Adeladius Makwega-MBAGALA
“Leo ni Jumapili ya nne na ya mwisho ya Majilio. Katika siku chache zijazo, itakuwa Sikukuu ya Krismasi, sherehe yetu ya kuzaliwa kwa Bwana. Maandalizi yako wewe unayeyasoma makala haya yakoje?
Tunaweza kujifunza jambo nzuri kutoka kwa Mtakatifu Yosefu katika Injili ya leo. Malaika alimtokea Yosefu katika ndoto akimwambia,
‘Mzee Usiogope.’-Lo salale!
Sasa kwa nini malaika anayasema haya?
Kwa sababu wakati huo Yosefu na Maria walikuwa tayari wamechumbiana, ambalo katika utamaduni wao ilikuwa hatua ya kwanza ya ndoa. Hata hivyo, kabla hawajaishi pamoja, Maria alionekana kuwa na mimba. Yosefu akaamua kumwacha kwa siri Bikira Maria.
Astaghafilulai! (Mungu Amsamehe)
Lakini malaika alimfunulia kwamba mtoto aliyekuwa ametungwa ndani ya Maria alitungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, na mtoto huyu atawaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.
Mashallah.
Ndugu zangu Kujua kuhusu ujauzito wa Maria lazima kulimtisha sana Yosefu. Hapa Maria angeweza kushitakiwa kwa uzinzi, adhabu yake ikiwa ni hukumu ya kifo-eheee Hukumu ya Kifo,pia lazima alikuwa na hali ya kuogopa kwa kujua kwamba mtoto aliyekuwa tumboni mwake alikuwa Mwana wa Mungu na hivyo Yosefu alipoamka alifanya uamuzi wa kumchukua Maria, mke wake, aingie nyumbani mwake.
Yosefu alimpenda Mungu na Maria kwa upendo ulioshinda hofu yake. Alitii kwa imani na kutenda kulingana na neno la Mungu.
Ndugu zangu, je, tunaogopa kupenda na kushiriki katika kazi ya Mungu?
Sasa tuelekeze macho yetu kwa Yosefu, ambaye upendo wake ulishinda hofu, eeeh upendo wake ulishinda hofu na ambaye imani yake iliongoza utiifu wa haraka.
Mtakatifu Yosefu, utuombee na pia na sisi watoto wako. Amina.”
Msomaji wangu haya ni sehemu tu ya mahubiri ya Kadinali Luiz Antonie Tagle Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki Inayojihusisha na Uinjilishaji wa watu Ulimwenguni yenye Makao Makuu pale Vatikani.
Mwanakwetu pia alitembelea Ukuta wa Redio Vatikani kujua je unatafakari gani juu ya Dominika hii?
Redio Vatikani walikuwa na tafakari ndefu yenye aya zaidi ya 10, ikiwa na aya zenye sentensi ndefu ndefu huku awali mtayarishaji wa tafakari hii Padri Bonaventura Maro alilichekecha vilivyo KAYAMBA homilia yake kwa kusema maneni haya:
“Utabiri wa Nabii Isaya unakuja wakati taifa la Yuda yaani ufalme wa Israeli kusini, walikua katika mgogoro mkubwa sana wa kisiasa (Syro-ephramite Crisis 734-732BC). Mataifa ya Aramu (Syria) na Israeli yaani Ufalme wa Kaskazini (Ephraim) waliungana na kutaka kuivamia Yerusalemu na kuuangusha ufalme wa Kusini, yaani Ufalme wa Yuda. Mfalme wa Yuda, Mfalme Ahazi pamoja na watu wake waliingiwa na hofu, mashaka na mahangaiko makubwa sana. Katikati ya hali hii, Mwenyezi Mungu anamtuma Nabii Isaya kumwambia Mfalme Ahazi kwamba, hakupaswa kupaniki, hakupaswa kuwa na hofu kwa kuwa Mwenyezi Mungu hatauacha mji wa Yerusalemu kuvamiwa na kuangushwa. Mwenyezi Mungu kupitia Nabii Isaya anamwambia Mfalme Ahazi aombe Ishara yoyote kutoka mbinguni, kama uthibitisho kwamba Mungu yupo pamoja nao. Lakini Ahazi anakataa kuomba Ishara, akisema kwamba,
‘Sitaitaka wala sitamjaribu Bwana’
Mfalme Ahazi alijifanya kwamba hakutaka kumjaribu Bwana lakini kimsingi hakua na Imani, wala hakumtumainia Mungu wa Israeli. Kinyume chake alikwishaanza kuwaza kutafuta msaada kutoka kwa taifa kubwa la Waashuru badala ya kumtegemea na kumtumainia Mungu lakini Nabii Isaya anamhakikishia kuwa hata kama yeye alikataa kuomba Ishara, bado Mungu atatoa Ishara.
Ni ishara gani hiyo?
Somo hili ni utabiri juu ya Ishara ya Imanueli. Kwamba Bikira atachukua Mimba, naye atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli, yaani Mungu pamoja nasi.
Mungu hawaachi kamwe watu wake, licha ya udhaifu wao, licha ya Imani haba na mashaka, anakuja Katikati yao, anawaletea ukombozi.”
Haya ni dominika hii kutoka kwa Padri Bonaventura Maro wa Austria na awali ni Kutoka kwa Kadinali Luiz Antonie Tagle wa pale Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki inayojihusisha na Uinjilishaji wa watu Ulimwenguni.
Wakati haya ni ndani ya kuta za Kanisa hali ya hewa ya Mbagala , Temeke Dar es Salaam nyumbani kwa Mwanakwetu ni nyuzi joto 29, unyevunyevu ni wa asilimia 20 ujirani na mvua ni wa asalimi 73 na huku upepo ukivuma kwa KM 10 kwa saa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka?
“Mzee Usiogope.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257.











Post a Comment