamaa aliyowakuta kwa salaam ya SHIKAMONI, kisha muuzaji nyama kuitikia MARAHABA na kusema maneno haya:
“Mwanangu, ukifika eneo lolote watu wakiwa mbele yako kwanza unasalimia kisha ndipo unaeleza shida yako, sasa weka chai hapo chini nenda pesa uje kuchukua baadaye.”
Binti huyu mfupi mweusi akaaga na kuondoka zake huku akicheka , hii ilionesha kuwa palikuwa ujirani baina ya muuzaji wa nyama buchani nab inti muuza chai lakini ujirani huu muuza bucha hakupenda mteja wake haufahamu. Buchani wakabaki watu wawili muuzaji na mteja wake huku sasa muuzaji anaikata nyama vipande vipande. Mnunuzi akauliza hivi bei ya nyama ya ng’ombe kuna dalili yoyote ya kushuka? Muuzaji akajibu:
“Hapana tajiri akishapandisha bei unadhani anaweza kushusha labda muwe na serikali jamii ya kama ya Magufuli ambayo ipo mitaani inanusa kila kinachoondelea kwa wananchi wao, kabla ya Oktoba 29, 2025 bei zilikuwa za nafuu baada ya matukio ya siku zile nyama ikapanda bei na bei hii imepanda kwa shilingi 2000 zaidi , mathalani kwa kila kilo moja ya nyama yenye mifupa ilikuwa ni shilingi 10,000 sasa ni shilingi 12,000 za Kitanzania, nyama ya steki ilikuwa 12,000 shilingi lakini sasa ni shilingi 14,000 labda kwa utumbo tu ndiyo umepanda kwa shilingi 1000 zamani ulikuwa 7000 na sasa ni shilingi 8000…”
Mnunuzi akafungiwa nyama yake vizuri akalipa shilingi 15,000 na kurudisha shlingi 1000 ya Tanzania iliyochakaa mno na kisha muuzaji kuanza kunywa chai yake huku mnunuzi akarudi alipotoka.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu alipoipata simulizi hii ya kweli alitaka kujua bei ya kilo moja ya nyama kwa nchini kenya ni kiasi gani?
“Kwa nyama yenye mifupa inauzwa kati ya shilingi 750 hadi 850 kwa shlingi ya Kenya huku kwa nyama steki ni shingi 1300 ya Kenya”
Hizo ni bei ya Kenya ambalo ni taifa la Afrika Mashariki kama ilivyo Tanzania Bara ambapo simulizi ya awali ilipatikana. Swali likaja je bei ya nyama ya ngombe huku Zanzibar ikoje? Jibu lake ilikuwa ni kati ya shlingi 13,000- 14,000 za Kitanzania.
“Kwa hesabu za uchumi bei ya nyama ya Ng’ombe Zanzibar ilipaswa iwe juu zaidi maana ng’ombe husafirishwa mara zote toka Bara kwenda Visiwani na bei ya nyama ya Bara ilitakiwa iwe chini maana maeneo kadha ya Iliyokuwa Tanganyika ng’ombe wanafungwa. Kwa hesabu za uchumi inakataa bei ya Bara na Visiwani kufanana.”
Ukitazama bei ya Kilo ya nyama kwa Kenya na Tanzania Bara zinafanana lakini bei ya kilo ya nyama za Tanzania Bara lazima iwe chini kwa hoja moja kubwa ya idadi ya mifugo milioni 38 karibu milioni 40 ambayo ni robo tatu ya Watanzania huku Kenya wakiwa na mifugo karibu milioni 24 tu. Jambo la mwisho nakuomba msomaji wangu fahamu kuwa nyama inayonunuliwa kwa wingi ni nyama yenye mfupa, na hii nyama ndiyo inayonunuliwa na watu masikini. Kwa hiyo kupandishwa kwa bei ya nyama ya ng’ombe kutoka shilingi10,000 hadi 12,000 kulitulenga watu masikini ambao ndiyo tunaokula nyama zenye mifupa na ndiyo tuliyo wengi na ndiyo wateja wa nyama ya ng’ombe, nani kwambia masikini anakula steki?
Mwanakwetu kwa heshima ya walaji wa nyama ya ng’ombe Tanzania anaomba aelezi kwa kifupi faida ya kiafya za kula nyama ya ng’ombe kwa binadamu kama zilivyowahi kuelezwa na Dkt, John Somi daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Watoto wilayani Lushoto mwaka wa 2017.
“Nyama ya ng’ombe (beef) inaweza kuwa chanzo muhimu cha virutubisho muhimu vinavyotoa faida mbalimbali za kiafya. Faida hizi ni pamoja na: kuwa chanzo bora cha protini kamili, kwani ina amino asidi zote tisa muhimu zinazohitajika kwa ukuaji wa mwili, matengenezo, na ukarabati wa tishu, misuli, na mifupa. Ni chanzo kikuu cha madini ya chuma mwilini ambayo hufyonzwa kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.
Hii husaidia kuzuia upungufu wa damu (anemia) unaosababisha uchovu na udhaifu. Nyama ya ng’ombe ina vitamini B nyingi, hasa B12, B6, niasini, na riboflavini. Vitamini B12 ni muhimu kwa kazi za neva, afya ya ubongo, na utengenezaji wa chembe nyekundu za damu.Hutoa kiasi kikubwa cha zinki, ambacho ni muhimu kwa kazi ya kinga ya mwili na uponyaji wa majeraha.
Mashirika ya afya yanapendekeza kula nyama nyekundu isiyosindikwa na isiyo na mafuta mengi kwa kiasi (kwa mfano, chini ya gramu 350–455 za uzito uliopikwa kwa wiki) ili kupunguza hatari za kiafya zinazoweza kuhusishwa na ulaji mkubwa, kama vile kuongezeka kwa hatari ya magonjwa ya moyo na baadhi ya saratani. Inashauriwa kuchagua vipande visivyo na mafuta mengi na kutumia njia bora za kupika kama kuoka au kuchoma.”
Haya ni Dkt. John Somi wa huko Lushoto Tanga ambayo yanatumika kama zawadi kwa walaji wa nyama ya ng’ombe yenye mifupa.
Mwanakwetu ninaona kuwa kuna wajibu wa mamlaka husika kulifanyia kazi jambo hili haraka maana ng’ombe zinafungwa jirani iweje bei iwe juu? Hii bei ikiwa ya haki itawasaidia Watanzania masikini kula nyama na ng’ombe na kupata protini za kutosha mwilini ambapo kwa mujibu wa wataalamu wa afya inashauri kwa juma mtu mzima ale angalau grammu 500 ya nyama.
Mwanakwetu Upo? Kumbuka:
“Hata Masikini Tunahitaji Protini.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257






Post a Comment