Haya yalikuwa ni majira ya jioni sana, huku magharibi ilishavuka, kama tungekuwa jirani na msikiti basi mnadi sala kesha nadi na Waislamu wamesali Salat Magharibi na sasa wanarudi majumbani mwao na kama ungekuwa mwezi wa Ramadhani basi wale wa imani hiyo na waliofunga, wakikamilisha nguzo moja ya dini yao wangekuwa wameshapiga pafu hata tatu za uji wenye pilipilimanga na hamdalasini na matonge kadhaa ya futari, yanayolisalimu kinywa kilichokosa chakula kwa saa zaidi ya 12 kwa Imani.
Njiani zilipitiwa taasisi kadhaa za umma ambazo ndizo zilizopamba njia hii. Mwanakwetu na nduguye wanarudi nyumbani kwao.
Ndugu huyu wa Mwanakwetu akasema :
“Kaka leo nataka nikanunue korosho maana sijala korosho muda mrefu, huku siyo kama kwetu Pwani, mwaka unaweza kupita bila ya kula korosho.”
Hapa sasa Mwanakwetu na nduguye wanakwenda pahala zinapouzwa korosho na wakiwa wanakwenda hapo Mwanakwetu akasema;
“Haya maduka yote unayoyaona ni ya watumishi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama. Mimi hili nilikuwa silifahamu lakini wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata wafanyabiashara wengi wa maduka mengine yalifungwa lakini maduka haya yalikuwa wazi. Siku hiyo nilinunua bidhaa katika maduka haya na nilipomuuliza muuzaji una nguvu gani inayokufanya uweze kufungua duka katika kipindi hiki cha hali ya hatari? Muuzaji alijibu akisema ‘mzee line yote hii unayoiona ni na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa usalama ni mkubwa.”
Kwa ukweli wa Mungu maduka haya yaliwasaidia mno watu wa mji huo kipindi cha hali ya hatari.
Tukafika dukani, ndugu Mwanakwetu akanunua nusu kilo mbili za korosho nayeye Mwanakwetu akanunua kilomoja ya korosho na tende pakiti mbili.
Mwanakwetu akasema;
“Dada hizi korosho ni nzuri nikitaka kuzipata nikiwa mbali nitazipataje? Naomba namba ya simu.”
Dada muuzaji ambaye alikuwa amekata nywele , mweupe na mavazi yake ya kawaida akajibu:
“Namba yangu ya simu ipo katika pakiti ya korosho hizi.”
Jamaa kando ya Mwanakwetu akasema unataka kumpiga simu ? Unataka aulizwe kwanini anafanya mawasiliano na raia? Maana hawa askari sisi wanatuita raia.
Mwanakwetu akamuuliza huyu dada kwani wewe ni askari? Binti huyu akajibu:
“Mimi nipo kwa afande RCO.”
Mwanakwetu akasema sasa dada nikipiga simu kwako kisha akapokea Afande RCO itakuwaje? Dada huyu akajibu mjibu hivi:
“Afande RCO Nimempigia Simu Huyu Dada Nataka Anikamatie mhalifu, maana huyu mhalifu ananisumbua sana huu ni mwaka sasa.”
Kwa hakika jioni hii dada huyu alifanya biashara sana maana manunuzi ya Mwanakwetu na ndugu yake yalikuwa yanafikia karibu laki moja.
Afande RCO Usione Gere maana kama karani wako au afisa mpelelezi wako anapendeza kazini tambua anafanya biashara vizuri huku mtaani maana akina Mwanakwetu wanamuunga mkono katika biashara yake ya korosho. Wakati tunatoka ndugu wa Mwanakwetu akasema:
“Kumbe kaka ulisema kweli kumbe hapa wamejaa wenyewe tu.”
Mwanakwetu akacheka kisha akasema mimi ni mdau wa Jeshi la Polisi Tanzania, wako vijana wa polisi wanaweza kumsumbua Mwanakwetu lakini hawana kibali cha kunipoka udau wangu kwa jeshi hili. Mwanakwetu akaongeza na hili:
Ukimtazama mwanamke anayefanya kazi na vyombo vya ulinzi na usalama ni nyepesi sana kumfahamu kwanza lugha zake anazotumia mathalani Afande RCO, wanakuwa na maneno machache, wanakuwa wajanja wajanja sana lakini maumbile yao mabega yao huwa yanafunguka–yanakaa upande kwa sababu ya mafunzo ya kijeshi na kubeba silaha.
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu na nduguye wanarudi nyumbani, huyu ndugu wa Mwanakwetu akasema anakwenda benki, naye Mwanakwetu akasema yeye anawahi nyumbani kwake.
Mwanakwetu akapanda bodaboda huyu na safari yak wake ikaanza. akiwa njiani akamkumbuka rafiki yake mmoja Afande Advocate Nyombi ambaye aliwahi kuwa RPC Mbeya na RPC Iringa.
“Afande Advocate Nyombi alikuwa ni polisi wa aina ya pekee sana huku akishirki vizuri katika shughuli za kijamii. Hata jamii ya watu Iringa ilimtambua askari huyu kwa tabia zake njema na ujirani nao kwa hiyo alikuwa anapokea mialiko mingi hata ya wanamuzki wakifika Iringa Advocate Nyombi ilikuwa lazima apewe mualiko na akipewa mualiko lazima awepo yeye na mkewe. Akiwa katika ukumbi hauwezi kuamini kama ni askari alijichanganya vizuri huku akicheza muziki kwa uhuru.
Nikiwa Iringa kama kiongozi kutoka Serikali ya Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa mara nyingi tulimualika Advocate Nyombi katika matamasha kadhaa na alikuwa anakuja yeye na mkewe.
Siku moja nilipeleka mualiko ofisini kwake, RPC Nyombi alikuwa na karani wake mama mmoja mzee lakini alikuwa mrembo sana. Mwanakwetu nilikwa nampenda sana huyu mama ambaye alikuwa pia askari na kila nikifika nilikuwa namtania.
‘Mama nimekuja kuleta mualiko wa RPC lakini Naomba Niongee Kwa Sauti ya Chini RPC Asisikie asije akaniweka ndani. Sasa mwambie RPC, Makwega kaleta mualiko tuna tamasha chuoni, anakuja Jackline Ntabaliwe, Banana Zoro, Mr Blue na TID sasa najua Afande Advocate Nyombi atakuja na mkewe, mimi naomba ruhusa mapema mimi niwe na wewe.’.
Kumbe Advocate Nyombi anasikia maneno ya Mwanakwetu kwa Karani wake. Nilipomaliza vituko hivyo karani akaingia kwa RPC Advocate Nyombi, mama karani akatoka akasema RPC anakuita, mlango upo wazim mara RPC akasema – we Makwega, we mwandishi wa habari, we mwanaCCM njoo. Mama karani akaongeza akasema Makwega unaitwa na RPC. Nikaingia ndani
‘Makwega kilio chako nimekisikia, nimetoa kibali, kesho jioni utaambatana na Karani wa RPC katika tamasha lenu na vijana wangu watakupa ulinzi.
Kweli siku ya Tamasha la Tumaini Night of Talent ilifika, RPC Advcoate Nyombi yupo mbele na mkewe, RPC kavaa cheni inaning’inia, sare kaweka kando naye Mwanakwetu Sambamba na Karani wa RPC.
Kweli maisha yalikuwa mazuri sana.
Baadaye Afande Advocate Nyombi alihamishiwa Mbeya na ndipo kipindi hicho hicho Iringa ikapata RPC mpya na kibaya zaidi Iringa chini ya RPC mpya ndipo Kifo cha mwananahabari Daudi Mwangosi kilitokea.
Tukio la kifo cha Daudi Mwangosi ilikuwa ngumu sana kutokea wakati wa RPC Advocate Nyombi maana alikuwa polisi kamili, polisi hodari na alikuwa anajua sana kukaa na jamii yake anayoifanyia kazi.”
Swali analojiuliza Mwanakwetu hadi kesho, hana hakika kama mahusiano baina ya Polisi na wanahabari mkoani Iringa na maeneo mengine kwa sasa kama yanaweza kufikia kama enzi ya RPC Advocate Nyombi mkoani Iringa.
Kumbuka msomaji wangu haya Mwanakwetu anayakumbuka tu akilini mwake akiwa juu ya pikipiki baada ya kuagana na nduguye nayeye akirudi nyumbani kwake yu juu pikipiki.
Kisha Mwanakwetu kuamua kuyaweke yote haya ya siku hii katika makala haya unayoyasoma msomaji wangu.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika Tanzania ya sasa na ya mara baada ya Oktoba 29, 2025 mahusiano baina ya polisi na raia yamezorota sana.
Polisi ni jamii ya Watanzania, IGP ili awe vijana wa Polisi lazima jamii itoe vijana wao na ndipo wamfikie IGP, huko sasa yeye anawapa mafunzo ili waweze kupata uthabiti ili waweze kulinda raia na mali zao.
Katika makala haya Polisi mkubwa aliyetajwa na Afande Advocate Nyombi angalia alivyokuwa anakaa vizuri na wananchi wa Iringa. Kitu kimoja kizuri hata mikutano yake na wanahabari Afande Advocate Nyombi alikuwa anatoa taarifa za kuvutia sana, Vijana wa RPC Watapanda miti, leo vijana wa RPC watatembelea hospitali, Leo unakuja ugeni mkubwa wa wanamuziki kadhaa usalama utakuwepo. Mara chache sana alizungumzia mambo mabaya mabaya.
Kwa kuwa Mwanakwetu ni mdau wa Jeshi la Polisi Tanzania anaomba leo aishie hapa.
Mwanakwetu upo?
Je makala haya yaitwaje?
Mwanakwetu Sambamba na Karani wa RPC? Naomba Niongee Kwa Sauti ya Chini ili RPC Asisikie? Afande RCO Usione Gere au Samahani Afande RCO Nimempigia Simu Huyu Dada Nataka Anikamatia Mharifu? Mwanakwetu anachagua Afande RCO Usione Gere.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257













Post a Comment