BURIANI CPA SHAABAN NDALU

 

Adeladius Makwega-Musoma MARA.

“Bosi kumbe upo? Leo asubuhi nimeona gari lako linaingia, nikasema bosi wangu kumbe amerudi likizo? Bosi kumbe yupo! Heri yako wewe umeenda likizo Mungu amekujalia umeenda kwenu umerudi salama lakini mwenzetu CPA Shaamban Ndalu ameenda hajarudi, ameenda likizo amefariki dunia… ”

Haya ni maelezo ya wafanyakazi wawili wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Maisha Mwanisegele na Mwalimu Kinyemi Sepeku wakizungumzia juu ya Kifo cha mtumishi mwenzao CPA-Shaaban C.Ndalu Mhasiku Mkuu wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara aliyefariki dunia mwishoni mwa mwezi wa Januari 2026. Mwanakwetu alipoyasikia maelezo haya alifunga safari hadi katika dawati la ndugu Shaaban Ndalu ambalo lipo chumba namba F14, Uhasibu sakafu ya pili ya jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

“Hapa Mwanakwetu alikaribisha na meza na kiti cha mti wa mninga. Kiti kikiwa kimegusanishwa na kuumana kabisa na meza, kuonesha kuwa mwenye samani hizi hapa kazini hayupo, huku nyaraka za serikali zikionesha kuwa yu likizo.

Kiti, meza, kompyuta na nyaraka mezani hazijui kuwa CPA-Shabaan Ndalu amefariki dunia huko Jijini Dodoma.

Mwanakwetu akitamani kunadi kwa sauti ya juu ‘asalaam aleikuum samani za chumba hiki, kwa unyonge, upole na unyenyekevu nimekuja kuwajulisha kuwa ndugu yenu CPA Shaaban Ndalu mwili wake umeagana na roho huko Dodoma.”

Maneno haya ya Mwanakwetu akiwa chumba cha F14 yalitamkwa kimya kimya, kimoyo, moyo na kisha kuzipiga picha samani hizo na kutoka zake. Mwanakwetu akiwa sakafu ya pili alikutana na ndugu Hashimu Ujonjo ambaye ni mhasibu hapa ofisini na yeye alisema kuwa CPA-Shaaban Ndalu akiwa hai jukumu lake kubwa alikuwa anafanya ukaguzi (examination) wa nyaraka za malipo kabla malipo yoyote kufanyika:

“Hapa kaka yetu alikuwa anakagua kama tunamlipa mtumishi XXZ shilingi XCCCCD je malipo haya yana nyaraka zote za uhalali wa malipo ?”

Jukumu hili linasaidia kutunza rasilimali fedha zitumike kwa usahihi na hata taasisi kupunguza hoja za ukaguzi, iwe ukaguzi wa ndani au ukaguzi wa nje, alimalizia maelelezo yake Ndugu Unjonjo.




 

Mwanakwetu alifunga safari hadi Ofisi ya Katibu Tawala Msaidizi Anayeshughulikia Utawala na Rasilimali watu Ndugu Dominicus Lusasi hapa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na yeye alisema haya:

“Ni kweli tumepata msiba huo ambapo CPA Shabaan Ndalu amefariki dunia usiku wa kuamkia Januari 30, 2026 huko Dodoma. Taarifa zake katika makabrasha yetu zinaeleza kuwa alizaliwa Julai 11, 1975 huku Chibelela Bahi Dodoma, alisoma Shule ya Msingi Chibelela(1984-1990) kisha akafaulu kwenda Azania Seondari(1991-1994) na baadaye kujiunga na Mazengo sekondari (1995-1997), kisha alijiunga na Stashahda ya  Uhasibu Chuo cha Fedha (IFM) kati ya mwaka (2001-2004) huku mwaka(2005-2006) alisoma Diploma ya Juu ya Uhasibu na Fedha na mwaka wa 2007 alipata Cheti cha Awali cha Uhasibu wa Umma (CPA).”

Ndugu Lusasi alisema kuwa CPA Shaaban Ndalu ni Mkristo ameacha mjane na watoto watatu Doreen Ndalu, Hilda Ndalu na Shedrack Ndalu na taratibu za mazishi zinafanyika huko huko Mkoani Dodoma wakishirikiana kwa karibu baina ya familia ya marehemu na ofisi yao.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu anatoa pole kwa familia na wafanyakazi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kumpoteza ndugu na mfanyakazi mwenzao. Mwanakwetu anamfahamu vizuri CPA Shaaban Ndalu, huku akikumbuka swali hili:

“Kaka mbona malipo yangu ya uhamisho sijayapata …”

Majibu ya CPA Shaaban Ndalu yalikuwa haya:

“Hapa katika dawati langu ninayakagua, sijaona nyaraka zako kadhaa ikiwamo vyeti vya watoto, hakikisha kila malipo unayotarajia kuyapokea weka nyaraka husika…”

Bwana Ametoa, Bwana ametwaa , Jina la Bwana Lihimidiwe Amina. Mwanakwetu upo? Kumbuka:

“Buriani CPA SHAABAN NDALU.”

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 


 

 


0/Post a Comment/Comments