Adeladius Makwega-MBAGALA
Huu ni wasaa mwingine wa siku nyingine, nakualika tena katika Makala ya Katuni siku ya leo. Kumbuka haya ni Makala ya Uchambuzi wa Katuni kama zilivyochorwa na kuzingatiwa na wachoraji mbalimbali.
Hapa Mtayarishaji wetu huchagua katuni nne huku moja baada ya nyingine huielezea namna ilivyo kisha kuichambua kwa jicho la mtayarishaji wetu.
Kuyaanza makala haya Mwanakwetu sasa anaikamata katuni ya kwanza iliyochorwa na Said wa Michael ambapo katuni zake hupachika katika ukurasa wa mitandao ya kijamii ya Shirika la Utangazaji la Ujerumani DW KISWAHILI.
Hapa kunaonekana jamaa mmoja aliyefunguliwa zulia lake jekundu lililopewa kibandiko MADARAKA akilikanyaga kwa madaha, jamaa huyu kiongozi uchwala anaonekana kama kiongozi wa SUDAN vile, chini ya zulia hili wapo binadamu wanakanyagwa na kuuawa huku damu zikimwagika kwa mkanyago huo sakafuni.
“Lo salale, wewe baladhuri, wewe mshenzi, kwanini haujali utu wa binadamu?”
Jamaa huyu anaelekea kuyakalia madaraka. Kando ya bwana mkubwa huyu wapo ndege wanamuhesabia hatua anazopiga moja, mbili tatu… Huku mwingine akisema:
“Mzee bado nusu ya safari.”
Mwanakwetu anaitazama katuni hii kwa kina akijiuliza kama mkubwa huyu nusu ya safari ya madaraka yake ameimaliza je akiimaliza safari yake mapipa mangapi ya damu yatamwagika?
“Hii ni hali ya siasa za huko Sudan lakini taswira ya mfano ya mataifa mengi ya Afrika kuwa viongozi wanapokuwa madarakani wamekuwa wakitumia nguvu kubwa na kusababisha wananchi wao kuumia na hata kufariki kwa sababu ya kuyang’ang’ania madaraka tu.
Jamani hili siyo jambo zuri maana unapomwaga damu ya wananchi wako wenyewe tambua hili linakaribisha chuki zaidi, hasira zaidi, kususia kazi za umma na damu zaidi kumwagika na hata wewe mwenyewe kiongozi tambua kuwa damu yako inaweza kumwagika muda wowote ule.”
Mwanakwetu anaivuta kwa mikogo katuni yake ya pili ambayo imechorwa na Masoud Kipanya hapa kunaonekana bulidoza moja kubwa likiwa njiani linatengeneza barabara huku mchoraji hajasema hii ni barabara ya wapi.
Mwanakwetu anaona kama Ingekuwa bora kama hili bulidoza lingekuwa linatengeneza barabara ile ya Mahenge Ketaketa-Ulanga Morogoro, ukifika Misheni hakupitiki tangu mvua zibomoe daraja hili miaka kadhaa nyuma huko Morogoro.
Katika katuni hii nyuma ya bulidoza njia ni nyeupe, imeshakuwa vizuri lakini mbele yake bulidoza hili linakanya miti midogo midogo. Bulidoza Baladhiri linakanyaga miti midogo tu bila huruma huku nguvu kubwa ikitumika kuikanyaga miti dhaifu.
Mtayarishaji wetu anaona kuwa:
“Hapa kinachoelezwa ni matumizi ya nguvu kubwa kupita kiasi inayofanywa na Serikali dhaifu mara baada ya kukosa ushawishi, zinatumia maguvu kupitia vyombo vya Ulinzi na Usalama ambalo hili ni jambo baya.
Viongozi dhaifu wanajisahau kuwa jeshi linatokana na watoto wa hao hao unaowatesa. Hakuna chombo ca Uienzi na Usalama ambacho kinamashine ya kuwafyatua binadamu kama vifaranga vya kuku, huku fedha unazotumia ni hizo hizo za unawatesa ambao ndiyo walipa kodi, unadhani unaweza kufanya uonevu muda mrefu?
Utafanya uonevu muda mfupi, kisha nguvu hizo hizo ulizozitumia wale unawatuma watakugeuka zinakugeukia na kukurudia wewe mwenyewe.”
Katuni hii ya bulidoza inatoa nafasi ya kuikamata katuni ya tatu inayoonesha taswira ya mwanamke juu ya ramani ya Tanzania, huku akifanya usafi kutoka Mikoa ya Kaskazini kuelekea mikoa ya Kusini ya Tanzania na hapa anaonekana yu katikati ya ramani ya taifa hili. Huku kile kinachoonekana kuwa uchafu ni maandamano na vurugu katika taifa hili huku viungo vya binadamu kama vile mifupa na mafuvu yakifagiliwa haya yote ni kutokana na kile kilichotokea Oktoba 29, 2025, huku mfagiaji huyu akitaka taifa hili liwe safi kabisa. Kulingana na jicho la mtayarishaji wetu huyu anayefanya usafi ni Rais wa Tanzania kwa mwaka wa 2025, swali la kujiuliza je huu usafi utafanikiwa?
Je ndugu wa hao ambao sasa na mifupa na mafuvu wamelipokeaji hali hii na je Tanzania itabaki kuwa salama?
Mwanakwetu anaamini haya:
“Usalama wa Tanzania mara baada ya Oktoba 29, 2025 ni mdogo sana, hali ya taifa hili itaendelea kuzorota kila siku inayokwenda kwa Mungu maana viongozi wote walio katika nafasi ya juu wamebeba mzigo wa lawama kwa yalitokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata, huku wamekuwa wazito kuungama wazi na kuomba msamaha hadharani, lolote linaweza kutoka nchini Tanzania.
Kikubwa viongozi wa juu wamepoteza mvuto, wamebeba mizigo na mafurushi ya lawama ambayo kwa sasa hakika inahitaji majina mapya ya viongozi wapya kushika jalife la uongozi.”
Mwanakwetu sasa anaikamata katuni ya nne na ya mwisho ambayo imechorwa na Said wa Michael WAKUDATA na kutumiwa na Shirika la Utangazaji wa Ujerumani DW KISWAHILI. Hapa kunaoneka Gari ndogo kama kama Kenta inamadumu makubwa ya maji juu, huku ikisaka maji mtaani jijini Dar es Salaam, jambo baya zaidi gari hili ni la mamlaka ya maji ambao walikuwa na wajibu wa kufanikisha maji yanatoka lakini hali kinyume wao wanayasaka maji mtaani.
Maneno yakisika mvua kidogo maji yanatapakaa mitaani lakini maji hakuna katika mabomba. Mabomba hayatoi maji huku jamaa akiwa na madumu kadhaa anauza maji. Jamaa mmoja anasema shida ya maji ikitokea jamaa wanaonunua maji wao hawaulizi maji haya yanatoka wapi?
“Katuni hii inazungumzia tatizo la Maji katika jiji la Dar es salaam ambalo linategemea sehemu kubwa ya maji yake kutoka Mto RUVU ambapo hili ni tatizo la nchni nzima. Kwa hakika tatizo la Maji jijini Dar es Salaam ni kichekesho maana Dar es Salaam ipo kando ya Bahari ya Hindi huku mito mingi ya Dar es Salaam inamwaga maji yake Bahari ya Hindi.
Kwa Tanzania ipo mito kadhaa mikubwa kwa midogo inayomwaga maji yake Bahari ya hindi , kwa mito mikubwa ni Pangani, Rufiji, Ruvuma (Mozambiki) na Wami.Msimbazi na Wami inakatisha katika mipaka ya Mkoa wa Dar es Salaam au jirani. Ndani ya haya ipo mito kadhaa inayomwaga maji yake Bahari ya Hindi ambayo ni Mzinga, Kizinga, Mpiji na Mzimbazi huku Mpiji niMto wa msimu.
Swali ni je Mamlaka za Maji Dar es Salaam na Mamlaka za Tanzania zimejizatiti kweli kulitatua taizo la mji kwa jiji hili? Uwepo a Mto Mpiji unategemea sana mvua maana yake Dar es Salaam mvua zinanyesha. Dar es Salaam ina misimu miwili ya mvua ambayo ni Masika na Vuli.Vuli ni kwa Oktoba,Novemba, Disemba hadi Januari nayo Masika ni kwa Machi , Aprili na Mei.
Ukipiga hesabu ya jumla ya miezi mvua inayonyesha Jijini Dar es Salaam ni miezi nane swali ni je Dar es Salaam kukosa maji ni haki na tukisema Dar es Salaam kukosa maji ni Kichekesho tutakuwa tumefanya kosa?.
Kosa moja kubwa ambalo limefanywa na Serikali ni pale iipoacha kusisitiza UVUNAJI WA MAJI YA MVUA MAJUMBANI na kusisitiza kila nyumba kuunganishwa na maji ya Bomba kutoka Mamlaka za Maji. Hapa ndipo Serikali ilimkanygaa kifa urongo, sasa Dar es Salaam ina watu wengi. Jambo la msingi kwa Serikali siyo kukusanya kodi za maji tu bali wana wa Dar es Salaam wawe na njia bora za kuyapata maji safi na salama, kisha ndipo hoja ya kodi na tozo za maji zije. Kama Watu wa Dar es Salaam wangekuwa wanavuna maji ya mvua katika matenki yao wasingetaabika pale maji yakikatika, lakini kwa sasa hakuna mahimizo ya kuvuna maji ya mvua baadhi ya wajanja waliona kuwa hili litalinyima taifa mapato, lakini sasa tumeshindwa kuwapa maji wananchi, afya zitazorota na hata magonjwa ya matumbo yanaweza kutokea mara dufu Serikalia itawapa mzigo wananchi kujitibia magonjwa haya huku huduma za afya siyo bure. Pesa ni karatsi tu umuhimu ni maisha salama na yenye kuzingatia uhai wa binadamu, Swali la kujiuliuza Mamlaka za Maji ya Mikoa zimetumia kiasi gani katika kuwekeza miundombinu ya wananchi kuvuna maji ya mvua?”
Kutatua uhaba wa maji Jijini Dar es Salaam ambapo ndipo nyumbani kwa akina Mwanakwetu hasa kule Mbagala hii sera ya uvunaji wa Maji ya mvua irejeshwe mara moja tangu ngazi ya familia na taasisi za umma.Kila nyumba inayojengwa lazima iwe na iwe na mfumo wa kuvuna maji ya mvua na tenki kubwa la kuhifadhi maji hayo.Hayo maji ya Mamlaka hata yakikatika kwa wiki wananchi kila mmoja atakuwa na maji ya dharura huku mamlaka za maji zitatumia muda huo kuboresha miundombinu yake huku maisha ya wananchi yataendelea.
Basi hadi hapo msomaji wangu ndipo na mimi nafika tamati ya Makala ya Katuni siku ya leo , kumbuka kulikuwa na katuni nne : ile ya zulia, Ile ya mama mfagizi na hata ile ya Bulidoza na katuni ya nne hii ya tatizo la Maji jijini Dar es Salaam ambayo ndiyo iliyoyajenga na kuyafunga Makala ya Katuni siku ya leo.
Mwanakwetu upo?Kumbuka:
“Rejesheni Mara Moja Ari ya Uvunaji Maji ya Mvua”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257













Post a Comment