Adeladius Makwega –Musoma MARA
Disemba 12, 2025 Mwanakwetu alikuwa katika katika dawati lake hapa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, huku akiendelea na shughuli zake za hapa na pale. Akiwa hapo alipita mzee mmoja mwenye umri wa kukaribia kustaafu akawasalimu kisha, kisha na kisha kutoa neno kutoka Biblia Takatifu kwa mzee mwenzake na kusema maneno haya:
“Hatimaye, ninyi nyote muwe na nia moja, mhurumiane, mpendane kama ndugu, muwe na mioyo ya upole na ya unyenyekevu. Msilipe ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; ila barikini kwa maana hili ndilo mliloitiwa na Mungu, mpate kurithi baraka.”
Mzee huyu alimwambia mzee mwenzake:
“Hili ni neno la leo kwako, naomba ulisome sana na ulitafakari na linatoka katika Kitabu cha 1 Petro 3, 8-9.”
Masikio ya Mwanakwetu ni hodari wa kusikia, alinukuu aya hiyo ya Biblia na kisha kuamua kuyatayarisha makala haya unayoyasoma msomaji wangu. Jina la mzee huyu anaitwa Richard Magoiga ambaye ni Msaidizi wa Ofisi Mwandamizi katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Mwalimu Gerald Musabila Kusaya.
Taarifa za kiutumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara zinadokeza kuwa ndugu Richard Magoiga ndiye mtumishi pekee katika Mkoa wa Mara ambaye alifanya kazi tangu ngazi ya Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na baadaye mwaka 2023 akahamishiwa Ofsi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara yaaani katoka Kijijini hadi Mkoani.
Richard Magoiga alizawa Oktoba 8, 1967 Mkoani Mara huku aliajiliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara (RDD) mwaka 1988 ambapo hadi makala haya yanatayarishwa mchana wa Disemba 12, 2025, Mzee Magoiga ana maiaka 37 kazini huku akitarajiwa kustaafu rasmi Utumishi wa Umma Oktoba 2027.
“Unajua utumishi wa umma wa sasa una nafuu, mie nakumbuka mwaka 1988 hali ilikuwa ngumu hasa wakati wa kukusanya kodi, yaani ilibidi watumishi mtembee na mapanga kiuononi kukusanya kodi wakati huo hata polisi walikuwa wachache, siku hizi kodi mnakusanya kwa mfumo hii ni raha kubwa.”
Mzee Magoiga alimwambia mzee mwezake kando kuwa analikumbuka tukio hili;
“Nikiwa naanza kazi kijijini nilikuwa na Mwenyekiti wa Kijiji Jangili, Jambazi na Mwizi wa ng’ombe za watu, hali ilikuwa ngumu kila mnalolipanga kupambana na majangili lilikuwa halikamiliki maana nia yake ilikuwa kwingine na sie Watumishi wa Umma nia zetu zilikuwa kwingine. Haki na Udhalimu haivikai pamoja, Lazima katika kazi nyote muwe na nia moja?”
Mwanakwetu alisikiliza mazungumzo ya wazee hawa, Mzee Magoiga alipoondoka Mwanakwetu alilinganisha kisa cha Mwenyekiti jangili na aya hii ya 1 Petro 3, 8-9.
“Hatimaye, ninyi nyote muwe na nia moja, mhurumiane, mpendane kama ndugu, muwe na mioyo ya upole na ya unyenyekevu. Msilipe ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; ila barikini kwa maana hili ndilo mliloitiwa na Mungu, mpate kurithi baraka.”
Mwanakwetu upo? Je makala haya yaitwaje? Mwenyekiti Jangili, Nyinyi Nyote Muwe na Nia Moja au Kutoka Kijijini Hadi Mkoani?
Vichwa vyote Mwanakwetu kavipenda kikubwa msomaji wangu kumbuka Nyinyi Nyote Muwe na Nia Moja.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257










Post a Comment