Adeladius Makwega-MBAGALA
“Wewe Makwega! Za siku ndugu yangu… sisi huku siyo kwema…rafiki yako, ndugu yangu na mdogo wangu mpendwa Kitindi Ramadhan Langweni amefariki dunia…”
Haya ni majira ya Jioni ya Januari 30, 2026 Mwanakwetu anapokea simu hiyo kutoka kwa ndugu yake anayefahamika kama Iddi Ramadhan Langweni(1961) wa Mwanadilatu, Mipeko Wilayani Mkuranga mkoani Pwani nchini Tanzania akipewa taarifa ya msiba wa ndugu Kitindi Ramadhan Langweni ambaye alikuwa kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilayani Mkuranga huku akiwa pia Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Mipeko ambayo kwa CCM na hata Kiserikali hii ni kata maarufu mno kutokana na kuwa jirani na Dar es Salaam kwa miaka mingi . Mwanakwetu alipopokea taarifa hii kwa huzuni na alitoa pole huku akieleza namna atakavyotuma rambirambi yake , huku akiwa na majonzi haya Mwanakwetu alikumbuka mengi, miongoni mwayo ni huyu Mwenyekiti Kitindi Langweni alifundishwa siasa na Mwenyekiti Mzee Hassan Mohammed Msangule(Maarufu kama Mzee Mao kada maarufu wa TANU na CCM Wilayani Kisarawe.)
Kukumbuka mambo si dhamb:
“Historia inadokeza kuwa maeneo kama vile Mwanadilatu, Tambani, Minaki, Pugu, Kongowe, Mbagala, Vikindu, Mwanambaya, Kisere, Magoza, Kiparang’anda, Dundani na Kisiju ni maeneo ya asili ya koo nyingi za Kizaramo na Kindengereko ambazo vijana wake wengi walikwenda katikati ya Dar es Salaam hata kuvuka Bahari ya Hindi hadi Pemba na Uguja kufanya shughuli kadhaa za kazi ndogo ndogo na hata kuoleana. Jambo la kushangaza maeneo haya kwa asili ni ya makabila mchanganyiko (Cosmopolitan) kama Wahehe, Wabena, Wanyamwezi, Wagogo, Wapogoro,Waluguru, Wamakonde na hata Wamatumbi, hili utaliona kwa kutambua majina ya Koo zao lakini wakizungumza Kizaramo vizruri na siyo lugha zao za mababu na mababu za makabila ya asili.”
Kumbukumbu za Mwanakwetu ziliendelea kuchanja mbuga ya Uzaramoni. Mwaka wa 2009 katika miongoni mwa tafiti za Mwanakwetu katika Kijiji cha Mwanadilatu alibaini kuwa Ukoo wa LANGWENI walikuwa ni jamii ya Wahehe huku ukoo huu ukitaja koo zingine za asili ya Uheheni kama vile MLAWA. Mwanakwetu alibaini ukoo wa LANGWENI walikuwa warefu sana na miili yao ikiwa iliyojengeka.
“Wazee wetu wanadai kuwa tulifika maeneo haya kwa sababu kadhaa ikiwamo biashara ya utumwa na ha ta upagazi wa mizigo ambapo wazee wetu wa asili ya Iringa wakaona na jamii waliyokutana nayo na hapa ndipo na sisi kuzaliwa na kubaki hapa hapa MWANADILATU na sasa sisi siyo Wahehe tena bali ni Wazaramo.”
Haya yalinukuliwa na Mwanakwetu mwaka wa 2009 kutoka kwa Shaaban Langweni ambaye sasa ni marehemu ambaye alikuwa ni mdogo wa marehemu Ramadhan Langweni sasa ni marehemu pia, huku Ramadhan Langweni ni baba mzazi wa Kitindi Ramadhan Langweni huyu aliyefariki Januari 30, 2026 na kuzikwa Januari 31, 2026, huyu huyu aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Mipeko.
Safari ya kukumbuka iligonga mwamba katika haya:
“Ukoo wa LANGWENI ulikuwa una ardhi kubwa wanayomiliki kwa hati za kimila na ulitoa maeneo yao mengi kwa shughuli la kiserikali ikiwamo ujenzi wa shule ikiwamo Shule ya Msingi Mwanadilatu, Zahanati, Misikiti na Makanisa kadhaa ambayo yalipewa maeneo haya kwa kuipa familia hii pesa kidogo.”
Kwa hakika bila ya kusahau Mwanakwetu anakumbuka kuwa mara nyingi alishuhudia vikundi kadhaa vya kuigiza filamu za Kitanzania zilifika Kijijini Mwanadilatu na mwenyeji wao alikuwa ni Kitindi Ramadhan Langweni huku akiruhusu waingizaji hao wa filamu Tanzania na hata nje ya nchi baada ya kupata vibali kutumia nyumba za wanavijiji hao na mashamba yao kuigiza ili kupamba mandhari halisi ya kijijini. Mara baada ya Mwanakwetu kuyakumbuka haya yote, ndipo alipoamua kuyaandika yote katika makala haya unayoyasoma msomaji wangu siku ya leo.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu kwa heshima ya familia hii na mchango wake wa kutoa ardhi yao bure kwa miradi ya kiserikali na hata kutoa ardhi hii iwe bure au kwa pesa kiasi kwa kujengwa makanisa (Enzi za Padri Wolfram) katika eneo hili ambalo awali halikuwa na makanisa na ndiyo maana Mwanakwetu aliamua kuyaandika makala haya, maana haya yote Mwanakwetu ameyashuhudia kwa macho yake.
Mwanakwetu anatoa pole kwa familia ya Langweni ya Mwanadilatu ikiwamo ndugu wote mkewe na mtoto wake mmoja.
Mwanakwetu Upo ? Kumbuka:
“Buriani Kitindi Langweni.”
0717649257


.gif)
Post a Comment