Adeladius Makwega-MBAGALA
Miongoni mwa wanafunzi wapole sana wa Same Sekondari wakati huo (1994-1995) alikuwa Adeladius Makwega. Jambo hili lilifanya hata Mwalimu wa darasa la Kidato cha tatu B ambalo walikuwa wakisoma masomo ya sayansi na historia lakini hawakusoma Addition Mathematics Miss Yona alimpenda sana Mwanakwetu.
“Yule kijana wa mpole wa Dar es Salaam mwambieni namuita nimtume Same Mjini.”
Mwanakwetu alipofika kwa mwalimu Yona aliyekuwa anasomesha English Language alimtuma mara nyingi mjini Same kuchukua nyama katika bucha fulani ambapo aliposema tu katika bucha hilo kuwa ametumwa na Miss Yona alipewa nyama hiyo na kuifikisha kwa mwalimu huyu aliyempenda sana.
“Katika uchunguzi wa Mwanakwetu alibaini kuwa Miss Yona alizaa mtoto mmoja wa kike na Mbunge wa Same na Waziri wa Elimu wa Tanzania wa zamani Chediel Mgonja ambaye ndiyo alikuwa mmiliki wa mabucha yale ya nyama Same Mjini wakati huo ambapo Mwanakwetu alikuwa anatumwa na mwalimu wake kila mara.”
Mwanakwetu alifika Same Sekondari Julai 1994 ambapo alikariri kidato cha tatu huku wakati huo alitakiwa awe kidato cha nne maana maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati huo walisema,
“Makwega ukienda kufanya mtihani wa kidato cha nne 1994 hautofanya vizuri hivyo basi kwa kuwa tangu Novemba 1993 hakuingia darasani hadi Juni 1994 Kariri kidato cha tatu kisha mwaka 1995 ndiyo utafanya mtihani wa kidato cha nne, tumeshakuombea kibali cha kukariri nenda kasome acheni fujo za Tambaza.”
Haya yalisemwa na miongozi mwa Maafisa Wakuu wa Wizara hii akiwemo Julius Mushi ambaye awali alikuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tambaza.
Mwanakwetu akiwa Same Sekondari baadhi ya wanafunzi walidhani ni mwanafunzi wa kidato cha tano kumbe alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu. Wanafunzi wengi wa Tambaza walikuwepo waliohamishiwa hapo na wengi wao ulikuwa unawatambua maana waliendelea kuvaa sare zao za Tambaza japokuwa walishahama na hata walimu washindwa kuwaambia lolote lile japokuwa shule hii ilikuwa na walimu wakali kama vile mwalimu Mzirai.
Mwanakwetu hakufanya kosa hilo yeye alivaa sare za Same Sekondari kama kawaida ambayo ilikuwa shati jeupe mikono mifupi na suruali ya rangi ya khaki siku zote.
Vijana kutoka Tambaza wanajua Mwanakwetu kaka yao walimuheshimu mno lakini vijana hawa walikuwa watundu kidogo na walikuwa vigumu kuwaonea miongoni mwao, katika kundi hili alikuwepo bwana mdogo mmoja aliitwa Samora Machel, huyu ndugu siku moja alifanya kosa na adhabu yake akapewa kudeki Bwalo la Same Sekondari, akasomewa adhabu yake na wakati wa kudeki bwalo hilo huwa ni usiku baada ya jioni ndiyo unadeki kisha kiongozi atakuja kukagua asubuhi kama ulideki bwalo hilo au la.
Samora Machel alipopewa adhabu hii, jioni wakatoka na vijana wa Tambaza wakaenda Stesheni ya Gari Moshi Same kuchota maji ya kudeki bwalo wakayahifadhi ili usiku wafanya ile adhabu.
Usiku ulipofika muda wa kwenda kujisomea jamaa waliotoka Tambaza isipokuwa Mwanakwetu wakaanza kumsaidia ndugu yao kudeki bwalo, wakadeki wanakaribia kumaliza Samora Macheli damu zikawa zinamtoka puani. Wanafanyaje? Vijana hawa wakampa huduma ya kwanza kisha wakamfuata Mwanakwetu na maamuzi yakawa usiku huo huo jamaa apelekwe Same Hospitali, Same Mjini kwa miguu, safari hii ya shoto kulia hadi Same na walipofika hapo jamaa akapewa huduma ya kwanza usiku huo huo na kurudi bwenini.
Mstarini ikazungumza kuwa Samora Machel hajakamilisha adhabu pia adhabu hiyo alisaidiwa, hivyo adhabu Samora Machel atafanya adhabu hii mara mbili yaani kwa siku mbili kisha aonekana kikaragosi yoyote akamsaidie.
Msomaji naomba utambue kuwa hawa akina Samora Machel na wengine wengi walikuwa kama vijana 60 wa kidato cha kwanza na cha pili huku kaka yao mkubwa ni Mwanakwetu wa kidato cha tatu na hapa Mwanakwetu anakariri kidato cha tatu anafanyaje? Kumbuka zile hekaheka za kutoka Same Sekondari hadi Hospitali ya Wilaya usiku ule mwendo kama wa KM10 kwa mguu Mwanakwetu alikuwepo. Hapa wanafunzi wako mstarini. Mwanakwetu akanyoosha mkono.
“Ni kweli mnatoa adhabu na huyu Samora Machel kafanya kosa lakini unapotoa adhabu ilingane na uwezo binadamu huyo unayempa adhabu. Jana usiku tumehangaika na Samora Machel damu zinamtoka puani KM10 kutafuta tiba hili ni haki? Kama mnatoa adhabu ziwe zile ambazo nyinyi wenyewe viongozi mkipewa kuzifanya mnaweza kuzigusa na mikono yenu.Msitoe adhabu ambazo hata nyinyi wenyewe hamziwezi.”
Mwalimu wa zamu aliyekuwepo mstarini ambaye alikuwa mwanachama cha NCCR MAGEUZI akauliza tukio lilivyokuwa, Mwanakwetu akalisimulia vizuri. Mwalimu wa zamu akasema sawa ni kweli Samora Machel asifanye hiyo adhabu tena huku akiyasema maneno haya:
“Viongozi wa nidhamu hata kama adhabu ametoa Mwalimu wa nidhamu wa shule lakini hiyo adhabu angalia unampa binadamu wa namna gani? Samora Machel mwembamba, kakonda hivi akifa hapa mtaambiwa nyinyi viongozi, mwalimu wa nidhamu na mimi mwalimu wa zamu tumeuwa mnadhani kutuhumiwa kuwa sisi tumeuwa ni jambo jema? Samora Machel usifanye hiyo adhabu.”
Wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita tukatawanyika na kuingia madarasani kila mmoja.
Tukasoma jioni saa 12.00 ya siku hii kengele ya kuhesabiwa ikapigwa tukafika mstarini mwalimu wa nidhamu Mr Mzirai jioni hii akafika laki ni asubuhi yake hakuwepo bila shaka aliambiwa kilichotokea asubuhi. Matangazo yakatangazwa kisha Mr Mzirai akaongea na Wanafunzi wote.
Nani anaitwa Adeladius Makwega? Mwanakwetu akanyoosha mkono. Akauliza Baba Same umefika lini? Mwanakwetu akajibu Julai 1994.
“Baba wewe unatokea Tambaza. Baba hapa ni Same Kilimanjaro, hapa Baba usituletee Udare salaam, ukileta udaresalaam tutakunyanyua juu tutakuweka katika kifuti tutakuwa katika kiganja kisha tutakupeperushwa , ukawa yule yule yule. Baba wewe umemtetea Samora, Baba Usimtete, Samora Machel, Samora Machel ni muhuni wa Dar es Salaam.”
Mwalimu Mzirai alikuwa mkali sana mstarini lakini adhabu ile Samora Machel hakuambiwa aifanye tena.
Kweli mwalimu wa nidhamu aliondoka zake na Mwanakwetu alisoma shule hii hadi kumaliza salama salimini.
Mwanakwetu kwanini ameikumbuka simulizi hii ya shuleni akiwa Mwanafunzi?
Kwa hakika Samora Machel kama alivyofanya adhabu akatibiwa na siye kama tungekaa kimya mara ya pili akafanya ile adhabu na kisha angefariki dunia maana yake sisi wote tulioshuhudia tukio hilo tulikuwa tumeshiriki katika mauwaji ya Samora Machel kwa kitendo cha kukaa kimya, lakini kitendo cha vijana wale wa Tambaza walivyoona hali ni mbaya ya Samora Machel ,damu zinamtoka puani wakamfuata Mwanakwetu darasani, kisha kuamua kwenda Hospitali ya Wilaya ya Same na wakati huo Serikali ilikuwa inatibu wananchi wake bure, bila pesa yoyote na Samora Machel alitibiwa na kurudi shuleni na kesho yake akawa mzima.
Jambo hili ni sawa kabisa na kisa cha kutekwa na kupotea kwa Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Kuba Humphrey Polepole, hapa kwa kiongozi yoyote yule wa CCM kukaa kimya maana yake ni sawa na vile vile kama kwa kisa cha Samora Machel wa wanafunzi wanzake pale Same Sekondari wakati ule.
“Je tutaweza kuzungumzia Usalama wa mtu ambaye hatumfahamu kama tumeshindwa kuzungumzia usalama wa mtu tuliyekuwa naye jirani? Unadhani nani atakuelewa katika hili? Hakuna Atakayekuelewa. Hapa sote tunaonekana hatuna utu na hatuna ubinadamu na sisi ni sehemu ya tatizo.”
Katika kisa hiki wanafunzi waliyokuwa wanatoka mikoa mingine ya Tanzania walisema hawa vijana wa Dar es Salaam, hawa vijana wa Tambaza wanapendana sana , kwanza kaka yao kazungumzia shida ya Samora Machel mstarini hadi jambo hili likawa limekwisha. Hata kama Samora Machel alikuwa mtundu lakini adhabu ya mtundu damu zimtoke hadi afe bila ya kupewa msaada?CCM lazima ijitafakari.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Hakuna Anaye Tuelewa”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257







Post a Comment