Adeladius Makwega-MBAGALA
Kwa muda wa siku mbili yaani Disemba 11&12, 2025 Mwanakwetu amekuwa akimtafakari Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Ndugu Albert Chalamila ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa mzuri sana, mwenye ushawishi mkubwa, enzi za Rais John Pombe Magufuli lakini kwa sasa jina hilo linaonekana limepokwa na Mwenyenzi Mungu nguvu ya ushawishi, viganja vyake vya mikono yake miwili Mnyalukolo huyu vimebeba tuhuma tele za kushindwa kulinda uhai wa binadamu Mkoani Dar es Salaam. Mwanakwetu anajiuliza katika makala haya nini kimemkuta ndugu Albert mwana wa Chalamila mnyalukolo kutoka Lilinga(Ngome ya Mkwawa)? Au ndugu Chalamila kwa sasa anaogopa kutumbuliwa na kukaa benchi? Je kipi cha kufanya dhidi ya ndugu huyu?
Msomaji wangu twende taratibu, ngazi kwa ngazi nakuomba ukumbuke haya:
“Mkoa wa Dar es Salaam umeongozwa na Wakuu wa mikoa wengi tangu ulipoanzishwa mwaka 1930 ambapo awali ulianza kwa kujengwa makazi ya Sultan mwaka 1865 na kukamilika mwaka mmoja baadaye. Huku mkoa huu ukibahatika kuongozwa na Watanganyika na Watanzania kadhaa wenye asili ya Mkoa wa Lilinga(Iringa) akiwamo Bi. Merry Chipungahelo, Ndugu. Abasi Kandoro na baadaye Ndugu. Albert Chalamila.”
Msomaji wangu siku ya leo nakuomba ufahamu kuwa Mwanakwetu nilikuwa miongoni mwa watu niliosikitika sana mara baada ya Ndugu Albert Chalamila kuondolewa ukuu wa Mkoa wa Mwanza, huku nikikusanya maoni ya watu kadhaa wa Mwanza ambao walimzungumzia vizuri juu ya Ndugu Chalamila kutokana na tabia yake ya ucheshi mbele ya hadhira yake. Haya yalikusanywa katika sherehe za Bulabo nadhani mwaka wa 2022 ambapo Mwanakwetu niliambatana na Maafisa kadhaa Wizara ya Habari ambapo kiongozi mmoja wa kitaifa alikwenda Mwanza katika Tamasha hilo la Utamaduni wa Wasukuma.
Jamii ya Mwanza ilimzungumzia vizuri wakati ambapo tayari Albert Chalamila alikuwa ameshatumbuliwa amerudi nyumbani kwao Lilinga akinywa Ulanzi kutoka Ipogoro. Jambo la kushangaza ucheshi, wema, tabasamu la Albert Chalamila sasa limeangushiwa mzigo wa tuhuma:
“Kwa hakika majina ya watu waliotekwa, kupotea na kuuwawa wakati ndugu Chalamila Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam yako mengi moja tu ni la Ndugu yetu Ali Mohammed Kibao kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo mwili wake ulipatikana umefanyiwa vitendo vingi vya ukatili usiosimulika ambapo Ndugu Kibao alikuwa mwanasiasa tu, hatuwezi kusema alikuwa na ugomvi juu ya kugombea mke wa mtu, hilo abadani moja kwa moja kinachokuja akilini ni msimamo wake wa kisiasa ulimponza, Je Tanzania kuwa na msimamo wa kisiasa tafauti kosa nahukumu yake kifo.Mwaka 1992 kwani tuliruhusu vyama vingi? Kumbe Ile Ilikuwa Geresha Ya Danganya Toto Kula Kunde Mbichi!”
Yote haya yanafanyika Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni Ndugu Albert Chalamila, mpaka kesho hakuna majibu ya nini kilitokea? Nani kakamatwa? Kisa kilikuwa nini? Huku Albert Chalamila anaendelea kupokea mshahara wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania! Ati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama?
“Kwa hiyo linapotajwa jina Chalamila, kengele kichwani inalia kuwa Ali Kibao alitekwa na kuuwawa kipindi hiki hiki. Swali ni je Ndugu Chalamila binafsi anafahamu nini juu ya tukio hilo?Je Chalamila alichukua hatua gani kuhakikisha upuuzi huu kwa utu wa mwanadamu haujirudii tena katika eneo lake la utawala?Je watu wasiojulikana wamemfanya Chalamila kuwa babu wanafanya watakavyo? Mbona hawakuwafanyia hivyo akina Merry Chipungahelo na hata Abasi Kandoro?”
Kwa hakika hili ni jambo la kusikitisha:
“Ndugu Albert Chalamila, ebu fikiria wewe kama ni beki wa mchezo wa soka umekuwa hodari wa kupigwa darizi(Kanzu), matobo, chenga za dharau huku wewe ukiendelea kubaki mchezoni? Hauoni kuwa vitendo hivyo ni vya dharau kwa nafasi yetu wanavyovifanya hao wahuni katika eneo lake la utawala?”
Kwa hakika Dar es Salaam chini ya Bi Merry Chipungahelo na hata chini ya Ndugu Abasi Kandoro haya mambo ya kihuni hayakuwepo na hata kama yalitokea yalifanyiwa kazi kwa uhodari mkubwa.
Ndugu Albert Chalamila umekwama wapi?
Msomaji wangu mambo haya yanaumiza sana na kwa kuwa Ndugu Albert Chalamila ni Mkristo naomba nisimulie kisa hiki cha kweli pale Dola ya Baganda kati ya mwaka 1885-1887:
“Muzeeyi Kiwanuka alikuwa ni mjuzi wa tiba asili katika Ufalme wa Buganda, huku akiwa na nguvu sana ambapo alichukuliwa kutoka Minziro ambao sasa ni eneo la Tanzania kwenda katika makazi ya Mfalme kama mhudumu na mtunzaji wa bustani. Naomba ikumbukwe kuwa Kagera, Mara na hata sehemu ya Mwanza zilikuwa sehemu ya Dola la Baganda, baadaye huyu ndugu alikuwa Muisilamu wakati wa ujio wa Waarabu na baadaye akawa Mkristo. Wakati huo huo palipotokea kifo cha Kabaka Mwanga I na baada ya kifo hicho ndipo kukatokea migogoro mikubwa ndani ya ufalme huo kisha mtoto wa Kabaka akalithi kiti Kabaka Mwanga II, huku baadhi ya watu waliondolewa kufanya kazi katika ufalme huo kutokana sababu nyingi, hapa kukawa na patashika nguo kuchanika, huku na kule binadamu wakiwindwa kama wanyama na wale waliokuwa Wakristo walisakwa ili wauwawe pia akiwamo huyu Muzeeyi Kiwanuka.
Kabaka Mwanga wa II alikuwa mgeni wa utawala, umri mdogo na alikuwa hana uzoefu mkubwa ambapo Baba yake alikuwa uzoefu mkubwa na hata mahusiano mazuri, huku wasaidizi wake walitumia udhaifu huo kushauri mambo kadhaa ambayo yalikuwa ni hatari kubwa wa dola hii na yalikuwa na manufaa binafsi kwa wasaidizi hao.
Udhaifu huo na kuumizana wenyewe kwa wenyewe tamati Muzeeyi Kiwanuka akaandaliwa mtego ili akamatwe auwawe na kweli mtego ulikamilika na wakamkamata na kumtesa na kumpeleka machakani kumuuwa kwa siri kwa kumkata kichwa, huku kichwa hicho kikadumbukizwa kisimani.
Wakati hawa jamaa wa Mfalme wanatekeleza ufedhuli huu, Mungu Bahati kwa kando mama mmoja alikuwa msituni anaokota kuni, alipoona zile harakati mama huyu Mkristo ajibanza kwenye kichaka kimya hadi jamaa wanamalize zoezi lao kwa usalama wake. Walipomuuwa wakachukua udongo ambao ulikuwa na damu kutoka mwili wa Kiwanuka na kuutumbumikiza kisimani ili kupoteza ushahidi na kichwa chake kukidumbukiza humo humo na kisha mwili wakautupa kando ili uliwe na wanyama wakali, wauwaji wakaondoka zao. Mama huyu alijificha kwa muda mrefu msituni na baadaye alipoona kimya alichomoka msituni na hata kuni hakubeba na kurudi kwa Wamisionari na kuwaeleza kilichomkuta Muzeeyi Kiwanuka. Wakristo wakafunga safari hadi eneo la tukio na kweli walifika eneo la tukio walikikuta kichwa cha Muzeeyi Kiwanuka na kukibeba huku kikitirika damu mithili ya kwamba muuwaji alifanya tukio hili dakika chache, kumbe muda ulipita, kichwa kikabebwa, kusaliwa na kisha kuzikwa na nduguze Wakristo.”
Kisa hiki kinakwenda mbali zaidi hadi kuondolewa madarakani kwa Kabaka Mwanga II na yeye kiongozi huyu kupokwa madaraka ya Dola ya Baganda na akakimbilia Ushelisheli ,alifia huku huko ughaibuni na alizikwa huko huko, lakini baadaye sana mabaki ya mwili wake yalirudishwa Baganda kwa maziko mara pili.
Haya mwisho ni ya Buganda kati ya mwaka 1885-1887 kumbuka yale ya awali ni Dar es Salaam (Mzizima) nyumbani kwa akina Mwanakwetu na Mkuu wa Mkoa huo kwa mwaka wa 2025 Albert Chalamila.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika matukio ya mauwaji katika kipindi hiki tangu Chalamila awe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni mengi na Ndugu Chalamila yeye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Dar es Salaam. Je Ndugu Chalamila hafahamu chochote kwa kinachoendelea?
“Sikutaka kabisa kukugusia kutekwa kwa Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Kuba Ndugu Humphrey Polepole lakini hakuna namna, sikutaka kugusia matukio ya Oktoba 29, 2025 lakini hakuna namna Watanzania wamekufa na wana Dar es Salaammite wamekufa, Ndugu Chalamila anafahamu nini juu ya kilichotokea?Je wale jamaa wadunguaji mitaani walikuwa wanadungua Shole(ndege)?Wewe Mwneyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoani Dar es Salaam Unafahamu nini ? Umechukua hatua gani? Wapo watu wanaotajwa kwa majina yao, majina ya baba zao na majina ya babu zao na hata makabila yao wakituhumiwa kwa matukio kadhaa, je Ndugu Albert Chalamila umeshawaita hata mara moja katika kikao cha Kamati ya Ulinzi wa Usalama cha Mkoa wako na Je kuna nyaraka za ushahidi wa Kiserikali iwe leo, iwe kesho au kesho kutwa kuichwa hao ndugu au hatua ulizochukua zinaonekana?”
Kama hajafanya hivyo haoni kuwa Kamati nzima ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam haijatimiza wajibu wake na wao ndiyo watuhumiwa kwa kwanza katika haya haya yote kwa majina yao, majina baba zao na majina ya babu zao katika haya yote yanayoendelea?
“Ikumbukwe kuwa kila mmoja anapopewa majukumu majina yake matatu hutajwa: la lake mwenyewe, la baba yake na Babu yake, sababu ni nini? Ndugu Chalamila sababu kubwa ili uwezo kushitakiwa pale panapohitajika kufanywa hivyo.”
Kwako wewe mweyewe Ndugu Albert Chalamila na Kamati Nzima ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam nakuombeni mrejee kisa hiki cha mama huyu wa Kiganda aliyeshuhudia kifo cha Mezeeyi Kiwanuka(Mtakatifu) msituni kule Baganda, huyu mwanamke alikuwa mwenyewe na Mungu wake msituni alipotoka pale msituni salama bila shaka alimwabia mumewe, huo ndiyo Uafrika.
Mwanamke hawezi kulijua jambo la hatari haraka haraka akakurupuka na kuongea tu hadharani, wakakubalina na mumewe kisha wakafunga safari ndefu kwa siri hadi kwa viongozi wa kanisa jirani na walieleza kilichotokea hadi mwili wa Kiwanuka kupatikana na kuzikwa. Ndugu Chalamila wewe kama Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, wewe kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa mamlaka yako upo jirani na haya matukio kufahamu kinachoendelea, maana walio chini yako wanachunguza na wewe kukaa kimya maana yake wewe na wenzako hamjatimiza wajibu wenu.
Wadau wanasema mengi;
“Yeye tunajua anatoka Iringa, anakuja kutufanyia ufedhuli watu wa Dar es Salaam, yeye kama hodari kweli awe Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwao, akawafanyie haya yote kwa ndugu zake aone kama Wazee wa Lilinga(Iringa) watakubali na kama atabaki salama.”
Katika hili wapo wanaoamini kuwa Kanisa lina wajibu wa kupambana na hali hii kwa kushugulika na mtu mmoja, tangu wale waamini wake, muumini anayetuhumiwa aitwe katika Jumuiya yake akanywe, aitwe kwa Mchungaji/Padri wake, aitwe kwa Askofu wake akanywe huku akihojiwe anafahamu nini katika haya yanayoendelea na yeye binafsi amechukua hatua gani hadi sasa? Hili litasaidia kuzuia mambo haya ya kihuni kama yale yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata. Hapa Kanisa litaamua cha kufanya ikiwamo kuwanyima huduma za kiroho kwa mujibu wa sheria na kanuni za kanisa maana wameshindwa kupamba na wauwaji na kwa wale amabo siyo waamini wa Kanisa linaweza kuwasilina na viongozi wa dini husika kuwa Fulani Bini Fulani ndiye anayefanya haya kwa ushahidi kadhaa wa kadhaa achukuliwe hatua. Kama wapo viongozi wa chama na serikali wanashabikia hawa viongozi wa dini wasishirikiane nao.
Hali hii imemkumbusha Mwanakwetu hili:
“Balozi wa zamani Vatikani nchini Tanzania kati ya mwaka 1999-2005 alikuwa anaitwa Askofu Luigi Pezzuto ambaye alikuwa rafiki wa Mwanakwetu na kama angekuwa bado Balozi wa Vatikani nchini Tanzania Disemba 2025 hii ningemfuata Ubalozini kumpa ushauri huu kwa Wakatoliki hawa akina Albert Chalamila tungewawajibisha tangu ngazi ya jumuiya,Parokia/Ushariki, Jimbo/Dayosisi lakini kwa sasa Balozi wa Vatikani nchini Tanzania simfahamu hata jina lake, ngoja nitamuuliza Paroko wangu Padri Julius Ogolla anitajie jina lake ili niweze kumuuma sikio hili.”
Mwanakwetu Upo?Kumbuka:
“GERESHA, DANGANYA TOTO, KULA KUNDE MBICHI.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257




















Post a Comment